Fresha Kinasa TimesMajira Online, Mara.
MWENYEKITI wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali Tanzania Mwantumu Mahiza, amelipongeza Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) la Mkoani Mara kwa kazi nzuri ambazo linafanya ikiwemo kuwasaidia kuwapa hifadhi Wasichana wanaokimbia ukeketaji, ndoa za utotoni na kuwaendeleza kitaaluma ili watimize ndoto zao.
Mwantumu ameyasema hayo Januari 29, 2025, wakati akizungumza katika kikao cha Mkuu wa Mkoa huo Kanali Evans Mtambi na Viongozi mbalimbali wa Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ya Mkoa wa Mara kilichofanyika katika ukumbi wa Uwekezaji wa mikutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo Mjini Musoma.
“Mimi na timu yangu tumeguswa sana tulipotembelea Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania katika kituo cha Nyumba Salama Butiama linaloongozwa na Rhobi Samwelly, tumekuta kituoni kwake mabinti waliokimbia ukeketaji amewapa hifadhi, huduma mbalimbali, anawaendeleza kitaaluma, wengine vyuo mbalimbali Jambo hili ni jema sana kwani watoto hao wasingesaidiwa tujiulize wangekuwa wapi leo?”amehoji Mwantumu.
Amesisitiza Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali kufanya kazi kwa weledi na kwa uwazi zaidi katika kusaidia Jamii na Kutanguliza mbele uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao na kuachana na kasumba chafu za kuusema hovyo Mkoa na nchi kwa maslahi binafsi ya kujipatia fedha.
“Niwaombe, tuipende nchi yetu, msiichafue nchi mnapoomba misaada huko nje ya nchi. Wapo watu wanaumiza mikoa yao kwa ajili ya kupata fedha kutoka nje wanatoa taarifa za uongo, na mkipata mnatumia wenyewe tabia hii ni mbaya sana na chafu haifai kabisa, tusiseme uongo kwani nchi yetu siyo maskini kabisaa kiasi hicho ondoeni usiri katika kazi zenu.”amesema Mwantumu.
“Nimekuwa nikipokea sababu za baadhi ya Mashirika kufutwa sababu nyingine utakuta mwingine amesajili Shirika kwa kufuata mkumbo kwamba naye awe na Shirika, mwingine Shirika halikidhi vigezo hana Ofisi, halipi ada, hatoi taarifa. Mengine hayatambuliki na hayafanyi kazi Wala hayajulikani kabisa mfano Kuna zaidi ya Mashirika 13,000, yamesajiliwa nchini, lakini yaliyolipa ada ni zaidi ya 2,500 tu.” amesema Mwantumu.
Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza kuu la Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali Tanzania (NaCoNGO) Mkoa wa Mara ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) Rhobi Samwelly, ametoa wito kwa mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali Mkoa wa Mara kuimarisha  ushirikiano na Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema kuwa, Mkoa wa Mara unajumla ya Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali yapatayo 200 ambayo yamesajili, Hivyo yanalojukumu ya kufanya kazi kwa karibu na Serikali na kushirikiana kwa kila hatua badala ya kufanya kazi kimya kimya.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amesema serikali ya Mkoa huo inatambua kwa dhati kazi kubwa zinazofanywa na mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali katika kusaidia maendeleo kwa Wananchi.
Amesema, kazi mbalimbali zinazofanywa na mashirika hayo zimeendelea kupunguza matukio ya ukatili Mkoani humo, huku pia akisisitiza mashirika kutotumia NGOs kama kichaka cha kukwepa kulipa Kodi kwa huduma zao mbalimbali za kibiashara wanazozianzisha na kuziendesha.
More Stories
Bungua mweusi anayeshambulia zao la kahawa aibuka Bukoba
DED mpya Mbeya DC ataka watumishi kuwatumikia wananchi
Rais Samia kuzindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2024 Toleo la 2023