February 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri Tunduma kikaangoni



Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.

MKUU wa Mkoa wa Songwe,Daniel Chongolo, ameikalia kooni Halmashauri ya Mji wa Tunduma kwa kushindwa kulipa madeni ya wazabuni,ambayo yanadaiwa kufika shilingi bilioni 1.8 tangu mwaka 2019, hali inayosababisha malalamiko mengi.

Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Maendeleo ya Mkoa (RCC) kilichofanyika Februari 19, 2025, kwa ajili ya kupitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26, Chongolo alionesha masikitiko yake kwa hali hiyo na kuhoji sababu ya kuchelewesha malipo ya madeni hayo.

“Lipeni madeni ya watu!…najua mlihitaji huduma hizi kwa sababu zilikuwepo kwenye bajeti, sasa hela ilienda wapi” alihoji kwa msisitizo.

Chongolo alisisitiza kuwa, wazabuni hao walitoa huduma kwa nia njema, lakini sasa wanakumbwa na hali ngumu, ikiwa ni pamoja na kushindwa kulipa mikopo yao ya benki.

Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mariam Chaurembo,Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu Halmashauri ya Mji Tunduma,Emmanuel Shija, alieleza kuwa baada ya uhakiki, deni halali lililobaki ni shilingi bilioni 1.01.

Alibainisha kuwa halmashauri hiyo imeanza kulipa, ambapo shilingi milioni 270 zimetengwa kupitia mgawo wa fedha wa dharura (reallocation), na kwamba kwenye bajeti ya mwaka huu pia Halmaahauri hiyo imependekeza kulipa shilingi milioni 370.

Mbali na madeni ya wazabuni,Chongolo pia alimbananisha Mkurugenzi Chaurembo kuhusu madai ya watumishi.

Hata hivyo, kupitia Ofisa Utumishi, Gilbert Mbowe, alieleza kuwa hakuna madeni ya watumishi isipokuwa malimbikizo ya mishahara, ambayo tayari yameingizwa kwenye mfumo kwa ajili ya kushughulikiwa.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa alilazimika  kumtoa nje ya ukumbi Mkurugenzi huyo pamoja na wataalamu wake ili wakae ‘chemba’ na kupanga taarifa yao kwa mtiririko unaoeleweka na kuiwasilisha upya ili iingie kwenye kumbukumbu za kikao hicho.

Chongolo alihitimisha suala hilo,  aliagiza halmashauri hiyo na Halmashauri nyingine katika Mkoa huo kuhakikisha zinaweka mikakati madhubuti ya kulipa madeni hayo haraka, ili kuimarisha uaminifu kwa wazabuni na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma.

Katika hatua nyingine, wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) wa Songwe wamepitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26, ambapo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na Halmashauri zake zinatarajia kukusanya na kutumia jumla ya Shilingi bilioni 231.8, ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.59 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2024/25.

Katika bajeti hiyo, matumizi ya kawaida yanakadiriwa kuwa Shilingi bilioni 165.3, huku, Shilingi bilioni 130.3, zikielekezwa katika malipo ya mishahara kwa watumishi.