November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili

Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara

MKURUGENZI wa Shirika  lisilo la Kiserikali la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na kutetea haki za Wanawake na Watoto Mkoa wa Mara  Rhobi Samwelly amewataka Wazazi na walezi kuendelea kuweka misingi bora ya elimu kwa Watoto na kuwalinda dhidi ya vitendo vya Ukatili wa Kijinsia ili wasome na kufikia ndoto zao. 

Rhobi ameyasema hayo leo,Novemba 22, 2024, wakati akizungumza na Wazazi na Walezi  katika mahafali ya sita kwa  wahitimu wa Elimu  ya  Awali ya pili  katika  Shule ya Msingi St. John Bosco iliyopo Musoma.

Amesema,ili Watoto wafike mbali kielimu Wazazi na walezi wanalojukumu la kuhakikisha wanaimarisha misingi bora kwa  watoto wao kuanzia nyumbani ikiwemo kuhakikisha wanakuwa na nidhamu ya kupenda kusoma, kufuatilia maendeleo yao kitaaluma na kushirikiana na Walimu wao kwa ukaribu. 

Pia, amewahimiza Wazazi na Walezi kusimamia malezi na makuzi bora  ya watoto na kuwajenga katika  mafundisho ya kiroho na kuwaombea kwa Mungu ili  wafanikiwe kwa uwezo mkubwa kwa manufaa ya Jamii na Taifa pia.

“Tukemee pia vitendo vya ukatili wa Kijinsia kwa Watoto wetu na pia tuwalinde,tuweni makini na waangalizi wa Watoto wetu pamoja na kuachana na mila na desturi  mbaya dhidi ya watoto ukiwemo ukeketaji, ulawiti, vipigo visivyo na utaratibu. Lengo ni kuona Watoto  wanasoma vyema  na kufika mbali zaidi kwa manufaa yetu na Jamii pia.”amesema Rhobi. 

Akisoma risala ya shule hiyo Mwalimu Mkuu Msaidizi Simon Machango amesema, shule hiyo ilianzishwa rasmi  na Shirika la Liones Club  mwaka 1985, kama shule ya awali na mwaka 1993, shule hiyo ilikabidhiwa rasmi kwa Jimbo la Musoma chini ya usimamizi wa Masista wa Moyo Safi wa Maria Africa. 

Ameongeza kuwa,  Uongozi wa Masista  uliifanya  shule hiyo iwe ya kwanza kujulikana kama shule binafsi inayotoa huduma stahiki. Huku pia wakiiendeleza shule hiyo  ya awali kuwa Msingi. 

Amesema, jumla ya Wahitimu wa elimu hiyo ni 34,  ambapo wavulana ni 17 na Wasichana wakiwa ni 17.  Huku pia akitaja mafanikio kuwa ni pamoja na watoto kuwa na uwezo wa kusoma na kuandika kabla ya kuingia darasa la kwanza, madarasa yenye mazingira sanifu ya kujifunzia, vitabu vya kutosha vya kiada, kompyuta kwa ajili ya wanafunzi kujifunzia, Walimu mahiri na wenye weledi.

Rhobi amekabidhi msaada wa vifaa vya michezo ukiwemo mpira, na akabasi 30 kwa ajili ya wanafunzi kujifunzia shuleni hapo,huku pia akitoa wito kwa wanafunzi kusoma kwa bidii na malengo.