January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wasichana 246 waliokimbia ukeketaji wapewa hifadhi

Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara.

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya ukatili wa Kijinsia Mkoani Mara limewapokea Jumla ya wasichana 246 na kuwapa hifadhi katika vituo vyake vya  ‘Hope Mugumu nyumba Salama’ kilichopo Wilayani Serengeti na kituo cha Nyumba Salama kiabakari’ katika Wilaya ya Butiama  wakiwa wamekimbia kufanyiwa  ukeketaji  kuanzia Disemba mosi, 2024, hadi Disemba 10,2024.

Ambapo kituo kituo cha’Hope Mugumu nyumba Salama’ kimepokea Wasichana 45, kituo cha ‘Nyumba Salama Butiama’ kimepokea  Wasichana 189, huku Wasichana  120,  ni wale ambao wako Katika vituo hivyo wakipewa hifadhi kwa kipindi  kirefu.

Kutokana na hali hiyo, Shirika hilo limeiomba Jamii kuhakikisha inaungana pamoja kuwalinda Watoto wa kike katika Wilaya ambazo ukeketaji unafanyika sana hasa Tarime na Serengeti msimu huu wa mwezi Disemba 2024. Ambapo  wanafunzi wako likizo pia kubadilisha  mtazano na kuachana na mila na  desturi za kuwakeketa, badala yake wasomeshwe  kuja kusaidia Jamii na Taifa pia.

Mkurugenzi wa Shirika hilo (HGWT) linalomiliki vituo hivyo  Rhobi  Samwelly,ameyasema hayo Disemba 10,2024 wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia yaliyofanyika katika Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari na kuhusisha Viongozi wa serikali, Polisi,Asasi za Kiraia  na pia kutoka Mahakama ya Wilaya ya Butiama.

“Msimu huu ni wa ukeketaji,niiombe Jamii kuhakikisha inakuwa macho na chonjo kuwalinda Watoto wa kike wasifanyiwe ukatili huo,tumepokea idadi kubwa ya watoto ambao wamekimbia kutoka kwenye familia zao katika Wilaya za Tarime,  Serengeti na maeneo mengine na huenda idadi ikawa kubwa, tuwafichue mbele ya vyombo vya  sheria wote wanaobainika. Koo nyingi zinakeketa kipindi hiki tusiposhirikiana ukatili huo watafanyiwa binti zetu,”amesema Rhobi. 

Pia Rhobi amesema Wasichana hao wakiwa katika vituo hivyo watakuwa wakipewa msaada wa kisaikolojia, elimu ya hedhi salama, madhara ya ukatili, haki za Watoto,mahitaji yao ya msingi na kwa wale ambao wamekimbia wakiwa ni wanafunzi watakuwa wakipatiwa elimu ya ziada (Tuition) ili msimu wa ukeketaji uishe warudishwe makwao, na kwa wale ambao si wanafunzi, wataendelezwa katika fani mbalimbali za ujuzi ukiwemo ufundi.

Kwa upande wake Judith Semkiwa Hakimu  Mkaazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Butiama ameomba Wasichana hao kuendelea kujisimamia kipindi hiki  wakiwa  kituoni hapo. Huku akisema Mahakama  itaendelea kutoa ushirikiano kwa Wadau wote wanaopinga vitendo hivyo.

Naye Lilian Sospter kutoka  Asasi ya VSO amewapongeza Wasichana hao kwa kufanya maamuzi sahihi ya kukimbia kufanyiwa ukatili huo na Wazazi wao pamoja na ndugu zao na kwenda kupata hifadhi katika vituo hivyo ili wawe salama.

Huku akisema, madhara ya ukeketaji ni pamoja na kuathirika kisaikolojia, maumivu makali wakati wa kukeketwa, kutokwa damu nyingi, hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza, fistula na pia kuhatarisha maisha.