Na Penina Malundo,TimesMajira Online
WAKATI dunia iliposhambuliwa na ugonjwa wa Covid-19, mataifa mengi yaliingiwa na hofu juu ya ugonjwa huu, hali ambayo iliwafanya watu wengi kupoteza maisha.
Kwa sababu ya ugonjwa huo kuendelea kushika kasi nchi mbalimbali ulimwenguni, serikali za nchi nyingi zililazimika kufunga mipaka yao na wananchi wake kukaa ndani (lockdown)ili kupunguza kusambaa kwa ugonjwa huo.
Tanzania, kama nchi zingine, zilichukua hatua za haraka kuzuia kuenea kwa janga la Covid-19. shule zote na vyuo vikuu vilifungwa na wanafunzi waliamriwa kukaa nyumbani. Serikali ilitoa maagizo juu ya jinsi ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa ikiwa ni pamoja na kuvaa Barakoa , kunawa mikono na kutumia dawa ya kusafisha mikono. Mikusanyiko yote ya watu wengi ikiwa ni pamoja na mikutano na shughuli za michezo zilipigwa marufuku.
Kwa upande wa nyumba za ibada ikiwemo makanisa na misikiti ziliruhusiwa kuendelea kwa sharti kwamba viongozi wa kidini wawaongoze wafuasi wao kuzingatia hatua za kujikinga. Katika maeneo mengine, haswa katika vituo vya mabasi, maduka, na masoko ya umma, watu ambao walishindwa kutii maagizo yaliyotolewa na serikali, haswa kunawa mikono na kutumia dawa ya kusafisha mikono, walichukuliwa hatua ya kupigishwa faini.
Kwa sasa hakuna kizuizi cha kutoka nje ya nchini na watu wanaruhusiwa kuendelea na shughuli zao za kila siku lakini wanaendelea kusisitizwa kuendelea kuchukua hatua za kinga, wakiwemo wakulima, ambao waliendelea kufanya shughuli zao za kilimo kama kawaida.
Masoko yako wazi na usafirishaji wa umma unafanya kazi,viongozi wa Serikali pamoja na Rais John Magufuli amekuwa akitoa wito kwa washiriki wa madhehebu tofauti ya kidini kuomba kwa sala na dua kama njia ya kupigana na Covid-19 kuendelea kuwepo nchini.
Hatua mbalimbali zilichukuliwa na Tanzania, kama vile kuruhusu watu wa madhehebu mbalimbali kuendelea kuabudu katika makanisa na misikiti na hakukuwa na vikwazo kwa nchi hiyo, na ni nchi pekee iliyofanywa hivyo ikilinganishwa na nchi zingine za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Hali ya uzalishaji na upatikanaji wa mazao ya chakula nchini uliendelea kuwa mzuri katika kipindi cha zaidi ya miaka mitano mfululizo hata baada ya ugonjwa wa Covid-19 kuingia nchini Machi, 2020. Kufuatia uzalishaji wa ziada wa mazao ya chakula kuanzia msimu wa kilimo mwaka 2015 /2016 hadi 2019/2020 katika kipindi hicho, nchi imekuwa na kiwango cha utoshelevu kati ya asilimia 120 hadi 125.
Katika msimu wa 2019/2020, nchi ilitarajiwa kuwa na uzalishaji wa ziada ikilinganishwa na mahitaji. Mafanikio hayo yalitokana na hali ya hewa nzuri, upatikanaji wa pembejeo kwa wakati pamoja na usimamizi na utekelezaji mzuri wa sera na mikakati mbalimbali inayotekelezwa na serikali pamoja na wadau wengine wa masuala ya kilimo.
Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wataalam kutoka Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwezi Juni 2020 ilifanya tathimini ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2019/2020 na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2020/2021 katika mikoa yote 26 na kuhusisha halmashauri 184 za Tanzania Bara kwa lengo kubaini uzalishaji na mahitaji.
Matokeo ya tathmini yanaonesha kuwa hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini iliongezeka kwa msimu wa 2019/2020 ikilinganishwa na msimu wa 2018/2019. Chini ni jedwali inayoonyesha hii.
Mahitaji ya chakula kwa mwaka 2020/2021 ni kiasi cha tani 14,347,955 ikilinganishwa na tani 13,842,536 kwa mwaka 2019/2020. Huku kwa tani 9,131,803 ni za mazao ya nafaka na tani 5,216,152 ni kwa mazao yasiyo nafaka.
Kutokana na mahitaji haya yakilinganishwa na uzalishaji, nchi inatarajiwa kuwa na ziada ya tani 3,394,434 za chakula, ambapo tani 1,322,020 ni za mazao ya nafaka na tani 2,072,413 ni za mazao yasiyo nafaka.
Kulingana na uzalishaji wa chakula, nchi itaendelea kuwa na utengamano wa usalama wa chakula, ambapo uwepo na upatikanaji wa chakula nchini utakuwa ni wa kuridhisha.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 18,2020, aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini kwa msimu wa mwaka 2019/2020 na upatikana wa chakula kwa mwaka 2020/2021.
Anasema tathmini iliyofanyika na Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) imebainisha kuwa msimu wa mwaka 2019/2020 mahindi yatachangia asilimia 36, mchele asilimia 16.6, muhogo asilimia 14, mikunde asilimia 10.5, viazi asilimia 9.2, mtama asilimia 5.9 na ngano asilimia 0.4.
Anasema kwa kuzingatia Kigezo cha Upimaji wa Kiwango cha Utoshelevu (Self Sufficiency Ratio – SSR), matokeo yanaonesha kuwa mwaka wa chakula 2020/2021, nchi inatarajiwa kuwa na kiwango cha utoshelevu cha asilimia 124.
“Kiwango hiki kimeongezeka ikilinganishwa na msimu wa 2018/2019 katika kipindi kama hiki ambapo kiwango cha utoshelevu kilikuwa asilimia 119,” anasema .
Aidha,anasema Serikali imeendelea kuhimiza na kuelekeza wakulima kuzalisha kwa tija ili kuongeza uzalishaji na kufanya kuimarisha mifumo ya usambazaji na upatikanaji wa pembejeo kwa wakati hususani mbolea, mbegu bora, viuatilifu na zana bora za kilimo.
Jitihada mbalimbali zilizofanywa na Rais John Magufuli za kuhakikisha Watanzania wanaondokana na hofu juu ya ugonjwa huo na kuona kwamba Covid-19 ni ugonjwa kama magonjwa mwingine.
Hali hiyo imewasaidia Watanzania wengi wakiwemo wakulima kuendelea na shughuli za kilimo na kuzalisha mazao mengi ambayo yatasaidia kuimarisha hali ya chakula nchini na kusaidia kuuzia mataifa mengine ambayo yamefungiwa sababu ya ugonjwa huo.
Makala hii imeungwa mkono na Kanuni ya WanaData Initiative ya Afrika, Twaweza na Kituo cha Pulitzer juu ya Kuripoti Majanga
More Stories
Ushiriki wa watoto, vijana katika vita ya mabadiliko ya tabianchi
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini