March 3, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri Rungwe yapongezwa  nafasi ya kwanza matokeo kidato cha nne

Na Esther Macha,Timesmajira Online,Mbeya

MKUU wa mkoa Mbeya,Juma Homera ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kuwa kinara wa elimu na kushika nafasi ya kwanza kimkoa katika  matokeo ya kidato cha Nne kwa halmashauri zote saba zilizopo mkoani hapa.

Akizungumza Februari 28,2025 wakati wa  maadhimisho ya siku ya elimu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe,Homera amesema kuwa kazi iliyofanyika ni kubwa  hivyo uongozi wa Halmashauri hiyo unastahili pongezi kubwa  kwa jitihada wanazofanya katika suala la elimu .

“Kuanzia mkuu wa wilaya ,Mbunge, Mkurugenzi,pamoja na Chama cha Mapinduzi hawa ni vinara wa elimu wilaya ya Rungwe mmepata majembe kweli kweli  kwasababu Rungwe wakati tunaanza mchakato huu wa  kupandisha ufaulu ilikuwa kama masihara lakini leo hii wamethibitisha kufanya vizuri na tumeona kazi waliyofanya ni kubwa nawapongeza Sana”amesema Homera

Aidha Homera amesema kuwa kwa wilaya ya Rungwe kushika nafasi ya kwanza kwa matokeo ya kidato cha Nne(4) kwa halmashauri zote Saba wanastahili pongezi kubwa kwani wamepata viongozi majembe na wanastahili kupewa maua yao kwani wakati mchakato huo  wa kutafuta namba moja ilikuwa kama masihara lakini wameweza na kufanikisha .

Mgeni Maalum wa Maadhimisho ya siku ya elimu kwa wilaya ya Rungwe Rais umoja wa mabunge duniani na Spika wa Bunge na Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini,Dkt.Tulia Ackson amesema kuwa tuzo za mara ya kwanza zilifanyika Wilaya ya Rungwe katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Msasani ambapo  zilikuwa tuzo za elimu za  mkoa wa Mbeya .

“Wazo hili za tuzo mkuu wa mkoa na mgeni  rasmi wa shughuli hii mara ya kwanza tuzo za mkoa Mbeya na zilifanyika katika viwanja hivi  na tuzo zile hazikua za Rungwe bali zilikuwa tuzo za elimu za mkoa Mbeya leo tumerejea tena hapa na Sasa ikiwa ni tuzo za elimu kwa wilaya ya Rungwe ni jambo la kheri na lazima walimu mmepewe sifa hii kubwa “amesema Dkt.Tulia.

Akitoa taarifa ya elimu kwa wilaya ya Rungwe, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rungwe, Renatus Mchau amesema kuwa halmashauri hiyo imeweka mikakati ya kuongeza  ufaulu pamoja na kuendelea kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa.

” Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe imeendelea kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa ya upimaji  ya darasa la nne kwa upande wa shule za msingi ambapo kwa mwaka 2021  ufaulu ulikuwa asilimia 94.7,2023 asilimia 96.1  huku 2024 ufaulu ukiwa ni asilimia 96.7 na ufaulu huu  unatokana na ushirikiano kati ya ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri na wadau mbalimbali lakini pia halmashauri inaendelea kuweka mikakati zaidi ya ufaulu kwa wilaya hiyo “amesema mkurugenzi huyo.