December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hakimadini, yasisitiza elimu kwa jamii kuondoa Imani potofu dhidi ya wanawake sekta ya madini

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Imani potofu dhidi ya wanawake katika sekta ya madini ni miongoni mwa changamoto zinazokabili kundi hilo hali ambayo inaweza kusababisha kushindwa kusonga mbele.

Hivyo muarobaini wa kutatua changamoto hiyo ni jamii kupewa elimu ili iweze kuachana na imani hizo potofu dhidi ya wanawake.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Shirika la HakiMadini, Zawadi Joseph, katika mafunzo ya siku nne yanayofanyika jijini Mwanza, na kuratibiwa na shirika hilo,linalotekeleza kwa vitendo tamko la kimataifa la Haki ya Kusema Hapana ama Ndiyo (Right To Say No/ Yes) kwa ufadhili wa shirika la WoMin African Alliance la Afrika Kusini ambapo imeshirikisha
wanaharakati 22 kutoka mashirika yanayotetea haki za wananchi na wachimbaji wadogo wa madini Afrika kutoka nchi za Uganda,Kenya, Zimbabwe, Tanzania Cameroon na Afrika Kusini.

Zawadi ameeleza kuwa, wanawake wengi wanamiliki migodi na wameajiri wanaume ila sheria inatambua mwanaume zaidi kwa sababu ya uhalisia wa sekta hivyo na wengi wanaozama migodini kuchimba madini ni wanaume na bado sekta hiyo ni kandamizi kama walivyo sikia kutoka kwenye mafunzo kutokana na imani potofu kuwa mwanamke anaposogelea kwenye mgodi akiwa katika siku zake za hedhi basi madini yanapotea hali ambayo siyo kweli kwani hakuna uhusiano kati ya kukosekana kwa madini na mwanamke kuwa katika siku zake.

Hivyo ameeleza kuwa jamii inatakiwa ipewe elimu na itambue kuwa hizo ni imani potofu tu wala siyo kweli kwamba mtu akilala na mwanamke mzee basi atapata madini mengi au mwanamke akiwa katika siku zake za hedhi basi madini yanapotea.

Amesema kama mashirika wanahitaji kutoa elimu kwa jamii hasa jamii husika inayolenga sekta ya madini kuwaelimisha kuwa hizo ni imani potofu na zitazidi kuwarudisha nyuma wao wanawake na hawataweza kwenda mbele.

“Tunakazi kubwa mbele yetu ya kuelimisha jamii tusiamini zaidi mila potofu tukitaka kusonga mbele zaidi hasa tukitaka kuwainua wanawake kiuchumi na tusiwe tegemezi kwa kina baba,serikali na jamii,elimu tunayoipata hapa kwenye mafunzo haya isiishie hapa bali tuipeleke katika maeneo yetu kwa watu ambao hawana uelewa ili wasizidi kuamini imani potofu,”ameeleza Zawadi na kuongeza kuwa

“HakiMadini imekuwa ikitoa elimu katika jamii kuondokana na dhana hiyo na katika maeneo ambayo tumefika na kutoa elimu, wanawake wameanza kushiriki kwenye uchimbaji madini na wamewaajri wanaume kwenye migodi yao,”.

Pia ameeleza kuwa serikali iendelee kutambua mchango wa wanawake hasa katika sekta ya madini na sheria isimamie kile ilicho tamka wanawake wataanza kujikita kwenye shughuli husika za uchimbaji madini bila hofu wala kuogopa.

Mkurugenzi wa taasisi ya Africa Transcribe, Evans Rubara,ameeleza kuwa kuna Sheria nyingi zimeundwa katika nchi za Afrika kusini,Zimbabwe,Kenya na Uganda pamoja na Sheria hizo zinahitaji makampuni ya uchimbaji kuwezesha wananchi na wanaweza kufaidika na shughuli za uchimbaji mdogo au mkubwa katika maeneo yao.

Rubara ameeleza kuwa katika Bara la Afrika moja ya vizingiti vilivyopo kwa wachimbaji wanawake kutokushirikishwa katika uchimbaji kutokana na mila potofu zilizopo ambazo zimekuwa zinadhofisha juhudi za wanawake katika kujihusisha na uchimbaji huku asilimia 27 ya wanawake ndio wanaojishughulisha kwenye sekta hiyo.

Mwakilishi wa wachimbaji wadogo wa madini ya Rubby kutoka Mundala mkoani Arusha Rose Olokwani, ameeleza kuwa kwa muda mrefu wanawake waliwekwa kando kushiriki kwenye shughuli za madini kutokana na mfumo dume lakini kutokana na jitihada za shirika la HakiMadini kuelimisha wananchi, utamaduni huo umeanza kutoweka na sasa wanawake wameanza kujikita kwenye uchimbaji madini na kujikwamua kiuchumi.

Mchimbaji madini ya dhahabu katika machimbo ya Mugusu mkoani Geita Benadetha Petro,ameeleza kuwa mkutano huo ni muhimu kwa kuwa umekutanisha wanaharakati kutoka mashirika mbalimbali ya Afrika na kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu namna sekta za uwekezaji zinaendeshwa katika mataifa yao hususani kuwasaidia wanawake kunufaika kiuchumi na raslimali zilizopo katika maeneo yao.

Naye Mratibu wa shirika la Center for Natural Resources Governance kutoka nchini Zimbabwe Zinzile Fengu,ameeleza kuwa nchini kwao wanaamini kuwa ukilala na mwanamke mzee unapata dhahabu nyingi huku Raya Ahmed kutoka nchini Kenya ameeleza kuwa jadi na mila zimekuwa zinawakandamuza wanawake kimaendeleo.

Mkurugenzi wa Shirika la HakiMadini, Zawadi Joseph kushoto akizungumza katika mafunzo ya siku yanayofanyika jijini Mwanza na kuratibiwa na shirika hilo,linalotekeleza kwa vitendo tamko la kimataifa la Haki ya kusema hapana ama ndiyo(Rights to say No/yes) kwa ufadhili wa shirika la Womin African Alliance la Afrika Kusini ambapo imeshirikisha wanaharakati 22 kutoka mashirika yanayotetea haki za wananchi na wachimbaji wadogo wa madini Afrika kutoka nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Zimbabwe, Cameroon na Afrika Kusini.(Picha na Judith Ferdinand)
Mkurugenzi wa taasisi ya Africa Transcribe, Evans Rubara (akiongoza majadiliano katika mafunzo hayo yaliyoshirikisha wanaharakati 22 kutoka mashirika yanayotetea haki za wananchi na wachimbaji wadogo kutoka nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Zimbabwe, Cameroon na Afrika Kusini ambayo yanafanyika jijini Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)
Washiriki wa mafunzo kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Zimbambwe, Afrika Kusini na Cameroon wakiwa katika mafunzo hayo yalioratibiwa na shirika la HakiMadini kwa ushirikiano wa karibu na taasisi ya AfricaTranscribe kwa ufadhili wa shirika la WoMin African Alliance yaliyofanyika jijini Mwanza.