Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza
WANANCHI wametakiwa kuchukua tahadahari kwa kufungua madirisha, kutokuwasha taa,feni wala friji(jokofu) endapo kutakuwa na kiashiria cha kuwa mtungi wa gesi ya kupikia nyumbani umevuja,ili kuepuka na madhara yanayoweza kutokea.
Huku wakishauriwa kutumia mchanga badala ya maji kuzimia moto endapo kwa bahati mbaya itakapotokea ajali ya moto iliosababishwa na kulipuka kwa gesi.
Hayo yamezungumzwa na Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji(EWURA),Kanda ya Ziwa George Mhina,wakati wa mahojiano na Majira ofisini jijini Mwanza, alisema wanapokuwa wamehisi kuwa gesi imevuja wanapaswa kuchukua tahadhari.
Mhina amesema,hatua za kuchukua endapo utahisi gesi yako imevuja ni kuhakikisha unafungua madirisha ili kuruhusu hewa itoke,usiwashe taa,feni,friji(jokofu) na baada ya hapo toa mtungi wako wa gesi nje na anza kuchunguza kama inavuja.
Amesema endapo kwa bahati mbaya ikatokea ajali ya moto iliotokana na gesi kulipuka basi wananchi watumie kifaa maalum cha kuzimia moto (fire extinguisher) ingawa katika maisha ya kawaida si rahisi kuwa nayo hivyo wanashauri watumie mchanga kuzima moto huo.
“Tunakataza watu wasitumie maji kwa sababu maji muundo (composition) wake una oksijeni ambayo ni chakula cha moto,ndio maana inapotokea hata gari imelipuka unaambiwa kama una blangeti funika ili kuondoa oksijeni,kwaio tunasisitiza watu watumie mchanga zaidi endapo itatokea moto umeanza kuwaka kuliko kutumia maji,”amesema Mhina.
Pia ameendelea kusisitiza kuwa wananchi wachukue tahadhari kwa kuhakikisha usafirishaji wa gesi ni mzuri,mtungi hauvuji mahali pa kuhifadhia gesi ni salama na kuweka mbali na vyanzo vingine vya moto au hakuna shughuli za uchomoleaji au za mioto angalau kwa umbali kidogo.
Na wanaponunua gesi wahakikishe mtungi hauna mvunjo na kizibo chake kiwe kimeziba vizuri,ili kujua kama una vuja au hauvuji wanaweza kuchukua povu la sabuni wakamwagia kwenye mtungi wao na kuweza kubaini kama hupo sawa.
“Mtungi wa gesi unatakiwa usafirishwe ukiwa wima ingawa kwa Watanzania usafirishaji wake ni mgumu na ukifika nyumbani kama umesafiri kwa umbali kidogo hakikisha una upumzisha mtungi hata dakika tano kabla ujaanza kuutumia,”alisema Mhina
Aidha amesema,EWURA wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi kuhusiana na matumizi sahihi ya gesi ya kupikia,ambayo imekua ni nishati yenye faida nyingi kuliko nishati yoyote ya kupikia lakini usipoitumia vizuri inaweza kuleta madhara na maafaa.
More Stories
Tanzania,Uturuki kushirikiana kuinua sekta ya utalii nchini
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu