November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

G20 wahaidi kusaidia soko la ajira

RIYADH, Mawaziri wanaohusika na maslahi ya wafanyakazi na ajira wa kundi la mataifa yaliyostawi kiuchumi (G20) wameahidi kulisaidia soko la ajira lisiporomoke huku janga la virusi vya corona (COVID-19) likiathiri kazi kote Duniani.

Mawaziri wa kundi hilo ambalo kwa sasa linaongozwa na Saudi Arabia wamesema kwamba mataifa yao yataendelea kutafuta njia za kusaidia biashara na waajiri, hasa biashara ndogondogo na za kati, kuweza kutunza ajira na kusaidia wafanyakazi walioathirika katika kipindi hiki kigumu.

Shirika la Kazi Duniani (ILO) lilionya Jumanne kuwa, athari za kiuchumi za mlipuko wa virusi vya corona zinawaumiza vibaya wafanyakazi na waajiri katika sekta zote.
Pia shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilieleza kuwa,wakati wowote vikwazo vikiondolewa, basi wafanyakazi wanapaswa kurudi kazini wakiwa na ulinzi sahihi ili kuzuia kutokea tena kwa janga hilo.

Wafungwa

Wakati huo huo, wakati juhudi mbalimbali zikiendelea za kuhakikisha mataifa mengi yanapunguza mikusanyiko ili kupunguza kasi ya ueneaji wa virusi vya corona, Saudi Arabia inadaiwa kushikilia misimamo ya kutowaachilia huru wafungwa.

Msimamo huo unashikiliwa, licha ya matakwa ya kila mara ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS), asasi za haki za binadamu na familia za watu wanaoshikiliwa huko Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa Gazeti la Lebanon la Al-Akhbar lilimnukuu mmoja wa viongozi wa Harakati ya HAMAS akisema kuwa, viongozi wa Saudi Arabia wamekataa kutoa jibu lolote kwa wapatanishi wanaoingia nchi hiyo kwa ajili ya kufuatilia suala la kutatuliwa faili la Wapalestina wanaoshikiliwa nchini humo.

Aidha, kwa mujibu wa afisa huyo wa HAMAS, viongozi wa Saudi Arabia wanadai kuwa suala la mahabusu hao linahusiana na usalama wa ndani wa nchi hiyo.

Hivi karibuni, Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Palestina (HAMAS) aliwasiliana na Saadeddine Othmani, Waziri Mkuu wa Morocco na kumtaka awe mpatanishi kuhusiana na suala la kuachiliwa huru Wapalestina wanaoshikiliwa na utawala wa Riyadh.

Tangu mwaka jana, Saudi Arabia imewatia mbaroni zaidi ya Wapalestina na Wajordan 60 kwa tuhuma zinazohusiana na kuwa wanachama wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS).