November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole

Hekaheka za ubunge CCM zaanza rasmi

Makada kupigana vikumbo majimboni wakichukua fomu,

Polepole atangaza utaratibu wa kupata wagombea,

Walioanza kujinadi kwenye mitandao kikaangoni

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaanza kupigana vikumbo majimboni kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania Ubunge, Chama hicho kimetoa maelekezo ya Kikanuni na Kikatiba yanayotakiwa kufuatwa na wagombea hao, vinginevyo hawatateuliwa.

Utaratibu huo mpya wa kikanuni na kikatika ulitangazwa jijini Dodoma jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole wakati akizungunza na waandishi wa habari.

Kupitia mkutano huo Polepole ametangaza Kanuni na baadhi ya maboresho yaliyofanywa kwenye Katiba ya CCM ili kupanua wigo wa demokrasia kupitia Mkutano Mkuu wa CCM uliomalizika wiki iliyopita kwa ajili ya uchaguzi unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Amesema kanuni ya uchaguzi na uteuzi inazungumzia makatazo fulani fulani kuhusiana na mambo ya kulalamikia ambayo hayahusiani na rushwa.

Ametoa mfano wa matendo hayo kuwa ni matumizi ya mabango, vipeperushi vikiwemo vya kwenye mitandao au mabango. Polepole amesema vitendo hivyo haviruhusiwi na kwamba ni kosa, kwani kufanya hivyo ni kuanza kampeni kabla ya wakati.

Amesema makada wa Chama hicho ambao watabainika kufanya hivyo   wataadhibiwa na Kamati ya Siasa inayohusika. Pia Polepole amezielekeza Kamati za Siasa za Wilaya na majimbo kuwaelekeza wale ambao walikuwa tayari wamechapisha vipeperushi na mabango kuwaonya na kuwaelekeza kuyaondoa.

“Ninawaonya waache mara moja kutumia mabango na vipeperushi kabla ya mchakato wa uchaguzi,” amesema Polepole na kuongeza; “ambao hawataacha tutaona namna nzuri ya kuwasaidia.”

Pia amesema Kanuni zinaelekeza kuwa ni mwiko kutoa au kupokea rushwa, hivyo yule ambaye atathibitika kutoa rushwa hatateuliwa, kuwania nafasi hiyo.

Amesema wameielekeza TAKUKURU, ishughulike na makada wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kwani wanataka Chama chao kiwe cha mfano katika mapambano ya rushwa.

Polepole amesema zoezi la uchukuaji fomu na urejeshaji linaanza leo Julai 14 kwa upande wa wabunge na wawakilishi kwa viwango vilivyoainishwa kwenye fomu.

Amesema ni ruksa kwa Kamati za Siasa kuweka viwango vya michango kwa ajili ya kukichangia chama, lakini uchangiaji huo uwe wa hiari, hivyo mtu asinyimwe fomu kwa sababu ya kukataa kukichangia chama.

“Michango isitumike kumkatalia au kumkubalia mtu kumpa fomu,” amesema. Polepole alitaja gharama za fomu za udiwani ngazi ya kata kuwa ni sh. 10,000, lakini kiwango hicho hakizuii Kamati za Siasa kutengeneza michango kwa ajili ya kukichangia chama.

Kwa upande wa fomu za wagombea ubunge Polepole amesema ni sh. 100,000, lakini nao hawazuiwi au kulazimishwa kutoa michango ya hiari kwa ajili ya kukichangia chama.

Amesema hata fomu ya ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki gharama yake ni sh. 100,000 na kwa fomu za wanaotaka kuwania Uspika gharama zake ni 500,000 na urais ilikuwa ni sh. 1000,000.

Amesema jambo la pili ambalo limefanyiwa mabadiliko kwenye Katiba upanuliwa wigo wa demokrasia kwenye Katiba ni kuingiza wajumbe wapya kwenye Mkutano Mkuu wa Kata wa CCM.

“Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM umepanua wigo, kwa hiyo kuanzia sasa Mkutano Mkuu wa Kata utajumuisha wajumbe wapya ambao ni wenyeviti wa mashina (mabalozi).

Kwa sasa ni wajumbe wa mkutano mkuu wa kata wana dhamana ya kupiga kura kwani wao ndiyo wenyeji wa maeneo hayo wanaomjua mwana CCM  anayekubalika katika ngazi ya udiwani,” amesema Polepole.

Ametaja eneo lingine ambalo limefanyiwa mabadiliko kwenye Katiba ni wajumbe wa kupiga kura za maoni.

Amesema zamani mtu alikuwa anachukua fomu na kuanza kujadiliwa na vikao vya ngazi ya wilaya, mikoa na kuendelea na baadaye mgombea kupitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM.

“Tumeona mchakato huo unaminya demokrasia kwa hiyo Mkutano Mkuu wa CCM wa Taifa umefanya mabadiliko, sasa hivi watakuwa na safari moja ya mchakato wa uchaguzi na inaanzia kura za maoni katika eneo linalohusika na uchaguzi.

Inaanzia mkutano mkuu wa kata, watapiga kura za maoni ili wapate picha, wagombea watapata nafasi ya kujieleza. Baada ya kura kupigwa watachujwa kuanzia kamati ya siasa ya wilaya hadi mkoa ambapo watampata diwani,”amesema.

Kwa upande wa ubunge, amesema kutakuwa na mkutano wa jimbo, ambapo wagombea watajinadi kwa nini wanataka kugombea na baada ya hapo Kamati za Siasa za Wilaya zitaweka mapendekezo na kupendekeza watu watatu na sababu zao za kupendekezwa.

“Watakuwa wamejadiliwa wote na baada ya hapo mkutano wa mkoa Sekretarieti ya Taifa, kamati Kuu na Baadaye Halmashauri ya CCM itampitisha mbunge wa CCM,” amesema.

Kura kupigwa hadharani

Amesema mchakato wa zoezi la kupiga kura za maoni utakuwa hadharani kama ilivyokuwa wakati wa kuwapata wagombea Urais wa Muungano na Zanzibar.

“Masanduku yatawekwa mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu na wale waliogombea washiriki kuhesabu kura zao wenyewe. Tunataka mchakato wa uchaguzi uwe huru na wazi ili kuonesha demokrasia,”amesema.

Amewataka wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi zote wawe na mawasiliano ya haraka na ofisi ya Katibu Mkuu kama kuna jambo lolote la ufafanuzi.

Amesema kanuni ya uongozi na maadili ukurasa 18 inazungumzia haki na wajibu wa mwanachama, ambapo atakuwa na haki ya kugombea nafasi ya uongozi, lakini endapo kugombea nafasi nyingine kutasababisha kuzorota kwa uhai wa chama hatateuliwa.