Na Iddy Lugendo, Timesmajira online
Geita Gold FC inatarajia kusajili wachezaji wapya nane, imefahamika kuwa Kocha Mkuu wa Geita Gold FC, Fred Minziro anaamini akipata nyota hao katika nafasi mbalimbali atakuwa na kikosi imara kitakachompa matokeo chanya.
Minziro alisema anaamini ujio mpya wa nyota hao utaimarisha na kikosi chake huku pia akianza maandalizi ya kusaka mechi mbalimbali za kirafiki.
“Ninatarajia kuongeza wachezaji nane kwa ajili ya msimu ujao, ninaendelea kufanya mazungumzo na wachezaji ambao ninawahitaji wajiunge katika timu yetu ili kuunda kikosi chenye ushindani kuelekea msimu ujao,” alisema Minziro.
Kocha hiyo alisema pia mara baada ya kumaliza mchakato wa usajili, atakiweka hadharani kikosi chake na programu rasmi ya mazoezi itakavyokuwa.
“Wiki ijayo tunatarajia kuanza kambi kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu itakayoanza Agosti 17, mwaka huu, tutajipanga zaidi ili kupata timu imara,” Minziro alisema.
Aliongeza anafahamu msimu ujao utakuwa na ushindani hivyo amepanga kuingia kambini mapema kwa lengo la kufanya marekebisho ya makosa aliyoyabaini wakati wanamaliza ligi ili kuanza msimu mpya kwa kasi.
Geita Gold FC ilimaliza msimu uliopita ikiwa katika nafasi ya nne na imekata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria