Na Grace Gurisha
HAKIMU Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba,imeamuru Mmiliki
wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited
(IPTL), Habinder Seth na Mwanasheria wa kampuni hiyo, Joseph Makandege
kupelekwa mahakamani kutokana na Gereza la Ukonga kutokuwa na mfumo wa
Video Conference.
Hakimu Simba, alitoa amri hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu kesi hiyo ilipotajwa. Pia ameamuru mfanyabiashara James
Rugemalira kuendelea kukaa mahabusu kwa kuwa Gereza la Segerea lina
mfumo huo wa Video Conference ambapo anaweza kusikiliza kesi yake
akiwa gerezani.
Hakimu Simba alifikia hatua hiyo baada ya Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Wankyo Simon kudai kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya
kutajwa, lakini washitakiwa wote hawapo.
Alidai washitakiwa hao wapo magereza tofauti hivyo wameshindwa kufika
mahakamani. Baada ya kutoa maeleza hayo, Hakimu Simba alisema kutokana
na washtakiwa hao kuwa magereza tofauti, huku Gereza la Ukonga likiwa
halina mfumo huo, washtakiwa Seth na Makandege watapaswa kupelekwa
mahakamani kila tarehe ya kesi yao itakapotajwa.
Aliagiza Rugemalira kuendelea kusikiliza kesi yake akiwa gerezani.
Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 23, mwaka huu kwa ajili
ya kutajwa. Washitakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa
yanayowakabili katika Jiji la Dar es Salaam na nchi za Afrika Kusini,
Kenya na India.
Wanakabiliwa na mashitaka 12 miongoni mwa mashtaka hayo yapo ya kula
njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi na kutoa nyaraka za
kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kutakatisha fedha
na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh
309,461,300,158.27.
Washitakiwa wanadaiwa kati ya Oktoba 18 ,2011 na Machi 19, 2014 jiji
Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na
India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Mwanasheria wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania
Limited (IPTL), Makandege, anakabiliwa na mashitaka matano likiwemo
la kuisababishia Serikali hasara ya dola za Marekani 980,000.
More Stories
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya
Prof.Muhongo awapongeza vijana 32 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza
Rais Samia atimiza ahadi Hanang