March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

HGWT yatoa wito jamii kuendelea kuwalinda watoto dhidi ya ukatili

Fresha Kinasa TimesMajira Online,Mara.

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya ukatili wa Kijinsia Mkoani Mara limetoa wito kwa Jamii kuendelea kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili  wa Kijinsia na kuimarisha malezi bora kwa Watoto wote kwa manufaa yao ya baadaye, jamii na Taifa pia.

Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania Rhobi Samwelly ameyasema hayo Juni 16, 2025,katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kituo cha  Nyumba Salama Kiabakari na kuwaleta pamoja  baadhi ya wadau wa  Mashirika yasiyo ya kiserikali na Viongozi wa Serikali wa Wilaya ya Butiama.

Pia, amesema,Shirika hilo limeendelea kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kutoa hifadhi kwa wasichana waliokimbia vitendo vya ukatili ukiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni,  kushirikiana na Serikali kupigania haki za Watoto,  kutoa elimu kwa Jamii ya madhara ya ukatili.

Aidha,amesema majukumu mengine yanayofanywa na Shirika hilo  ni kuwapa mafundisho ya kiroho, kuwajenga kisaikolojia na kuwaendeleza kitaaluma na  katika fani mbalimbali ili wapate ujuzi katika kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa  kujitegemea kimaisha kwa  siku za usoni.  

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Leopold  Constantine amepongeza jitihada zinazofanywa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania katika kuisaidia  serikali kuimarisha usawa wa Kijinsia, kutetea haki za watoto, kuwezesha kufikia doto zao na kuwalea katika maadili mema. 

Aidha Constantine,amewataka wasichana wanaopata hifadhi katika kituo cha Nyumba Salama Kiabakari, kusoma kwa bidii na kuhakikisha kila mmoja anajitahidi kufikia ndoto zake kwa manufaa yake, Jamii na Taifa pia.

Amesema,  Serikali itaendelea  kuwapa ushirikiano wa dhati kwani ipo kusimamia usalama na ustawi wao bora.Na ametoa wito kwa Wananchi kutoa taarifa haraka wanapoona viashiria vya ukatili ili kuvidhibiti kabla ya kufanyika.

Aidha, amewataka Wananchi na wale wote wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa Kijinsia kutokaa kimya badala yake watoe taarifa za vitendo hivyo kwa Viongozi mbalimbali kwa ajili ya hatua za kisheria.

Nao wasichana wanaopatiwa hifadhi katika kituo hicho wamesema, wanafurahi kuona huduma zote muhimu  wanazipata kituoni hapo. Na hivyo, wameahidi kusoma kwa bidii na kuwa mabalozi wa kupinga vitendo vya ukatili kwa kutoa elimu kwa wengine ili watambue madhara ya vitendo hivyo.