Na Lubango Mleka, TimeMajira Online Musoma Vijijini.
WANANCHI wa Kijiji cha Nyasaungu Kata ya Ifulifu Halmashauri ya Musoma mkoani Mara, wameiomba Halmashauri hiyo kuchangia ujenzi wa shule ya sekondari Nyasaungu ili kupunguza adha kwa wanafunzi wa kijiji hicho kukosa elimu.
Hayo wamebainisha katika ziara ya Mbunge wa Jimbo Musoma Vijijini Prof.Sospter Muhongo ambaye ametebelea Kata ya hiyo kwa lengo la kukagua na kutathimini utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Miradi inayotekelezwa kijijini hapo ni pamoja na ujenzi wa sekondari ya Nyasaungu,zahanati na uboreshaji wa miundombinu ya elimu shule ya msingi Nyasaungu.
Baadhi ya wananchi wa Kata hiyo akiwemo Mariam Jacob,amesema kutokana na juhudi zao wananchi za kujitoa katika ujenzi wa sekondari hiyo wanaiomba halmashauri hiyo iwaunge mkono kwa kuchangia ujenzi wa shule hiyo ambayo watumiaji wake wengi watakuwa watoto wa wafugaji na wavuvi wa kijiji cha Nyasaungu.
“Kata yetu bado kuna upungufu mkubwa kwenye upatikanaji wa maji, umeme, chakula kutokana na ukame ulio vikumba vijiji vingi, upungufu wa walimu katika shule ya Msingi Nyasaungu na ukosekanaji wa shule ya Sekondiri, tunakuomba mheshimiwa Mbunge wetu utusaidie juu ya kilio chetu hiki,” amesema Masingili Michael.
Aidha, wananchi hao wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wao kwa kuchangia kiasi kikubwa ujenzi wa sekondari Kata ya Ifulifu.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof.Sospter Muhongo ameahidi kuendelea kuchangia ujenzi huo kama alivyofanya hapo awali kwa kutoa mifuko ya saruji na mabati ili ujenzi huo ukamilika kwa wakati uliokusudiwa.
“Kijiji cha Nyasaungu ni moja ya vijiji vitatu vya kata ya Ifulifu, kijiji hiki kiko pembezoni na mbali na vijiji vingine vya kata hii, vilevile jiografia yake ina mito na vichaka, inakifanya kuwa na ugumu wa kufikika hasa wakati wa mvua na mazingira haya ni hatarishi kwa wanafunzi,” amesema Prof.Muhongo.
Ujenzi wa Nyasaungu sekondari umeanza kwa kutumia michango ya wanakijiji, Mbunge,serikali na Mfuko wa jimbo, ambapo mpaka sasa ujenzi umefikia hatua ya ukamilishaji wa vyumba 3 vya madarasa, choo cha matundu 6 na jengo la utawala na matarajio ya wananchi ni kufikia januari 2024 shule iwe imefunguliwa na watoto kuanza kusoma.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa