December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri ya jiji la Tanga kutumia bilioni mbili mwezi Februari

Na Hadija Bagasha TimesMajira Online, Tanga

HALMASHAURI ya jiji la Tanga itatumia shilingi bilioni mbili kuanzia mwezi Februari,miradi inayogusa makundi mbalimbali ya kijamii kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana.

Kadri majiji yanavyokuwa kwa haraka watoto na vijana waliopo mijini wanajikuta katika mazingira yasiyo rafiki kwa maendeleo yao.

Hii ni kwa sababu upatikanaji wa huduma muhimu za kibinadamu kama vile elimu afya ,maji safi na makazi salama hazikidhi mahitaji yao.

Shirika la Foundation Botnar la nchini Uswizi kwenye mkutano maalumu wa baraza la madiwani wa halmashauri ya jiji la Tanga linaeleza mpango wa kufadhili miradi ya maendeleo kwenye jiji hilo.

Dk.Hassan Mshinda ni Mwakilishi wa Shirika la Botnar Foundation amesema taasisi hiyo tangu mwaka 2018 imekuwa ikishirikisha wadau mbalimbali katika kutambua changamoto zinazowakabili vijana wa Tanga kwa kuwa wanatambua umuhimu wa kujenga mifumo bora ya miji inayotoa kipaumbele kwa mahitaji ya watoto na vijana.

Dkt.Mshinda amesema zaidi ya bilioni 2 zitatumika katika utekelezaji wa miradi ijayo inayotarajiwa kuanza mwezi Februari na machi 2022.

Aidha miradi hiyo ni pamoja na uendelezaji wa bustani ya jamhuri park (Forodhani),utengenezaji wa viti na meza kwa shule za sekondari,utengenezaji wa madawati kwa shule za msingi ,utengenezaji wa vyoo kwa shule za msingi na sekondari,Mradi wa mabadiliko ya kifikra na ujasiriamali.

Pia kuwajengea vijana ujuzi na maarifa ya kidigitali ili kupata kazi za kimtandao,kuwezesha vijana katika mnyororo wa thamani ya ufugaji wa kuku,uwezeshaji wa vijana kiuchumi kupitia mradi wa uvuvi na ununuzi wa boti 12 ili kuwezesha vijana kufanya uvuvi wenye tija.

Meya wa jiji la Tanga Abdarahaman Shiloo anasema miradi hiyo inaenda kuleta badadiliki chanya ya kiuchumi kwa wakazi wa jiji la Tanga na hususani vijana wenye uhitaji mkubwa ajira.

Meya Shiloo ameipongeza kamati ya uongozi ya Botner pamoja na wote waliowezesha mradi huo kuja jiji la Tanga na kueleza kuwa tangu Botner ilipoanza mahusiano na jiji la Tanga tayari imefanya miradi ya kuwajengea uwezo baadahi ya viongozi na watendaji katika jiji.

Kupitia mradi huo wa Tanga yetu ,miradi itakayofanywa ni ile inayohusiana na elimu ,uvuvi,barabara na kwamba miradi hiyo imekuja baada ya kushirikishwa kwa wadau mbalimbali wanaotambua changamoto vinazowakabili vijana.