Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua Mkoani hapa imedhamiria kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula ya alizeti kwa kuwezesha vikundi vya wakulima katika kata zote mbegu za kutosha za zao hilo ili kuanza kilimo hicho.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Mwaga alipokuwa akizungumza na gazeti hii Ofisini kwake ambapo alisema kwa kuanzia wamesambaza jumla ya kilo 6,650 za mbegu za alizeti katika kata 16.
Alitaja kata ambazo zimepata mbegu hizo kuwa ni Ukumbisiganga, Zugimlole, Ushokola, Ugunga, Kazaroho, Igagala, Usenye, Usinge, Kamsekwa, Ichemba, Mwongozo,Sasu, Ilege, Ufuutwa, Igwisi, Uyowa na Kona nne.
Alibainisha kuwa zoezi la usambazaji mbegu hizo litakuwa endelevu ili kuhakikisha wakulima wa wilaya hiyo wanakuwa na zao mbadala wa tumbaku litakalowaingizia mapato mazuri na kuwainua kiuchumi.
Aliongeza kuwa ili kuwa na kilimo chenye tija kitakachowanufaika wakulima na jamii kwa ujumla wameweka utaratibu wa kutoa elimu kwa vikundi vyote vya uzalishaji mali wilayani humo.
Alifafanua kuwa ili kuboresha shughuli za kilimo katika wilaya hiyo Ofisi ya Waziri Mkuu imewajengea kitalu-nyumba kitakachotumika kutolea mafunzo ya kilimo bora, hivyo akatoa wito kwa wakulima kuchangamkia fursa hiyo.
‘Tumedhamiria kuongeza uzalishaji wa mazao chakula na biashara ili kuwainua zaidi wakulima wetu, hadi sasa jumla ya vijana 97kutoka maeneo mbalimbali wamepatiwa mafunzo na zoezi bado linaendelea’, alisema.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Jafael Lufungija alisema licha ya kugawiwa mbegu mkakati wa halmashauri hiyo ni kuhakikisha vikundi vyote vya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu vinavyojishughulisha na uzalishaji mali vinawezeshwa mikopo nafuu ili kufanikisha shughuli zao.
Aliongeza kuwa halmashauri imetenga kiasi cha sh mil 107kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya kukopesha vikundi vyote vinavyojishughulisha na uzalishaji wa mafuta ya alizeti, mawese, utengenezaji viatu, chaki na sabuni.
Aidha alisema sh mil 17 zimetengwa kwa ajili ya kuwezesha vikundi 2 vya wanawake vinavyojishughulisha na uchakataji asali na mazao mengine ya nyuki.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa