November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Haki Elimu yaunga mkono kufutwa ada kidato cha tano, sita

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

TAASISI ya Hakielimu imeiunga mkono mapendekezo ya Bajeti ya serikali ya mwaka 2022/23 kwa kufuta ada, kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita, uamuzi ambao utawanufaisha wanafunzi takribani 95,000 wa kidato cha tano na zaidi ya 60,000 wa kidato cha sita waliojiunga kusoma katika shule za umma ambao wengi wao hutokea familia zenye kipato cha chini.

Hayo ameyasema Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Elimu, John Kalage wakati akitoa maoni kuhusu Bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Mwigulu Nchemba juzi Bungeni Jijini Dodoma.

“Ni muhimu kuzingatia kuwa uamuzi huu utaongeza zaidi ya Bilioni 10.3 katika bajeti ya utoaji elimu bila ada, kwa sasa serikali inatumia takribani Bilioni 321 kutoa elimu bila ada kwa wanafunzi wa msingi mpaka kidato cha nne”

Kalage alisema, kupitia hotuba ya mapendekezo ya kufuta ada, shilingi bilioni 10.3 zilizokuwa zikilipwa itasaidia kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati kama serikali ilivyoonesha niaserikali imeonesha nia

“Uamuzi wa kupanua wigo wa mikopo kwa vyuo vya kati na ufundi tunauunga mkono, hii itatoa fursa kwa wanafunzi takribani 385, 115 wanaomaliza kidato cha nne na ambao hushindwa kujiunga na kidato cha tano kutokana na ufaulu wa chini pia wastani wa wanafunzi 11, 551 wanaohitimu kidato cha sita na hushindwa kujiunga na vyuo vikuu kwasababu kupata alama za chini katika mitihani yao”

Kalage aliongeza kuwa ni muhimu serikali iongeze bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ili kutoa fursa kwa wanafunzi hao ambao hawapati fursa ya kujiunga na vyuo vikuu ili kuwahudumia wanafunzi wote ambapo pendekezo lao ni kuwa na Benki ya mikopo ya wanafunzi badala ya bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Aidha, Kalage aliipongeza Bajeti hiyo katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuongeza fedha kwa wizara ya elimu toka Trilioni 5.3 mwaka 2021-22 hadi Trilioni 5.64 kwa mwaka wa Fedha 2022-2023 na kusema ongezeko hili litasaidia kukuza sekta elimu nchini.

Mbali na hayo, Kalage aliiomba serikali kuongeza zaidi bajeti ya utoaji elimu ili kufidia gharama ambazo zinaongezeka kwa upande wa serikali.