Na David John,Timesmajiraonline
MKURUGENZI wa Ukuzaji Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya biashara Tanzania (TanTrade) Fortunatus Mhambe na Kaimu Mkurugenzi wa TCCIA wamebainisha kufungua kwa Soko la AfCFTA walipokutana na kufanya mazungumzo na Mfanyabiashara wa Kwanza Tanzania kutoka kampuni ya kizawa ya EXPORT TRADING GROUP ( ETG).
Amesema Kampuni hiyo imenufaika na mkataba wa eneo huru la biashara Afrika (Africa Free Continental Trade Area) kwa kusafirisha kontena 9 ambazo ni sawa na tani 172.8 za kahawa ya kitanzania aina ya robusta kutoka Tanzania Kwenda Algeria na kupata punguzo la kodi la asilimia 23 kupitia cheti cha uasilia wa bidhaa (Certificate of Origin) kinachotolewa na TCCIA.
Mkurugenzi huyo ameyasema hayo Leo Mei 9 mwaka huu ambapo amesema hayo yote ni moja kati ya juhudi kubwa zilizofanywa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha Uwekezaji na kuimarisha mazingira ya wafanyabiashara nchini na imeleta matokeo chanya katika ukuzaji wa biashara nchini.
Amesema Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara kupitia TanTrade inapenda kutoa wito kwa Watanzania wengi zaidi kuendelea kujitokeza na kuchangamkia fursa zinazopatikana katika mpango wa eneo la Soko Huru Afrika.
“Napenda kuwahamasisha Watanzania Kuchangamkia fursa hizo za unafuu wa kodi zinazopatikana katika soko hilo, kwani hii itatusaidia Watanzania kutokuwa wasindikizaji bali watendaji na walaji wa fursa hizo, hivyo Watanzania wengi zaidi wajitokeze TCCIA kuchukua Cheti cha Uhasilia wa bidhaa ili kuweza kupata unafuu huo na kupunguza gharama za kodi zitakazowasaidia kuongeza mitaji na kupanua uchumi wa mtu binafsi na Taifa kwa ujumla, hivyo kuwasaidia Watanzania wengi zaidi kuuza na kutangaza bidhaa zinazozalishwa na Tanzania kwa unafuu zaidi, Amesema.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa TCCIA Vincent Minja amesema kuwa kwa mara ya kwanza Tanzania inatoa cheti cha uasilia kinachomnufaisha Mtanzania wa kwanza kufanya biashara katika eneno la Soko Huru Afrika na kupata unafuu wa kodi kwa asilimia 23, kwani alitakiwa achajiwe kodi ya forodha kwa asilimia 35 lakini akupitia cheti cha uhasili amechajiwa asilimia 12 tu.
“Napenda kutoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa za unafuu wa kodi zinazopatikana katika Mkataba huu kwa kuja TCCIA na kuchukua cheti cha uasilia ili kulipa kodi kidogo na kutanua biashara zao,”amesema.
Naye Mfanyabiashara kutoka katika kampuni ya kizawa ya ETG ambayo imenufaika na mkataba huo Shaban Hamis Fwalo ameishukuru Serikali kupitia TanTrade kwa kuendelea kuwapigia Wafanyabiashara na kuwapa elimu kubwa inayosaidia kurahisisha ufanyaji wa biashara zao.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kutufungulia fursa za kurahisisha utendaji wa biashara zetu kuwa nafuu, kwani ilipaswa tulipe kodi ya ushuru wa forodha kwa asilimia 35 lakini kupitia mkataba huu tumelipa asilimia 12, hii itatuletea wateja wengi Zaidi kutokana na unafuu wa kodi na itasaidia kutanua soko la bidhaa zetu,”amesema.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini