January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Haya ndiyo yamedhihirishwa na Mkutano TCD, Rais Samia alivyokuza demokrasia

Na Jackline Martin,TimesmajiraOnline,Dar

BALOZI wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle, ameisifu Tanzania kwa kupiga hatua hivyo kwenye ukuaji wa demokrasia.

Amesema imekuwa ikipiga hatua vizuri, na wao (Marekani) wataendelea kuwa washirika wa Tanzania ili kusaidia kukuza demokrasia nchini.

Kauli hiyo ya Battle, aliyoitoa wakati wa mkutano wa wadau ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) uliofanyika wiki iliyopita.

Kauli hiyo ya Balozi, haikuja hivi hivi, bali ameitoa baada ya Taifa hilo kubwa duniani kujiridhisha na hatua zilizochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kukuza demokrasia nchini.

Kwa sasa hivi, ni wazi kwamba upungufu uliopo nchini upo katika sheria na jinsi ya kuzisimamia wakati wa uchaguzi, lakini pia chini ya uongozi wa Rais Samia, mchakato unaendelea.

Wapo wadau wa TCD wanaoweza kubeza kauli hiyo ya Marekani, kuhusu kuridhishwa na ukuzaji wa demokrasia nchini, lakini kwa waliofuatilia mkutano wa mwaka huu wa TCD, watakuwa mashuhuda, kwani sasa hivi Tanzania imepiga hatua kubwa.

Yale madai ambayo yalikuwa yakitolewa na wadau wa TCD, hasa wanaharakati na wanasiasa hayapo. Mfano vilio vingi vya wanasiasa vimefanyiwa kazi na kilichobaki ni Katiba mpya na marekebisho ya sheria ikiwemo ya uchaguzi.

Madai mengine ambayo yalikuwa kilio kikubwa cha wanasiasa wakati Rais Samia, akiingia madarakani hakikujitokeza kabisa mkutano wa TCD, mwaka huu na hicho ni kielelezo cha uongozi thabiti wa kiongozi huyo.

***Kuruhusiwa mikutano ya kisiasa

Wakati Rais Samia akishika wadhifa huo, Machi 21, mwaka 2021, kilio kimojawapo alichokutana nacho ilikuwa zuio la mikutano ya vyama vya siasa, lililowekwa mtangulizi wake, John Magufuli (mwaka 2016).

Chini ya uongozi wa Hayati Magufuli, vyama vya siasa havikufanya mikutano ya kisiasa kwa zadi miaka sita. Mazingira ya ufanyaji siasa nchini yalikuwa magumu na hiyo inadhihirishwa na kauli za viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani.

Mfano, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, mara kadhaa kwenye mikutano cha hadhara ya chama hicho, amekuwa akisema; “Chini ya uongozi wa Rais Magufuli, wengine hatukufa, lakini cha moto tulikiona.”

Lakini kutokana na Rais Samia kushamirisha demokrasia nchini, kwenye mkutano wa TCD mwaka huu hakuna mwanasiasa hata mmoja, aliyesimama kudai mikutano wa vyama vya siasa au kulalamika mikutano hiyo kuingiliwa na Polisi, maana inafanyika kwa uhuru tena kwa uhuru uliopitiliza.

Eneo hili, ni moja wapo ya maeneo yanayomsukuma Balozi Balozi wa Marekani Battle, kuisifu Tanzania akisema imekuwa ikipiga hatua vizuri kwenye suala la demokrasia.

***Kusahaulika mabomu ya Polisi

Kati ya mambo ambayo Watanzania wamesahau chini ya uongozi wa Rais Samia ni matumizi ya mabomu ya machozi yaliyokuwa yakitumiwa na Polisi kudhibiti wanasiasa nchini.

Tofauti hali ilivyokuwa chini ya uongozi wa awamu ya tano, Polisi walikuwa wakitumia mabomu ya machozi kudhibiti wanasiasa waliojaribu kufanya mikutano ya siasa.

Tangu Rais Samia, aingie madarakani hilo limesahaulika, Polisi wamekuwa wakilinda mikutano ya wanasiasa hadi kumalizika kwa amani.

Ushahidi wa hilo, ni kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na wapinzani, akiwemo Freeman Mbowe akisifu Jeshi la Polis kwa kuacha kutumia mabomu kudhibiti wanasiasa.

Alienda mbali zaidi na kushauri ikiwezeka mabomu hayo yakapelekwe Jamhuri ya Kidemokrasia na Ukongo (DRC), kwa sababu hapa nchini hayana kazi tena.

DRC kumekuwa na mapigano ya muda mrefu baina ya majeshi ya Serikali na vikundi mbalimbali vya waasi wakiwemo wa M23.

Kwa eneo hili, Balozi wa Marekani alikuwa na haki pamoja na kila sababu za nchi yake kuisifu Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia kwa ukuaji wa demokrasia.

***kufutwa kesi za wanasiasa wa upinzani

Kilio kingine ambacho alikumbana nacho Rais Samia mara baada ya kuingia madarakani, lakini hakikujitokeza tena kwenye mkutano wa mwaka huu wa TCD ni kuachiwa kwa wanasiasa, ambao kesi zao zilizokuwa na mwelekeo wa kisiasa.

Wanasiasa hao walikuwa wakikabiliwa na kesi hizo wakati wa kipindi cha uongozi wa Rais Hayati Magufuli. CHADEMA peke yake ilikuwa na wafuasi 400 waliokuwa wakikabiliwa na kesi za aina hiyo, ukiachia vyama vingine kama ACT Wazalendo na CUF.

Kupitia mazungumzo ya maridhiano wafuasi hao wa CHADEMA tayari wamefutiwa kesi zao kwa kufuata mfumo wa kisheria. Hii imedhihirishwa pia na viongozi wa vyama hivyo vya upinzani pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Kanali Abdurahman Kinana, ambapo alisema wafuasi wote 400 wa CHADEMA wamefutiwa kesi.

Dai hilo halikutokeza kwenye mkutano wa TCD, hivyo ni halali kwa Marekani kuisifu Tanzania kwa ukuaji wa Demokrasia.

***Waliokimbilia nje warejea

Kilio kingine kilichozoeleka ilikuwa ni wanasiasa waliokimbilia nje kutaka kuhakikishiwa usalama wa kurudi kwao. Dai hili, nalo halikujitokeza mkutano wa TCD, kwa sababu wote wamerudi na waliobaki nje, wamebaki kwa sababu zao binafsi.

Hiyo ni kwa sababu waliokimbilia nje kwa kuhofia usalama wao wakiongoza na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, wamerejea nchini.

Kwa sasa wanasiasa hao wanazunguka kila kona ya nchi, wakifanya mikutano, huku wengine wakiwa wamejipa uhuru uliopitiliza kuzungumza na wafuasi wao. Hili nalo ni moja ya maeneo yaliyoifanya Marekani iisifu Tanzania kwa kukua kwa demokrasia.

Ukiuliza wadau wote wa TCD kuhusu kukua kwa demokrasia nchini chini ya uongozi wa Samia, wengi watasema bila kumung’anya maneno kwamba demokrasia imekua, ukiacha kipindi fulani cha nyuma miaka michache iliyopita.

Itaendelea kesho