January 27, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Homera atoa agizo kwa watumishi wa afya

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema amechoka kusikia malalamiko ya kukosekana kwa dirisha maalum la kutolea huduma za afya kutoka kwa wazee, hivyo ameagiza wataalamu wa afya kuanzisha mara moja dirisha hilo.

Homera ameelezea masikitiko yake Februari 2,2024 wakati akisikiliza kero za wananchi kwenye viwanja wa stendi ya Kabwe jijini Mbeya.

Kufuatia malalamiko hayo ameagiza kila hospitali ya wilaya na maeneo yote ya kutolea huduma za afya yaliyoainiishwa kwenye sera kuwa na dirisha maalum la kutolea huduma za afya kwa wazee.

Amesema jambo hilo limekuwa likijirudia rudia bila kufanyiwa kazi, akieleza Kwa sasa uvumilivu umefika mwisho, hivyo ameitaka ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa kushughulia changamoto hiyo ili isijirudie tena.

“Hili jambo nalisema hapa ni mara ya mwisho sihitaji lijirudie tena, nataka hospitali zote zihakikishe kunakuwa na dawa pamoja na huduma za wazee kama ilivyoanishwa kwenye muongozo”amesema.

Awali Kiongozi wa Kimila Mkoa wa Mbeya, Rocket Mwashinga amesema bado kuna changamoto ya matibabu kwa wazee kwani baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya havitoi dawa na matibabu kwa kundi hilo na kusababisha usumbufu.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya Patrick Mwalunenge amesema chama kitafuatilia utekelezaji wa agizo la serikali kwa kufanya ziara ya kutembelea hospitali na vituo vya afya vyote ili kuona kama Kuna dirisha la wazee.