January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Gomes atuma salamu Yanga

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

USHINDI wa goli 2-1 walioupata Simba dhidi ya Kagera Sugar na kufanikiwa kutinga katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam ‘Azam Sports Federation Cup (ASFC)’ umezidi kuwapa kiburi benchi la ufundi la Simba ambalo limeapa kubeba alama zote tatu katika mchezo wao wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) wa Mei 8.

Simba itaingia katika mchezo huo huku ikiwa imeweka rekodi bora katika mechi zao za VPL walizocheza mwezo Aprili ambapo imefanikiwa kubeba alama 15 baada ya kuwafunga 5-0 Mtibwa Sugar, waliibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Mwadui, 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, 1-0 dhidi ya Gwambina na kisha juzi kuwafunga Dodoma Jiji FC goli 3-1.

Mbali ya mechi hizo za VPL, ndani ya mwezi huo Simba pia ilicheza mechi mbili za Ligi Mabingwa Afrika ambapo walipata ushindi wa goli 4-1 dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo huku wakipoteza ule wa ugenini dhidi ya Al Ahly.

Alama hizo 15 walizokuwanya katika mechi tano ziliwawezesha kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na 61 wakiwa wamewazidi alama nne Yanga ambao wapo nafasi ya pili wakiwa na alama 57 huku Azam wakiwa nafasi ya tatu na alama zao 54.

Vita kubwa kwa sasa ipo kwa Simba na Yanga ambao mbali na kutana kukaa katika uongozi wa Ligi Kuu ili kusogea karibu na ubingwa lakini pia wanachokihitaji ni kila mmoja kuendeleza ubabe kwa kwenzake baada ya kulazimishana sare ya goli 1-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Januari 13.

Kocha mkuu wa klabu ya Simba, Didier Gomes Da Rosa amesema, rekodi hiyo bora pamoja na kushinda mechi yao dhidi ya Kagera Sugar inawafanya kujiamini kuelekea katika mchezo ujao ulio mbele yao dhidi ya Yanga.

Amesema, kama timu wana ujasiri wa kutosha na nguvu na morali ya kufanya vizuri licha kucheza mechi sita ndani ya siku 17 ambazo wamefanikiwa kushinda zote.

“Ushindi wa mechi sita za michuano ya ndani tulizocheza ndani ya siku 17 unatufanya kuanza maandalizi kuelekea katika mchezo wetu ujao tukiwa na ujasiri wa hali ya juu kwani tuhachokihitaji ni ushindi kwani tukifanikiwa kwenye hili basi ubingwa utakuwa wetu,” amesema Gomes.

Kuelekea katika maandalizi ya mchezo huo, tayari kocha huyo ameshaandaa majuku maalumu kwa nyota wake ambao anaamini wataweza kuisukuma timu yake kupata matokeo bora anayoyahitahi ili kujisogeza karibu na ubingwa.

Amesema kuwa, pia atawapa kazi maalum wachezaji wake wa safu ya ulinzi ambao watatakiwa kuakikisha hawaruhusu hatari yoyote kumaribia kipa wao wala kuleta madhara ya aina yoyote langoni mwao.

Katika mchezo huo, huenda kiungo Benard Morrison pamoja na Nahodha John Bocco wakapata nafasi ya kuanza kutoka na uwezo wa kubadili mechi waliouonesha katika mchezo wao uliopita dhidi ya Kagera.

Katika mchezo huo, kipindi cha kwanza Kagera walionekana kuwashika Simba na kufanikiwa kuongoza kwa goli moja lakini mabadiliko aliyoyafanya wakibadili mchezo na kufanikiwa kupata magoli mawili huku wakitengeneza nafasi nyingi za mgoli ambazo hazikuzaa matunda.

Kocha huyo amesema kuwa, Morrison ni mchezaji anayecheza kwa uhuru hivyo ikiwa ataanza katika mchezo huo basi wenzake watapashwa kumlinda.

Mchezo wao dhidi ya Yanga utakuwa na tofauti kubwa na ule uliopita kwani anatambua ushindani mkubwa uliopi katika mchezo huo wa ‘Kariakoo Derby’ na kwakuwa walitoka sare katika mchezo uliopita basi wanajipanga kushinda mchezo huo.

“Nishaona mechi kadhaa za Simba na Yanga na jinsi ushindani unavyokuwa, hivyo kazi kubwa iliyo mbele yetu ni kwenda kujiimarisha ili kuwa bora zaidi na kuweza kupata usnidhi ambao utatuhakikishia kubeba ubingwa wa msimu huu lakini pia kuwapa furaha mashabiki wetu kabla ya kuanza rasmi maandalizi ya mechi yetu dhidi ya Kaizer Chief katika hatua ya robo fainali na Ligi Mabingwa Afrika,” amesema kocha huyo.