Judith Ferdinand, TimesMajira Online
Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Tanga na Manispaa ya Ilemela ni halmashauri tatu nchini zinazotekeleza mradi wa Uendelezaji Miji (Green & Smart Cities Sasa).
katika kuhakikisha miradi mikakati ya halmashauri inafanikiwa Tamisemi,Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya waliandaa majadilioano ya mada juu ya utekelezaji wa mipango mikakati ya halmashauri nchini,yaliyofanyika kwa siku mbili jijini Mwanza Machi 9 na 10, kupitia mradi wa Uendelezaji Miji (Green and Smart Cities Sasa).
Akizungumza katika majadilioano hayo Naibu Ofisa Muidhinishaji wa Mfuko wa EDF Wizara ya Fedha na Mpango, Jonathan Mpuya anasema Serikali ilibuni mradi wa uendelezaji miji kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) ambao ni wafadhili na kusainiwa Aprili 8, 2022.Ambao mradi huo utazingatia usafi wa mazingira pamoja na kukuza vipato vya wananchi kupitia ujenzi wa miundombinu itakayoanzishwa na halmashauri.
“Tulishirikiana nao kwenye kujaribu kuibua kwa kufuata malengo 17 ya maendeleo (SDGs) na lile lengo namba 17 linazungumzia maendeleo ya miji kwa hiyo tulijaribu kuangalia tuwe na mradi ambao unalenga majiji kama sehemu ya kuanzia na hasa tuliangalia miji yenye maji kwakuwa kumekuwa na uchafuzi mkubwa wa vyanzo vya maji,”anasema Mpuya.
Anasema mpaka sasa upande wa Serikali Umoja wa Ulaya umetoa fedha awamu ya kwanza kusaidia bajeti kiasi cha Euro milioni 7.
Ambapo maandalizi yanayoendelea kwa sasa ni ya uandaaji wa miradi mingine ambayo itatekelezwa kwa fedha nyingine ambayo EU itatoa na tayari upembuzi yakinifu wa awali umeshafanyika kwenye masoko ya samaki kwa upande wa Mkoa ya Tanga na mwanza.
Pia Mpuya alikiri katika mkutano huo kuwa mipango miji ambayo iliwasilishwa ni orodha tu ya miradi bila kufanyiwa upembuzi yakinifu nakudai wao na Tamisemi watafanyia kazi changamoto hiyo.
Kupitia Green & Smart Cities Halmashauri ya Jiji la Mwanza (Nyamagana) itatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya kuboresha machinjio huku Manispaa ya Ilemela ikitekeleza miradi mitatu na Tanga ikijiandaa kutekeleza miradi mitano ikiwa ni mpango makakati wa utekelezaji miradi hiyo kwa miaka mitano.
*Halmashauri ya Jiji la Mwanza*
Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza,Edward Mwamotela, anaeleza kuwa halmashauri hiyo inafanya kazi kwa ukaribu na Umoja wa Ulaya chini ya mradi wa Green and Smart Cities, ambapo unatekelezwa katika halmashauri tatu nchini, ikiwemo ya Jiji la Mwanza na Tanga na Manispaa ya Ilemela.
Lengo ni kuhakikisha halmashauri inaanda mpango ambao utaibua miradi mbalimbali itakayotekelezwa chini ya programu ya Green and Smart Cities,ambao unashirikisha mataifa mbalimbali ambayo yaliopo chini ya Umoja wa Ulaya ikiwemo Ufaransa,Ubelgiji,Ujerumani ambao wameisha onesha nia ya kushirikiana na halmashauri ya Jiji la Mwanza katika kutekeleza huo mradi.
Mwamotela anaeleza kuwa mpaka sasa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kushirikiana na Green and Smart Cities,wamefanya uchambuzi yakinifu wa awali ambao umeibua baadhi ya miradi ambayo itakuja kufanyiwa upembuzi yakinifu wa kina.
Katika hatua hizo wadau wote wameshirikishwa kwa miradi ambayo imeibuliwa ni pamoja na machinjio,masoko ya samaki,masoko ya biashara na mazao ambao lengo lake ni kuongeza mnyororo wa thamani.
“Tunapoenda kutekeleza,miradi hii itatupa matokeo makubwa kwa wananchi wa Jiji la Mwanza,kwa maana kama ni chakula watahakikisha wanapata chakula kilicho bora na kama ni nyama watapata nyama ilio bora na nzuri iliotoka katika machinjio ya kisasa ambayo haitaingiliwa na vitu vyovyote vinavyoweza kuharibu,”anaeleza Mwamotela.
Kipaumbele cha Jiji la Mwanza kupitia mradi wa Green and Smart Cities.Mwamotela anaeleza kuwa kipaumbele chao namba moja katika mradi huo ni kuboresha machinjio ya Nyakato ambapo wametenga bilioni 7.
Ambapo yatakuwa na ubora kwa maana kwamba ng’ombe anaingia kwenye mashine anachinjwa na kupembuliwa ng’ombe mzima mpaka anafika mwisho anakuwa kwenye kifungashio(package).
Pia wameweka mfumo wa kuzalisha umeme kutokana na kinyesi cha ng’ombe ambao utazalisha umeme utakaosaidia kuendesha mitambo ya machinjio hiyo.
Huku miradi mingine ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha ngozi Nyakato,soko la machinga la Nyegezi, Lwanhima industrial park, ujenzi wa soko la rejareja na samaki Mkuyuni, ujenzi wa soko la machinga Igoma, ujenzi wa soko la machinga Mchafukoga.
“Miradi yote tutakayoitekeleza mfano soko na machinjio zitazalisha taka,hivyo kudhibiti uchafuzi katika machinjio kinyesi cha ng’ombe kitatumika kuzalisha nishati ya umeme kwa ajili ya kuendesha mitambo,ujenzi wa masoko utasaidia kuondoa machinga kwani tukiwa na miundombinu ya masoko na watu wakaelimishwa na kutii sheria na kufuata utaratibu hakutakuwa na wajasiriamali wanaopanga bidha katika maeneo ambayo siyo rasmi,”.
Pia Mwamotela anaeleza kuwa halmashauri hiyo inahitaji siyo chini ya bilioni 100, baada ya upembuzi yakinifu wa kina kufanyika ili kutekeleza miradi,kama walivyopewa maarifa katika kikao hicho ,kuwa wanatakiwa kama halmashauri wanapoandaa mipango mikakati lazima waandae mpango wa kuhakikisha wanaibua fedha ili kutekeleza mpango mkakati wao.
“Green and Smart Cities ni mradi ambao umebuniwa kuhakikisha kwamba zinaziwezesha halmashauri kuwa na miradi ambayo itawezesha kuwa na mazingira mazuri,tutengeneze miji yetu iwe ya kuvutia hatuwezi tukajenga miji yetu kuwa ya kuvutia kama hatuna vyanzo vya uchumi mzuri, uwekezaji unahitaji fedha kama hauna fedha lazima utakwama,”anaeleza Mwamotela na kuongeza kuwa
Mwamotela anasema miradi hiyo itakapokamilika si tu itafanya jiji hilo kuvutia lakini pia huduma za kibiashara na hata za vyakula itakuwa bora iliyozingatia afya za watumiaji.
*Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela*
Mchumi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Herbert Bilia anasema ili utekelezaji wa mipango yao ya miradi ya kimkakati ifanyike vizuri wanahitaji rasilimali fedha.
“Kwetu kitu muhimu tulicho nacho ni Ziwa Victoria ambalo limezunguka Manispaa yetu kwa asilimia 73.3,”.
Anasema watatekeleza miradi mitatu katika program ya Green anda Smart Cities ambayo inashughulika na mnyororo wa thamani hususani kwenye rasiliamali za masoko upande wa ziwa.
Mradi wa kwanza ni uboreshaji wa mwalo wa Kirumba, mwalo huo unachangia pato zaidi ya milioni 700 hadi bilioni 1, katika manispaa kila mwaka kwa hiyo wanajua wakiboresha wataweza kwenda mbali zaidi ya hapo.
Mradi mwingine ni mwalo wa New Igombe ambao wanatarajia kuuboresha ili miundombinu yote iwe rafiki kwa maana ya samaki na dagaa watunzwe vizuri wasiharibike ili kuongeza thamani katika mnyororo mzima wa mazao ya uvuvi na mradi mwingine ni soko la Buswelu tutakaloliboresha kuwa la kisasa.
“Umoja wa Ulaya umeisha tembelea eneo hili la mwalo wa Kirumba na sasa wanaenda kufanya uchambuzi yakinifu pia wameuchagua kuwa ni mradi ambao utatekelezwa,”anaeleza Bilia.
*Halmashauri ya Jiji la Tanga*
Mratibu wa Mradi wa Green & Smart Cities jijini Tanga Kizito Nkwabi, anaeleza kuwa wanatarajia kuwa na miradi mingi ambayo itapelekea mji wa Tanga kupendeza lakini ukuaji wake uendane na mpango mkakati wa Jiji hilo.
Anasema kwa sasa wameanza kufanya tafiti mbalimbali akidai katika kutengeneza miradi lazima tafiti za awali zifanyike ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya.
Anasema kwa kuanzia watafanya mradi wa kuhakikisha Tanga inakuwa na mfumo mzuri wa chakula kwa kuanzisha ujenzi wa soko la chakula kutoka mashambani, soko la uchakataji wa samaki, miundombinu ya kijani, kudhibiti maji taka na kuboresha maji safi na kuhakikisha taka zote zinazozalishwa jijini hapo zinachakatwa na kutengeneza bidhaa mbalimbali.
Ambapo katika mradi huo wameanza na utafiti wa awali pia utaleta matokeo chanya ambayo yaweka mfumo mzuri wa chakula kwa Jiji hilo.Nkwabi anaeleza kuwa,mfumo wa chakula kwa maana ya kwamba wanategemea wawe na miradi ya ujenzi wa masoko mfano soko la chakula kinachotoka shambani.
“Tanga tuna bahari ambapo kuna chakula samaki,tunategemea kuona soko zuri la samaki kupitia mradi huu wa Green and Smart Cities,” anaeleza Nkwabi.
Pia anaeleza kuwa wana miradi mingine ya miundombinu ya kijani ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuna kuwa na maji safi mijini na vijijini na wanadhibiti maji taka,kuwa na mandhari nzuri ndani ya mji na maeneo ya wazi yaweze kutengenezwa vizuri.
“Kwenye tafiti za awali tumeanza kuona vipaumbele vyetu katika mradi ni chakula, kujenga masoko ya samaki, kuhakikisha hakuna taka kwa maana taka zote zinakuwa zinachakatwa,tunataka tuwe na mradi wa usafi wa jiji kupitia programu ya Green and Smart Cities Sasa na tupo tunakamilisha ili tuone tunatakiwa kufanya nini na tunaweka mfumo gani kudhibiti taka,”anaeleza Nkwabi.
*Serikali inavyosaidia kutekeleza miradi*
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Miji na Vijijini kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Rachel Kaduma anasema wameweka utaratibu wa kuhakikisha miradi hiyo inakamilika ikiwemo kuwapa mafunzo watumishi wa halmashauri jinsi ya kuipanga na kuitekeleza.
“Tumeweka utaratibu wa kuhakikisha miradi hii inakwenda kwa wakati kwa sababu hata fedha hii ambayo tunaipata kutoka Umoja wa Ulaya ni za muda kwahiyo ni wakati wa Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Serikali Kuu kuhakikisha hizo halmashauri ambazo zimehusishwa na miradi husika michakato ya kupanga miradi ipi itakayotumika kwa muda gani, lini ianze, ili fedha zikifika zinaenda kufanya kazi moja kwa moja kuhakikisha inakamilika kwa wakati,”anasema
*Changamoto zinazokabili majiji hayo kutekeleza miradi*
Kutokana na uwepo wa miradi hiyo EU, Serikali, Halmashauri pamoja na wadau mbalimbali kutoka taasisi za kifedha na sekta binafsi walikutana jijini Mwanza mwezi Machi,kujadili kuhusu utekelezaji wa mipango mikakati ya Mamlaka za Serikali za Mitaa na namna ya kufanikisha utekelezaji wake nchini.
Akizungumza katika mkutano huo wa siku mbili, Meneja Uendelezaji Biashara wa Benki ya Maendeleo ya TIB, Joseph Chilambo anasema halmashauri nyingi hazina uwezo wa kuandaa miradi inayokidhi vigezo vya kukopesheka na hata ikikopesheka hairudishi fedha kwa wakati akitolea mfano benki hiyo hadi sasa imetoa bilioni 8 kati hizo bilioni 1.8 pekee ndio zilizorejeshwa.
Kuhusu halmashauri kutokuwa na fedha za kutosha za kutekeleza miradi, Mratibu wa Programu ya Uimarishwaji Mikoa na Serikali za Mitaa (RLGSP)kutoka Tamisemi, Lemmy Shumbusho anasema wanawatafuta wadau, kuhamasisha miradi ya mashirikiano pamoja na kuhamasisha halmashauri kuwekeza katika miradi inayolipa ili ijisimamie.
“Tumegundua halmashauri nyingi zinakosa uwezo wa uandaaji wa mipango mikakati lakini Serikali imekuwa na juhudi mbalimbali za kuwapa mafunzo hao watendaji wa halmashauri pamoja na kuandaa muongozo wa utekelezaji miradi”anasema.
Meneja Programu ya Maendeleo ya Miji Umoja wa Ulaya Tanzania,Martino Vinci anasema, Umoja wa Ulaya itaendelea kufadhili mradi huo na kuzitaka halmashauri zitumie fursa zilizopo kwa kushirikiana na sekta binafsi kuikamilisha licha ya changamoto wanazokabiliana nazo kwa ustawi wa wananchi na Taifa.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia