October 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Gazeti la The Citizen latakiwa kumlipa Mchechu bil.2.5/- kwa kumshusha hadhi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MAHAKAMA Kuu Jijini Dar es Salaam, imetoa hukumu katika kesi namba 48 ya 2021 ya Nehemia Mchechu dhidi ya Gazeti la the Citizen ambapo Gazeti hilo limetakiwa kumlipa Mchechu Shilingi Billioni 2, milioni 500 zikiwa ni ghrama za jumla pamoja na kuomba radhi na kuandika tena habari hiyo ikiwa imerekebishwa, kwa kuchapisha katika ukurasa wa mbele wa gazeti hilo.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam mbele ya Jaji Leila mgonya ambapo gazeti hilo limetakiwa kutoa sh.milioni 12 kila mwaka kama watakaa na pesa hizo tangu shitaka limesomwa mpaka siku watakapolipa.

Wakili wa Mchechu, Aliko Mwamanange amesema baada ya taarifa ile kutolewa katika gazeti hilo, Mchechu akaona kwamba imemshushia hadhi kwenye macho ya Watanzania na nje ya mipaka ya Tanzania ndiyo akaamua kwenda mahakamani kulalamika.

“Malalamiko yalikua yamelenga kusema kwamba yamemshushia hadhi na yalianza siku moja huko Dodoma wakati utawala uliopita wa hayati Rais John Pombe Magufuli alipokuwa anazindua mradi aliongea maneno ambayo hayakutoa kikamilifu yale yote ambayo yaliandikwa kwenye gazeti hivyo gaazeti la The Citizen wakaongeza maneno fulani kwenye gazeti hilo”

Akifafanua kuhusu muda wa gazeti hilo kulipa faini hiyo, wakili huyo amesema gazeti hilo hawajapewa muda wa lini walipe lakini kwa kawaida kama wanatakiwa kulipa, walipe kabla hawajafanya utaratibu wa kwenda kukata rufaa.

Mchechu alilishitaki gazeti hilo wakati akiwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Nyumba la Taifa (NHC), katika Mahakama kuu ya Tanzania kwa kuandika habari iliyochapishwa katika toleo lake la Machi 23, 2018 ikiwa na kichwa cha habari kilichosomeka ‘ Why JPM dissolved NHC Board, Sacked Mchechu’ ; kwa tafsiri isiyo rasmi ‘Kwa nini JPM alivunja Bodi ya NHC, Kumfukuza Mchechu’

Mchechu alidai kuwa habari hiyo ina upotoshaji mkubwa kimantiki na kimaudhui kwa kuwa hawajawahi kufukuzwa kazi na Hayati John Pombe Magufuli kama habari hiyo ilivyodai.

Katika habari hiyo iliyokuwa imebeba habari kubwa ukurasa wa mbele ya kuwekwa ukurasa wa nne, ilidaiwa kuwa Mchechu alikuwa akichunguzwa na Bodi ya NHC na kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) juu ya mgongano wa kimaslahi juu ya utafutaji na upatikanaji wa ekari 500 za mradi wa NHC wa Safari City jijini Arusha.

Ilidaiwa kuwa ardhi hiyo, awali iliripotiwa kununuliwa na kampuni inayomilikiwa na Mchechu ambayo iliinunua kutoka kwa raia wa kigeni na uchunguzi ulionyesha kuwa aliiuzia NHC kwa bei ya juu.

Pia kwa mujibu wa habari hiyo, Mchechu alidaiwa kumtumia mkandarasi wa NHC kutengeneza barabara kwenda kwenye eneo lake lililo karibu na eneo la mradi wa Safari City huku gharama zikiwa zinabebwa na shirika.

Sambamba na hayo, taarifa hiyo ilidai kuwa kampuni ya PHILS International ya Dubai ilipewa kazi katika mradi wa Kawe kwa uamuzi wa Mchechu bila kumhusisha Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi cha NHC, Hamis Mpinda.

Aidha, habari hiyo ilidai kuwa uchunguzi ulikuwa unafanywa kuhusu madai ya kampuni ambayo mke wa Mchechu ni mkurugenzi kupewa mkataba wa kutoa bima kwa ajili ya nyumba za shirika mkoani Mtwara jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za utumishi wa umma juu ya mgongano wa kimaslahi.

Kadhalika, kwa mujibu wa habari hiyo, vyanzo vya habari vilibainisha kwamba kamati iliyoundwa kuchunguza matumizi mabaya ya ofisi ndani ya NHC ulionyesha ukiukwaji mkubwa na matumizi mabaya ya kutisha ya fedha za umma uliofanywa na Mchechu.