January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri ya Mji Ifakara kuburuzwa mahakamani

Na mwandishi wetu, Timesmajira Online

HALMASHAURI ya Mji Ifaraka, inatarajiwa kufikishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro kutokana na kuvunja mkataba wa Kampuni ya ukandarasi ya Harmony Memorial iliyepewa zabuni ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Lipangalala iliyopo mjini Ifakara.

Akizungumzia hilo leo, wakili wa mkandarasi huyo, Gaston Chundu amesema baada kukamilisha taratibu anatarajia kufungua kesi hiyo baada ya siku tatu.

Chundu amesema, katika kesi hiyo mteja wake anadai Sh. milioni 204, ambazo zilitokana na madhara kubwa ya halmashauri kuvunja mkataba bila kufuata taratibu za kisheria.

Amesema, mkataba huo uliokuwa uanze Septemba hadi Desemba 2023, ulivunjwa akiwa ameanza kazi za ujenzi, huku akiwa ameshaanza kutumia gharama.

Wakili huyo, amesema kwa kuwa mteja wake alitumia fedha nyingi, ikiwa ni pamoja na kukodi vifaa, fedha zake kukaa muda mrefu bila kuwemo kwenye mzunguko ndio sababu iliyosababisha kuifikisha halmashauri mahakamani ili iweze kutafsiri sheria.

“Halmashauri imevunja mkataba wa mteja wangu kabla ya siku 90 ambazo alipewa zabuni ya ujenzi wa shule. nitahakikisha haki inapatikana mahakamani, amesema Wakili Chundu.

Pia, amesema kwa kuwa upande mmoja umevunja mkataba kabala ya miezi mitatu sasa ipo haja ya makusudi ya kuitaka mahakama kutafsiri sheria ili haki iweze kutendeka katika hilo.

Chundu amesema, kutokana na hilo mahakama itajua nani mwenye haki, kwa kuwa mkataba ulivunjwa bila kufuata taratibu za kisheria na mteja wake ameathirika na kiwango kikubwa.

“Kitendo kilichofanywa na halmashauri cha kuvunja mkataba wa mteja wake sio sawa na ninamsaidia kupata haki yake,” amesema wakili huyo.

Hata hivyo Timesmajira ilifanya jitihada za kuwasiliana na Mkurugenzi wa Mji Ifakara, Zahara Michuzi, ili kupata ukweli wa madai hayo, hakuweza kutoa ufafanuzi baada ya simu yake kukata, hata ilipomrudia hakupokea simu.