Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Tunduma.
KATIBU Tawala Mkoa wa Songwe, Happness Seneda, ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Mji Tunduma, kufuata taratibu za kisheria ili kuvunja mkataba na Mkandarasi wa kampuni ya ujenzi ya Chillisam ya Jijini Dar as salaam kwa kushindwa kutekeleza mradi kwa wakati.
Mkandarasi huyo anayejenga vyumba vya madarasa kupitia mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) katika shule ya sekondari Chipaka iliyopo Kata ya Chipaka wilayani Momba kwa gharama ya milioni 583.
Seneda ametoa maelekezo hayo Oktoba 16 , 2023 baada ya kutembelea ujenzi huo wa vyumba vya madarasa na kuonesha kutoridhishwa na kasi ya Mkandarasi huyo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika Halmashuri ya Mji Tunduma kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Hilo suala la tofali sitaki kusikia kwa sababu wewe umepewa ‘full contract ‘ hivyo hatutaki kusikia hizo habari nyeusi kwa kasi hii huyu hatuwezi kwenda nae, kikubwa angalieni taratibu kisha mvunje mkataba,” ameelekeza Seneda.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Ujenzi Halmashauri ya Mji Tunduma, Matha Zacharia,ameeleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa dhidi ya Mkandarasi ikiwemo kumuandikia onyo mara mbili jambo ambalo linatoa nafasi na mazingira mazuri kwa halmashauri hiyo kuweza kuvunja mkataba.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri hiyo, Burton Nisile,amesema alipewa siku 60 za kutekeleza mradi huo na kazi alizopewa kutekeleza Mkandarasi huyo kuwa ni vyumba vya madarasa nane, majengo mawili ya maabara kwa ajili ya masomo ya Fizikia,Kemia, Jiografia na Baiolojia.
Ametaja kazi nyingine kuwa ni ujenzi wa jengo la utawala, maktaba,maktaba ya tehama, vyoo matundu nane, kichomea taka pamoja na tanki la maji la ardhini.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua