Na Waandishi Wetu, Dodoma
MFUMO wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ya Kodi, Maduhuli, Tozo na Huduma Mbalimbali za Serikali (GePG) unatajwa kusaidia kuokoa fedha nyingi za Serikali zilizokuwa zikipotea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo udanganyifu.
Akizungumza leo jijini Dodoma wakati akipokea Ripoti ya Tathimini ya Mfumo wa Kielektroniki ya Ukusanyaji wa Mapato na Usimamizi wa Fedha za Umma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, alisema kuwa mfumo wa GePG ulianzishwa Julai 2017 ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizokuwepo serikalini wakati wa ukusanyaji wa fedha za umma umesaidia Serikali kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zikipotea kutokana na changamoto mbalimbali.
Katibu Mkuu huyo ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni gharama kubwa za miamala inayohusu makusanyo ya fedha za umma, utaratibu usio rafiki kwa mlipaji wa huduma za umma, ugumu wa kupata taarifa ya makusanyo yanayofanyika kwa wakati huo huo, pamoja na machaguo machache ya njia za kulipia (Benki, Mitandao ya simu za mkononi au Mawakala) kwa sababu kuongeza machaguo kulikuwa kunaongeza gharama za ukusanyaji kwa taasisi.
“Mfumo wa GePG umewezesha kuongezeka kwa makusanyo ya Serikali kwa ujumla wake na kwa taasisi moja moja. Mfano makusanyo ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yameongezeka kutoka shilingi bilioni 95.0 kabla ya kuanza kwa mfumo hadi kufikia shilingi bilioni 115.0 kwa mwaka baada ya kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki”, amesema Doto na kuongeza;
“Wakala wa Vipimo umeongeza mapato yao kutoka kiasi cha sh. bilioni 1.0 kwa mwezi kabla ya mfumo wa GePG hadi kufikia kiasi cha sh. bilioni 2.5 kwa mwezi baada ya kujiunga na GePG.”
Pia, taasisi nyingine zimepunguza gharama walizokuwa wanalipia ada za miamala ya kielektroniki inayohusu makusanyo ya fedha za umma. Kwa mfano TANESCO ilikuwa ikilipa zaidi sh. bilioni 38 kwa mwaka kwa mawakala wa kuuza umeme. Baada ya kufunga mfumo wa GePG kwa sasa Shirika halilipi chochote..
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), William Erio alisema tangu shirika hilo lijiunge na mfumo huo mwaka 2019 umesaidia kutatua changamoto mbalimbi pamoja na kuongeza mtaji wa Shirika.
“GePG imeleta mabadiliko makubwa na imesaidia utendaji wa mfuko ambapo katika kipindi kifupi cha miaka miwili tu thamani ya Mfuko imeongezeka hadi kufikia asilimia 40, kutoka makusanyo ya shilingi bilioni 600 hadi kufikia shilingi trilioni 1.1 kwa mwaka”, alisema Erio.
Naye, Mhasibu Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Peter Mwakosya, amesema kuwa licha ya mfumo wa GePG kusaidia katika ukusanyaji wa mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali, mfumo huo umeondoa tatizo la hundi feki, malipo hewa pamoja na kupunguza matumizi ya akaunti za ukusanyaji wa fedha kutoka 30 hadi kufikia 5 zilizokuwa zikitumiwa na TFS.
Katika kukabiliana na changamoto za ukusanyaji na usimamizi wa fedha za umma, Wizara ya Fedha na Mipango imebuni mifumo mikubwa minne ya kielektroniki na kutengeneza na kusimamia mifumo minne ambayo ni Mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato ya Kodi, Maduhuli, Tozo na Huduma Mbalimbali za Serikali (GePG); Mfumo wa Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi na Malipo ya Serikali (MUSE), Mfumo wa Usimamizi wa Miradi ya Maendeleo (NPMIS) na Mfumo wa Usimamizi wa Misamaha ya Kodi.
Wasilisho hilo lilitolewa na Dkt. Joel Mtebe wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye aliongoza timu ya Tathimini ya Mfumo wa Kielektroniki ya Ukusanyaji wa Mapato na Usimamizi wa Fedha za Umma.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
27 kulipwa kifuta jasho Nkasi
Mwakilishi Mkazi wa UN nchini awasilisha hati