Na Esther Macha,Timesmajira Online-Iringa
BODI ya Shirika la Kimataifa la Helen Keller limefika kituo cha afya Isimani wilaya ya Iringa kujionea kwa vitendo zoezi linaloendelea la kambi ya upasuaji wa mtoto wa jicho ambayo itatoa huduma kwa siku saba wilayani humo.
Akizungumza wakati wa kikao kifupi Kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa Agosti 6,2025 Rais wa shirika hilo , Rais wa shirika hilo Sarah Bochie amesema shirika hilo limeamua kutembelea mkoani Iringa ili kujionea na kujiridhisha huduma zinazotolewa kwa vitendo kwani shirika lake linafanya kazi kwa kanzi data na takwimu ili kutoa tathimini ya huduma zake.
Kambi hiyo ya upasuaji mtoto wa jicho inaendelea kwa siku ya nne sasa na inafanya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa takribani wagonjwa 120 kwa siku katika zoezi linaloendeshwa na Madaktari Bingwa kutoka hospitali za nyanda za juu kusini ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Kheri James wakati akikaribisha ujumbe wa Bodi ya Wataalam kutoka Helen Keller Ofisini kwake ameshukru shirika la Helen Keller kwa kutoa msaada wa vifaa kila vinapohitajika, kutoa utaalam kwa madaktari wenyeji na kuendeleza ushirikiano kati yao na serikali.
Aidha Mkuu wa mkoa amesema lengo la ujumbe wa Helen Keller Mkoani Iringa ni kujionea namna gani huduma wanazofadhili zinavyofanya kazi ikiwemo kujadiliana kwa pamoja maeneo mengine ya ushirikiano kwani shirika hilo limekuwepo hapa nchini kwa zaidi ya miaka 30.
Kufuatia uwepo wa zoezi hilo katika Kituo cha Afya Ismani idadi kubwa ya wanachi wenye tatizo la mtoto wa jicho imeendelea kujitokeza ili kupata tiba hiyo huku wagonjwa wengi wenye umri wa miaka 50 na kuendelea wakiwa wanaongoza kwa kuwa na uoni hafifu hivyo kufanya idadi kubwa ya watu wenye umri mkubwa kufanyiwa upasuaji kwa wingi.
Dkt. Stephen Nyamsae Daktari Bingwa wa macho amesema ugonjwa wa mtoto wa jicho ni ukungu unaotokea katika kioo cha ndani ya jicho kutokana na kuongezeka kwa umri hasa kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 50 ambao taratibu hupoteza uwezo wa kuona.
Dkt. Nyamsae ametaja makundi mengine kuwa ni watoto wanaozaliwa na mtoto wa jicho kwasababu kabla ya kuzaliwa kioo hiki hushindwa kujitengeneza, kundi lingine analitaja kuwa ni la watu wenye ugonjwa wa kisukari lakini pia watu wanaopata majeraha katika jicho kutokana na ajali.
Zoezi la Kambi ya Upasuaji wa mtoto wa jicho linaendelea kwa siku 7 likitarajia kuhitimishwa tarehe 9 Agosti mwaka huu hivyo Wananchi waendelee kujitokeza kutumia fulsa hii kwani huduma hii inatolewa bure na imedhaminiwa na shirika la kimataifa lisilo la kiserikali la Helen Keller.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi