January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hatua zachukuliwa vituo vya mafuta

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandishi Timotheo Sanga kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa maendeleo ya makazi, Deogratius Kaliminze kwa kuandika waraka ulioleta taharuki na kupoka baadhi ya majukumu ya wizara ya ardhi.

Silaa aliongeza kuwa waraka huo umesababisha vituo vya mafuta kujengwa kiholela kwasababu waraka huo unadaiwa kurasimisha ujenzi wa vituo ambao hauzingatii matakwa halisi ya ukubwa na kwamba waraka huo ulisitishwa tangu Septemba 4, 2023.

Silaa ameagiza hayo leo mkoani Dar es Salaam alipokutana na wahariri na waandishi wa Habari katika kikao kazi akitoa taarifa ya utendaji kazi wa siku 100 za tangu alipoletuliwa kushika wizara hiyo.

Pia Silaa amewataka wananchi kuepuka kununua ardhi kwa Mwenyekiti wa Kijiji kwasababu hana Mamlaka hayo kisheria.

“Wapo wananchi wengi wananitafuta wananiambia nina mgogoro wangu wa ardhi , nilinunua kwa Mwenyekiti wa Kijiji.
Mwenyekiti wa Kijiji hana Mamlaka ya kuuza ardhi yoyote kwenye Kijiji, ardhi ya Kijiji ipo mikononi mwa wanakijiji wao wenyewe”

“Ukihudhuria mkutano wa kijiji, chukua video kupitia simu yako ili siku ukija kwenye malalamiko yako ya kudhurumiwa ardhi yako na Kijiji angalau uwe na ushahidi,” amesema Silaa.

Kuhusu urasimishaji, Silaa amesema kumekuwa na zoezi la urasimishaji linalofanyika nchi nzima , zoezi linalotakiwa kuisha mwaka kuu ambapo tayari wameliongezea muda wake hivyo liendele kufanyika katika maeneo yote nchi nzima ambayo tayari wananchi wanaishi.

“Katika zoezi la urasimishaji ni kama zoezi la kupanga na kupima na kama zoezi la upimaji shirikishi,”

“Niwatake wananchi kama unamiliki eneo lako ambalo ulilipima kwa miguu ukiamini ni 30 kwa 30 ambao unaamini mguu mmoja ni Mita Moja na unaamini ni square Mita 900 likija kutambuliwa ni square Mita 800 uwe unajiandaa kuwa unafanyika urasimishaji na ukikutwa una square Mita 800 zoezi likikamilika utajikuta umepata kiwanja Cha square Mita 650,” amesema.

Silaa amesema kuwa Wizara hiyo imeelekeza nchi nzima kufanyike kliniki ya ardhi na maeneo yote wameelekeza kuanzia Januari 2024 kutokana na ratiba itakayopangwa wahakikishe kwamba kila kliniki inayofanyika kwenye mkoa, viongozi wakuu wa wizara wawe wanapatikana kwenye eneo hilo.

Aidha amesema wamekubaliana baina ya Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kuangalia ratiba itakayopangwa mkoani na wawasimamie makamishna wasaidizi wapange ratiba ambayo itawawezesha kila mmojawapo kati yao kuweza kushirikiana na kuwasikiliza wananchi wa Mkoa husika kwenye kliniki hiyo au Wilaya husika .

“Maeneo mengine wakuu wa Idara wa makao makuu ya Wizara na wao wapate fursa ya kwenda ili kwenda kutengeneza sura ya kutatua yale ambayo yamekuwa yamewazidi kimo viongozi wale wa mikoa na Wilaya husika wa Sekta ya ardhi”

“Kwenye kliniki wapo wanaokuja ambao tayariwa lalamikiwa wao ndiyo haohao watendaji wa ardhi kwenye Wilaya na mikoa husika, hivyo kukiwa na viongozi wa wizara kutasaidia wananchi kuweza kueleza matatizo yao na kupata huduma stahiki,” amesema.

Silaa amesema Wizara imejipanga kufanya mabadiliko kwenye Wizara ya ardhi nyumba na maendeleo ya makazi ikiwemo kufanya mabadiliko ya kisera, kisheria na kikanuni, ili kuweza kukidhi mahitaji ya sasa na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Tumedhamiria kuwa na mpango mkubwa wa kupanga na kupima maeneo yote ya nchi yetu, kwani Kasi ya ukuaji wa miji / mahitaji ya makazi inakua kubwa kuliko Mipango ya ndani ya wizara ya kuhakikisha wanafanya kazi ya kupanga na kupima maeneo,”

“Tumewaelekeza wataalamu wote nchi nzima kuhakikisha wanafanya upimaji wa awali , pia tutaendelea na mradi huu wa KKK katika sura iliyoboreshwa kwa Halmashauri zote zenye Nia ya kupanga na kupima maeneo yao , kuandika maandiko ili kujua tija yake katika mpango wa kupanga na kupima na upimaji shirikishi,”amesema.