Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
WAKATI NHIF ikitangaza kuanza kwa matumizi ya kitita kipya kuanzia siku ya Ijumaa, Chama cha Wenye Hospitali Binafsi (APHFTA) kimetangaza tena kugomea kuwahudumia wanachama wa NHIF wakisema kuwa watapata hasara na hatimaye kufunga kutoa huduma.
Chama hicho kinasema kuanza kutumika kwa kitita hicho kutazifanya hospitali nyingi binafsi kufa kifo cha asili natural death kwani zitashindwa kujiendesha kutokana na kuongezeka kwa gharama za maisha huku gharama za matibabu zikishushwa.
Hospitali ambazo zinasemekana huenda zisipokee wagonjwa wanachama wa NHIF kuanzia tarehe moja March ni pamoja na Kairuki Mikocheni, TMJ, CCBRT, Masana, Regency, Rabinisia, Aga Khan, BOCH.
Taarifa ya chama hicho iliyosainiwa na Mwenyekiti wao, Dr Egina Makwabe leo imesema pamoja na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuunda kamati teule hawakushirikishwa na wala hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika kwenye kitita hicho kipya kama walivyolalamika kilipotangazwa hivi karibuni.
“Kitita kilianza kutumika mwaka 2016 na mpaka mwaka huu hakikufanyiwa mabadiliko yoyote licha ya gharama za maisha kuendelea kupanda, leo wanakuja tena kupunguza gharama za huduma badala ya kuongeza wanataka hospitali binafsi zife, badala ya kusaidia sekta binafsi wanataka kuiua,” alisema
“Kamati iliyoundwa na Waziri wa Afya ilikuwa kama geresha kwasababu ilikutana na BAKWATA tu na Chama cha Madaktari Tanzania MAT lakini sisi hawakutushirikisha wamekuja kutupa taarifa mwishoni kabisa baada ya kufanya maamuzi yaona hakuna kilichobadilishwa gharama zimeshushwa hospitali binafsi zitajiendeshaje” alihoji mmoja wa viongozi wa APHFTA
“Serikali yenyewe haina uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wote ndiyo maana imekuwa ikisisitiza ushirikishwaji wa sekta binafsi kupitia PPP lakini mbona wamegeuka tena wanataka kuua hospitali binafsi badala ya kuzisaidia,” alihoji kiongozi huyo
Alisema hata kamati teule iliyoundwa na Waziri Ummy Mwalimu isingeweza kufanya mabadiliko yoyote kwasababu NHIF iko chini yake na wasingeweza kufanya tofauti na anavyotaka yeye aliyewapa kazi.
“NHIF iko chini ya Wizara inayoongozwa na Ummy Mwalimu, kamati teule ya maridhiano imeundwa na Ummy Mwalimu kwa hiyo hapo kungefanyika nini kama siyo geresha tu ionekana kumefanyika mazungumzo na mambo yamebaki pale pale,” alisema kiongozi huyo.
“Kama wanavyotangaza kwamba tumezungumza tumefikia muafaka waulizeni wamezungumza nanani? Wamezungumza na BAKWATA tu na MAT sisi wamekuja mwishoni kabisa kutupa taarifa tu kwasababu wanajua kwamba iwapo wangetushirikisha tungekataa hicho kitita, sasa MAT wana hospitali?” alihoji
Alisema ujanja unaofanyika sasa utasababisha matatizo kwenye maisha ya watanzania kwani hospitali nyingi kubwa kubwa hazitaweza kupokea wanachama wa mfuko huo kwasababu ya gharama ndogo za malipo.
“Halafu kwenye taarifa yao wanasema kitita kipya kianze kutumika halafu wataendelea kupokea maoni ya wadaunsasa hata ukipokea maoni wakati ulishapitisha matumizi ya kitita itasaidia nini, kama unataka maoni si uyapokee kabla ya kuanza kwa matumizi ya kitita kwa hiyo ukiangalia hapa unagundua NHIF kuna vitu wanaficha ficha,” alisema
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benard Konga, ilisema kitita kipya kitaanza kutumika Ijumaa baada ya maoni ya wadau wote kusikilizwa.
Ilisema maboresho ya kitita yalifanyika mwaka 2016 miaka nane iliyopita hivyo kuwa na umuhimu wa kufanya maboresho mapya ikiwemo kuongeza huduma ambazo hazikuwepo kwenye kitita kipya.
Alisema mabadiliko ya gharama za huduma yamefanyika kulingana na maendeleo ya teknolojia na hali halisi katika soko kwa sasa.
“Lengo ni kuwianisha kitita cha mafao na miongozo ya tiba iliyoboreshwa ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wanufaika wa mfuko na mabadiliko haya yanalenga kujumuisha maoni na mapendekezo mbalimbali ya wadau,” alisema
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua