December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi CBE wahimizwa kuishi kwa upendo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM

WATUMISHI wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Kampasi Kuu ya Dar es Salaam wamehimizwa kuishi kwa upendo na kushirikiana muda wote wanapokuwa katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili kutoa huduma bora.

Akizungumza mwishoni mwa wiki katika Kampasi kuu ya Dar es Salaam katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja kwa niaba ya Mkuu wa Chuo Prof., Edda Tandi Lwoga, Naibu Mkuu wa Chuo (Taaluma, Tafiti na Ushauri wa Kitaalamu), Dk Nasibu Mramba,  alisema watumishi wanapopendana wataoneana huruma na kusaidiana.

“Narejea maneno ya Waziri wetu, Dk. Selemani Jafo alipotutembelea hapa alisema tupendane, tusaidiane tuoneanae huruma, tuwe na utaratibu wa kupeana tahadhari kila kwenye dalili ya tatizo tukioneana huruma sisi kwa sisi tutaonea huruma pia wateja wetu,” alisema Dk. Mramba.

Naye Naibu Mkuu wa Chuo, (Mipango Fedha na Utawala) Prof. Emmanuel Munishi alisema katika siku hiyo ya kilele Chuo kiliamua kujitathmini kwenye eneo la mawasiliano ya ndani ambapo pamoja na mambo mengine watumishi walipata mafunzo kuhusu namna ya kuwasiliana kimkakati.

“Tumeona kuna uhusiano mkubwa kati ya mawasiliano ya wenyewe kwa wenyewe na huduma kwa mteja, tukiweza kuwasiliana na kuhudumiana vizuri sisi wenyewe kwa wenyewe inakuwa rahisi kuwahudumia wateja wetu kutoka nje lakini pia tujenge utaratibu wa kushirikiana, hapa ni sehemu tunayokaa kwa muda mrefu,” alisema Prof. Munishi.

Aidha, alisema watumishi wakipendana na kufanyakazi kwa ushirikiano wataleta tija kubwa kwenye maeneo yao ya kazi na kukifanya chuo hicho kuendelea kuwa tegemeo kwa wanafunzi wengi wa Tanzania wanaotaka kusomea elimu ya biashara.

Alisema upendo na ushirikiano ni nguzo muhimu sehemu yoyote ya kazi na kuahidi  kuwa uongozi wa chuo utaendelea kuwawekeza mazingira mazuri watumishi wa chuo hicho ili waweze kuendelea kukifanya kuwa miongoni mwa vyuo bora hapa nchini.