Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Arusha
MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini Mrisho Gambo amesema Benki ya CRDB imekuwa ikitoa mchango mkubwa kwenye jamii kwa kurudisha faida wanayopata kwa kujenga miundombinu ya shule ikiwemo vyumba vya madarasa, madawati, vituo vya afya, zahanati na vifaa tiba.
Aliyasema hayo Mei 17, 2023 kwenye hafla ya Benki ya CRDB kukabidhi vyumba viwili vya madarasa kwenye Shule ya Sekondari Kalimaji, Kata ya Moshono, vilivyojengwa kwa ufadhili wa benki hiyo kwa gharama ya sh. milioni 42
“Benki ya CRDB imekuwa ni mtu mwema kwetu na kwa jamii ya Watanzania kwa kurudisha faida kwa wananchi. Wamefanya mambo mengi sio kwetu tu bali nchi nzima, kwani wamejenga kila mahali vyumba vya madarasa, madawati, vituo vya afya na mambo mengine.
“Hata hii shule hapa tulipo bila CRDB, leo tusingekuwa na shule hii. Wao ndiyo watu wa kwanza kujenga vyumba vya madarasa kwenye shule hiii. Ingekuwa hatuna uchoyo, shule hii tungeita CRDB Benki Sekondari School. Niseme, CRDB haina mpinzani, na kama yupo, basi ana kazi kubwa ya kufanya” alisema Gambo.
Gambo alisema wana mpango wa kujenga mabweni mawili kwenye shule hiyo iliyoanza masomo Januari, mwaka jana kwa gharama ya sh. milioni 150, ili kuwasaidia wanafunzi wanaotoka mbali, kwani hata kuanzishwa kwa shule hiyo, kulitokana na wanafunzi kutembea umbali wa kilomita sita kwenda shule.
Gambo alimuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Group Abdulmajid Nsekela kuwasaidia kununua kompyuta kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Akizungumza na hadhara hiyo, Nsekela alikubali ombi la kuwanunulia kompyuta wanafunzi wa shule hiyo kwa kutoa sh. milioni 10, na kuongeza kuwa Benki ya CRDB ipo tayari kushirikiana na jamii na kuisaidia Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwaletea wananchi maendeleo.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa ambaye alikwenda kwenye hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella, alisema kwa kuwapatia vyumba viwili vya madarasa ni kwamba wanaunga mkono juhudi za Serikali, na wao wamekuwa ni Wazalendo kuona jamii inaneemeka kwa kuwepo benki hiyo hapa nchini.
“Kwa kutupatia haya madarasa, Benki ya CRDB ni Wazalendo, na wanamuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia wamesaidia Jiji la Arusha na kutatua mahitaji ya shule. Wenzetu Benki ya CRDB wametupa madarasa haya, hii ina maanisha tunapunguza msongamano wa wanafunzi kwenye shule na kuongeza ufanisi.
“Na hata walimu watapa utulivu kwenye kufundisha.. Niseme naguswa sana na Benki ya CRDB ilivyokuwa karibu na wananchi” alisema Mtahengerwa.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi