Na Jumbe Ismailly,TimesMajira Online, Igunga
KUNDI la tembo wanaokadiriwa kufika 800 wamevamia katika Kata ya Igoweko wilayani Igunga mkoani Tabora na kula hekari 66 za mazao ya chakula yakiwemo mahindi,mtama pamoja na mpunga na kusababisha kaya 50 za kata hiyo kukosa chakula.
Akitoa taarifa hizo kwenye mkutano wa baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga,Diwani wa Kata ya Igoweka,Omari Hamisi amefafanua kwamba, kundi hilo la tembo liliingia katika vitongoji viwili vya Igoweko “B”na Bugingija “D” na kula mazao ya wananchi waliokuwa hawajavuna na hivyo kusababisha kaya 50 kukosa chakula.
Kwa mujibu wa Hamisi kufuatia hali hiyo ndipo alipoiomba serikali kufika katika eneo hilo kwa ajili ya kuwatoa tembo hao ili wasiweze kuendelea kuleta madhara kwa wananchi sambamba na kuwalipa fidia wananchi walioathirika.
Naye ofisa Maliasili wa Wilaya ya Igunga,Jahulula Edward amethibitisha kundi la tembo hao kuvamia makazi ya watu na kuharibu hekari 66 za mazao ya chakula na kwamba kati ya hekari hizo,hekari 42 ni za mahindi,hekri 17 ni za mtama na hekari 7 ni za mpunga lakini hakuweza kutaja thamani ya mazao yaliyoathiriwa na wanyama hao.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam