Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Handeni
VIONGOZI wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya Shirika la World Tanzania kwenye Tarafa ya Mkumburu (Mkumburu AP) baada ya kufanya ziara ya kutembelea miradi iliyotekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja 2023/2024.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Jasmin Julius ndiyo aliongoza jopo la viongozi Disemba 16, 2024 waliotembelea miradi kwenye tarafa hiyo wakiwemo madiwani, Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, viongozi wa Mkumburu AP ngazi ya jamii na dini.
Julius amesema Mradi wa Maji Kwedizinga uliopo Kijiji cha Kwedizinga, Kata ya Kwedizinga, ni kielelezo cha kazi zilizotukuka za Shirika la World Vision, kwani zaidi ya wananchi 4,486 watanufaika na mradi huo na kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji.
Makamu Mwenyekiti, pia alimpa kongole mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kwedizinga Shania Shaaban ambaye alikuwa chachu ya kupata mradi huo wa maji, kwani akiwa mwanafunzi wa kidato cha pili, na akiwa na miaka 15, alikuwa Balozi wa Mazingira wa Shirika la World Vision, na lilimpeleka kwenye Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi nchini Misri (COP27- Egypt2022).
Akiwa huko ndiyo alipokutana na Shirika la We Are Water la nchini Hispania, na kuwaeleza kijiji chake cha Kwedizinga kina shida ya maji, hivyo anaomba wamsaidia, ndipo shirika hilo kwa kushirkiana na World Vision walipojenga mradi huo wa maji.
“Niwapongeze Shirika la World Vision kwa jitihada zenu za kuisaidia jamii hasa kwenye suala la maji. Kwa kuwepo mradi wa maji hapa, utasaidia jamii iliyopo eneo hili. Na sisi kama viongozi, tumeridhika na utekelezaji wa miradi kwenye Tarafa ya Mkumburu, lakini pia kwenye Tarafa ya Kwamsisi” alisema Julius ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kwasunga iliyopo Tarafa ya Kwamsisi,”amesema.
Diwani wa Kata ya Kwamsisi Hamis Juma amesema analishukuru Shirika la World Vision kwa ujenzi wa miradi ya huduma za jamii ikiwemo, afya, elimu na maji, kwani kwenye elimu, pamoja na mambo mengine, wameweza kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, na jambo hilo limeongeza ufaulu kwa wanafunzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Juma amewataka Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) kuongeza ujenzi wa miundombinu ya maji, kwani wilaya hiyo bado inakabiliwa na shida ya maji.
Naye Afisa Kilimo Kata ya Kwamsisi Mohamed Mbwana aliwashauri kikundi cha Kuweka na Kukopa cha Upendo kilichopo Kijiji cha Taula ambacho kilipewa elimu na World Vision, na sasa kikundi hicho wanaweka hadi sh. milioni 22 kwa mwaka, huku wakiwa na mradi wa kutoa huduma ya maji kwa wananchi, waweze kujiweka kwenye mfumo wa kukopa fedha za halmashauri.
Akisoma taarifa ya Mradi wa Maji Kwedizinga, Msimamizi wa Miradi ya Elimu na Uchumi wa Kaya, Mkumburu AP, Steward Mwilenga alisema mradi huo uliibuliwa na wanajamii wenyewe kutokana na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama, na utekelezaji wake ulianza mwaka 2023-.2024.
“Mradi huu wa usambazaji maji katika Kijiji cha Kwedizinga umetekelezwa katika awamu moja kwa hatua mbili kwa kutumia Wakandarasi wawili. Wanufaika wa moja kwa moja ni wananchi 3,890, na wanufaika wasio wa moja kwa moja ni 596, hivyo jumla kuwa wananchi 4,486″amesema Mwilenga.
Mwilenga amesema mradi huo uliogharimu sh. 245,886,900 ni wa kisima kirefu, na umejengewa tenki la lita za ujazo 50,000, mabomba ya usambazaji maji yenye urefu wa kilomita 4.3, vilula 10, ujenzi wa pump house, ununuzi wa Solar kwa ajili ya kusukuma maji.
Naye Napoleon Mlowe, Afisa Maliasili Halmashauri ya Wilaya ya Handeni,amesema Shania ni lazima akumbukwe kwa kuweza kuita chochote kwa jina lake kwenye Mradi wa Maji Kwedizinga iwe kumbukumbu kwa vizazi vijavyo, lakini kuwatia moyo watoto wa kike wengine wanaokuwa, kuwa kila mmoja hapa duniani ana talanta yake.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais