February 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

GreenFaith yatoa mapendekezo yake mkutano wa mission 300 kwa Wakuu wa nchi,Serikali za Afrika

Na Penina Malundo,Timesmajira.

JUMUIYA ya Asasi za Kiraia ya GreenFaith Tanzania,imetoa mapendekezo mbalimbali kwa wakuu wa nchi na serikali za Afrika katika utekelezaji wa misheni 300 na azimio la Dar es Salaam kuhakikisha watu milioni 300 wanapatiwa nishati iliyosafi ikiwemo Umeme wa Jua,Upepo,Maji pamoja na Jotoardhi na sio nishati zenye kuharibu mazingira.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam,Afisa Mwandamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi na Nishati Jadidifu,Baraka Machumu wakati wakitoa mapendekezo yao baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Nishati uliowakutanisha wakuu wa nchi na serikali za Afrika Januari 27 na 28 mwaka huu.

Amesema wananchi wa nchi za afrika wanapaswa kupewa kipaumbele kwa teknolojia jadidifu ambayo siyo tu zinapunguza uzalishaji wa hewa chafuzi wa mazingira bali zinatoa nafasi kwa wananchi kutengeneza ajira kupitia uzalishaji huo wa nishati safi.

Machumu amesema linapokuja suala la upatikanaji wa umeme mara nyingi serikali na viongozi wanaongelea suala moja la umeme pekee katika matumizi ya majumbani ambayo ni nishati la kupikia ,kumulikia mwanga, na zile zinazosaidia binadamu katika shughuli zake.

”Viongozi wanasahau kama kuna nishati nyingine ambazo zikitiliwa mkazo na kuanza kutumika zitatusaidia kwa kiasi kikubwa hata kuondokana na mabadiliko ya tabianchi,”amesema na kuongeza

”Jumuiya yetu tunatamani viongozi wetu wa Afrika ambao walikaa na kupitisha azimio la Dar es Salaam kuangalia kwa kina namna ya kuweka miradi ya nishati jadidifu (mbadala) ambayo uwa endelevu kwa wananchi na inaleta manufaa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Inashangaza kuona kuna mitaji mikubwa iliyowekwa kwenye nishati hizo nyingine ambazo si nishati rafiki,ikiwemo ile ya Bomba la Mafuta kutoka Tanzania kwenda Uganda,umekuwa mradi wa kuchafua mazingira mbaya zaidi mafuta tunayabeba na kuyapeleka nchi nyingine ulaya zingeweza tutimiza lengo kubwa la kuweza kuwafikia wananchi na hata pesa,”amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa Taasisi inayojishughulisha na mabadiliko ya tabianchi na Nishati Greenfaith,Baraka Lenga amesema nishati jadidifu zitasaidia kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa binadamu,wanyama na kwenye mazingira ya kawaida.

“Sisi tunaweza kusema mafuta sio nishati safi kwa muktadha huo tunashauri kusitisha mradi wa bomba la mafuta ambao unachochea kufanya uharibifu wa mazingira pia tunaomba wajitahidi kuweka miundombinu ya ardhi yenye ustamilivu kwenye majanga ya mabadiliko ya tabianchi,”amesema

Aidha amesema pia wanashauri kuangalia ni namna gani masuala ya sayansi ya mabadiliko ya tabianchi katika sera ya nishati ,katika utengenezaji wa miundombinu imara ikiwemo nguzo na nyanya za umeme.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Green Conservation inayojishughulisha na mabadiliko ya tabianchi,Ziada Kassimu alisema wakuu hao wa nchi wanapotekeleza miradi ya misheni 300 wanapaswa kuangalia kundi la Wanawake katika kuhakikisha wanapatia elimu ya nishati iliyosafi kutokana na wao ndio watumiaji wakubwa wa nishati zote nchini.

Aidha Steven Selestin Mkulima kutoka Mkoa wa Morogoro amesema wakulima wamekuwa wakihitaji kwa kiasi kikubwa nishati safi kwaajili ya utunzaji wa mazao yao pamoja na kusaidia kilimo cha umwagiliaji.

”Kilimo cha miaka hii hakitegemei mvua pekee ake bali kinategemea umwagiliaji hivyo tusipokuwa na umeme wa uhakika inakuwa changamoto kwetu kufanya shughuli zetu.