March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Gypson kutekeleza vipaumbele vitano akishinda Udiwani

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online ,-Bukoba

Mgombea Udiwani wa Kata ya Nshambya Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kupitia Chama Cha Mapinduzi ( CCM ) Godson Gypson,amewaahidi wananchi kutekelezaji vipaumbele vitano vya maendeleo endapo watamchagua tena katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29,2025.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika mtaa wa Bunkango,Gypson,amesema vipaumbele vyake vitazingatia mahitaji halisi ya wananchi na mafanikio ambayo tayari yameanza kuonekana wakati akiwa madarakani.

Vipaumbele alivyohaidi ni kuboresha shule ya msingi Nshambya,ambapo atahakikisha shule hiyo inapata miundombinu bora ikiwa ni pamoja na madarasa ya kisasa, madawati ya kutosha, huduma za maji na vyoo vya kisasa kwa wanafunzi na walimu.

Pia smeahidi kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha mitaa yote ya kata ya Nshambya inapatiwa umeme wa uhakika kupitia miradi ya serikali.

Amesema atatilia mkazo upatikanaji wa maji safi kwa wakazi wa kata hiyo kwa kusimamia ujenzi wa visima na mifumo ya maji ya bomba hasa maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo.

Sanjari na hayo ameahidi kuendelea kuboresha barabara zote 34 zilizopo katika kata hiyo ambazo tayari zimesajiliwa wakati akiwa madarakani.

Amesisitiza kuwa barabara hizo zitapitika kipindi chote cha mwaka ili kuwezesha shughuli za kiuchumi na kijamii.

Akiwa madarakani Mgombea huyo alieleza kuwa katika kipindi chake cha uongozi tayari ameanzisha na kusimamia miradi kadhaa ya maendeleo, na kuahidi kuwa endapo atapata ridhaa ya wananchi, ataendeleza jitihada hizo kwa kasi zaidi.

Amesema ujenzi wa daraja la Kyabitembe limefungua mawasiliano ya wakazi wa Kata ya Rwamishenye na Kata ya Nshambya na kurahisisha usafiri na usafirishwaji wa watu na bidhaa.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM),Mkoa wa Kagera Faris Buruan ,amesema mgombea Udiwani wa Kata ya Nshambya ambaye pia alikuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba amekuwa kiongozi wa mfano kutokana na kazi kubwa alizofanya wakati wa uongozi wake.

Buruan,amesema katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake Godson Gypson ametekeleza miradi 50 ya maendeleo katika sekta mbalimbali yenye thamani ya shilingi bilioni 9.3 Kata ya Nshambya ikiwemo sekta ya elimu,afya, miundombinu ya barabara na sekta nyingine nyingi.

Ameongeza kuwa pamoja na mafanikio hayo bado miradi 21, ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na kwa kumpa ridhaa tena kupitia sanduku la kura,watampa nguvu ya kuikamilisha na kusimamia maendeleo ya wananchi kikamilifu.

Sanjari na hayo amesisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi kina sera bora za maendeleo na mgombea wao amepitishwa kutokana na uadilifu ,uwezo wa kusikiliza wananchi na kutatua matatizo yao kwa vitendo.