-Uzinduzi wa msimu wa pili wa mashindano ya gofu ya NCBA yaongozana na upandaji miti Arusha.
Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Benki ya NCBA Tanzania imezindua rasmi msimu wa pili wa mashindano ya gofu ya NCBA. Mashindano haya yalifanyika kwenye uwanja wa gofu wa Gymkhana, Arusha. Mashindano ya mwaka huu yamelenga kuuinua mchezo wa gofu Tanzania, kama sehemu ya mkakati wa NCBA wa kutunza mazingira.
Mashindano ya gofu ya NCBA yamethibitisha kuwa ni zaidi ya mashindano, kwa kuwaleta pamoja wachezaji, mashabiki, na wadau wa gofu, na kuzidisha ushirikiano kati ya benki ya NCBA na wateja wake.
Kama sehemu ya maandalizi ya tukio hilo, Benki ya NCBA iliandaa hafla ya upandaji miti siku ya tarehe 28, mwezi Juni 2024 katika hospitali ya jiji, Arusha, ambapo miti 1,000 ilipandwa, ikiwemo miti ya kivuli 700, na miti ya matunda 300.
Juhudi hizi ni sehemu ya mkakati wa utunzaji mazingira wa NCBA kwa mwaka 2024; ambao umelenga kufanikisha upandaji wa miti 6,000 nchini Tanzania, sawasawa na dhamira ya serikali katika kutunza mazingira.
Claver Serumaga, Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya NCBA Tanzania, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huo katika dhamira moja.
“Kupitia ushirikiano wa mpango wetu wa gofu pamoja na juhudi za upandaji miti, tunaonyesha kujitolea kwetu kwenye mipango ya serikali katika utunzaji wa mazingira”. aliendelea kwa kusema
“Jambo hili linaendana na mpango wa kampuni yetu mama katika kukuza mchezo wa gofu ndani ya Afrika mashariki, kuhamasisha mambo mazuri kwenye jamii, na kutoa jukwaa kwa wachezaji wakubwa wa gofu, na wale wanaochipukia”.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa, na Michezo, mheshimiwa Damas Ndumbaro, ambaye alihudhuria tukio hilo kama mgeni rasmi, na pia alishiriki katika mchezo wa gofu, aliongelea ushirikiano wake kwa kusema;
“Serikali imefurahishwa kuona Benki ya NCBA ikichukua jukumu la msingi katika kuuinua mchezo wa golfu Tanzania. Mpango huu, ukijumlisha na upandaji wa miti, sio tu unakuza mchezo wa gofu peke yake, lakini inachangia katika juhudi za utunzaji wa mazingira, ikionyesha kuwa michezo inaweza kuleta mabadiliko chanya”.
Mashindano ya gofu ya NCBA yanalenga kubadilisha mtazamo wa wengi kuona golfu ni kwaajili ya wenye uwezo wa juu na wazee tu, kwa kuwakaribisha wote, ikiwemo wanawake, kujiunga na kushiriki.
Mashindano haya yanatoa jukwaa la kipekee kwa watu mbalimbali kutokea sekta tofauti, ili kufahamiana zaidi, na kuweza kushirikiana kwenye biashara.
Akizungumzia ushindani katika mashindano hayo, Serumaga alimpongeza mshindi wa kwanza ndugu George Ogutu akiongoza kwa kujinyakula pointi 41, Bwana Claver alimkabidhi mshindi huyo begi la gofu la kipekee kutoka NCBA lenye thamani ya Millioni 3 za kitanzania, pamoja na kulipiwa gharama na malazi kwenye safari ya kuelekea kwenye fainali za mashindano hayo, nchini Kenya.
Mabingwa hao wataonyesha ufundi wao wa gofu katika viwanja vya kupendeza nchini Kenya, na kufurahia vivutio vingine.
Bwana Claver Serumaga amewahamasisha wachezaji wa gofu nchini Tanzania kwa kusema;
“Baada ya hapa Arusha, mashindano ya gofu ya NCBA yataelekea Dar es salaam na baadae kuelekea Zanzibar, kabla ya fainali nchini Kenya. Wachezaji wa gofu kaeni tayari tutatangaza tarehe za kila mkoa hivi karibuni”.
Huku Benki ya NCBA Tanzania ikizindua msimu wake wa pili, Benki ya NCBA Kenya pia imetangaza kuanza msimu wao wa nne wa mashindano ya gofu ya NCBA, ikidhirisha nia ya pamoja kama kampuni, katika kuikuza gofu Afrika mashariki.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM