March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri zakopeshwa bil.2.8 kutatua migogoro ya ardhi Mara

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutambua uwepo wa changamoto ya migogoro ya ardhi, imezikopesha halmashauri jumla ya shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya zoezi la kupanga, Kupima na kumilikisha ardhi kupitia Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Kanali Evans amesema hayo jijini hapa leo Julai 18,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Amesema kuwa Mradi umesaidia kupunguza migogoro ya ardhi kutoka 964 mwaka 2020 hadi migogoro 125 mwaka 2025, kuongeza utoaji wa hati miliki za ardhi kutoka 1,405 hadi 5,867, kuongeza utoaji hati miliki za kimila kutoka 1,200 hadi hati 8,670 mwaka 2025 na kuongeza vijiji vyenye mpango wa matumizi bora ya ardhi kutoka 35 hadi vijiji 218.

Akizungumzia mafanikio ya Mkoa huo Kanali Evans amesema kuwa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ilipo katika Mkoa huo imeanza kuzalisha gesi tiba ya oksijeni kwa ajili ya kutoa huduma kwa wateja wanaohitaji huduma ya gesi tiba pamoja na kuhudumia vituo jirani.

“Uwepo wa hospitali hii pamoja na uboreshaji mkubwa uliofanywa katika vituo vya kutolea huduma za afya umesaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kutoka Mkoa wa Mara kwenda Hospitali ya Kanda Bugando kwa asilimia 70,”amesema  

Vilevile amesema Serikali imeongeza fedha za kuwezesha elimu bure kutoka shilingi bilioni 5.6 mwaka 2020 hadi shilingi bilioni 7.5 mwaka wa fedha 2025 kwa shule za msingi na kutoka shilingi bilioni 6 hadi bilioni 12.85 mwaka 2025 kwa shule za Sekondari.

Aidha amesema Mkoa wa Mara umetekeleza miradi mikubwa tisa kupitia Shirika la TANESCO na REA kwa gharama ya shilingi bilioni 435.1 kwa ajili ya maboresho ya vituo vya kupooza umeme na mifumo ya usambazaji umeme katika maeneo ya wachimbaji wadogo na maeneo ya wananchi.

“Hadi kufikia mwezi Juni, 2025 wilaya zote sita, Halmashauri tisa, Kata 140, Vijiji 458, Mitaa 242 na vitongoji 1,555 kati ya 2,502 vimewekewa umeme ambayo ni sawa na asilimia 62 ya Vitongoji vyote,”amesema.

Pia amesema Serikali imetekeleza miradi ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 426.3 kupitia Wakala wa Maji Vijijini, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma na Mamlaka ya Maji ya Mgango- Kiabakari.

“Miradi mikubwa ya maji mkoani humu ni pamoja na mradi wa Mgango -Kiabakari- Butiama wenye thamani ya shilingi bilioni 70.5 ambao umekamilika, Rorya-Tarime wenye thamani ya shilingi bilioni 134.4 ambao umeanza kutekelezwa na mradi wa Mji wa Mugumu wenye thamani ya dola za marekani milioni 8.75 ambao umeanza kutekelezwa.
 
“Upatikanaji wa maji safi na salama vijijini umeongezeka kutoka asilimia 54 mwaka 2021 hadi asilimia 81 Juni, 2025. Upatikanaji wa maji safi na salama katika miji unaridhisha na hadi kufikia Juni, 2025 upatikanaji wa maji katika Manispaa ya Musoma ni asilimia 98, Mji wa Mugumu asilimia 67, Mji wa Tarime asilimia 77 na Mji wa Bunda ni asilimia 86,”amesema.

Pamoja na hayo amesema kuwa Uchumi wa Mkoa wa Mara umeendelea kuimarika ambapo pato halisi limeongezeka kutoka shilingi trilioni 5.3 mwaka 2020 hadi tririoni 6.8 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 28.3 kwa mwaka.

“Hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2025, shilingi trilioni 1.3 zimetolewa na Rais Samia kwa ajili ya kutekeleza miradi katika sekta mbalimbali ndani ya Mkoa wa Mara,”amesema.