December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Furaha ya CHADEMA ni matunda ya Rais Samia

Na Markus Mpangala,TimesmajiraOnline,Dar

KWA muda wa miaka mitano na siku 114 vyama vya siasa havikuwa na fursa ya kufanya mikutano ya hadhara kama sehemu ya shughuli ya siasa nchini. Hata hivyo mabadiliko ya uongozi yaliyotokea Machi mwaka 2021 yamemshuhudia kuinuka tena kwa shughuli za kisiasa huku vyama vya siasa vikiwa vimepata nafasi ya kushiriki kwa dhati.

Katika mambo ambayo yalikuwa ynanisumbua ni kuelewa namna gani Rais Samia Suluhu Hassana atawaponya na kuwatuliza wanasiasa wenzake katika shughuli za siasa.

Kwa kazi yangu ya uandishi ilinikutanisha na wadau wengi ambao walitamani kuona Tanzania inarudi kwenye siasa za majukwaani kwa wananchi kupata fursa za kuhudhuria mikutano ya hadharani inayoitishwa na vyama vya siasa au wanasiasa mbalimbali nchini.

Mwaka 2021 ulimalizika bila tangazo lolote la Rais Samia la kuagiza kurejeshwa mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Kimsingi matumaini ya wananchi wa pande zote za kisiasa yalikuwa kuona Rais Samia anafanya upepsi kurudisha mikutano hiyo.

Lakini haikuwa hivyo, Rais Samia alimaliza mwaka huo kimya kimya na ilionesha wazi ndicho kipimo kingine cha kisiasa alivyokuwa anatakiwa kukivuka. Kilikuwa kipimo ambacho Rais Samia alidhihirisha kwamba licha ya Katiba kuagiza mikutano hiyo kuwa ni haki, lakini nafasi ya Rais wa Jamhuri ya muungano kutoa tamko lake na kutekelezwa ni kubwa.

Ni sababu hiyo maelfu ya wananchi wa Tanzania walikuwa wakisubiri tamko la Rais Samia kuhusu shughuli za kisiasa.

Rais Samia na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe

Tamkoa la Rais Samia lilikuwa muhimu ndilo tamko rasmi la Rais ambalo Katiba inamruhusu kufanya uamuzi wowote kadiri anavyoona kwa maslahi ya nchi. Rais Samia alivuka kipindi hicho na kuwafanya wanasiasa waone hana nia njema na shughuli za kisiasa hapa nchini.

Kwa kutambua hilo Rais Samia alionesha msimamo na kutotetereka kwa kuhakikisha tamko lake kuhusu shughuli za kisiasa lingekuja wakati ambao ameridhishwa na kile alichokipanga.

Uthibitisho wa hilo ni hotuba yake iliyosema “nasimamisha na kufungua nchi” akiwa amelenga kutekeleza kwanza mikakati iliyokuwa mezani kwake kuhusu marekebisho kadhaa ya masuala ya uongozi nchini.

Alianzia shughuli za diplomasia, afya, uchumi na ziara kadhaa katika nchi za Afrika nan je ya Afrika.

Rais Samia aliendelea na shughuli hizo huku akichora ramani yake ya kisiasa kuhusu namna anavyotaka nchi iendeshwe na wanasiasa wanapaswa kufanya nini kwa maslahi ya wananchi.

Kana kwamba haitoshi Rais Samia katika kuadhimisha siku ya Demokrasia nchini aliandika makala mazuri ambayo yalionesha ramani yake kwenye siasa.

Rais alisema anahitaji siasa za kistaarabu na wanasiasa wanaweza kuendesha mikutano bila matusi,kuvunjiana heshima na kutupiana kashfa.

Baada ya hapo Rais Samia alifanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya siasa mbalimbali pamoja na kukutana na nao kwenye Jukwaa la vyama huku akishauriwa kuendelea kuongoza vizuri nchi yetu.

Samia hakuishia hapo, alikutana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambapo ajenda kuu ilikuwa maridhiano.

Katika mikutano yao viongozi hao wawili walikubaliana na kuendesha siasa za kistaarabu kwa maslahi ya nchi. Katika kipindi hicho ndipo Rais Samia alileta falsafa yake ya R4 yenye kulenga maridhiano,Amani na ustaarabu miongoni mwa wadau na viongozi wa kisiasa bila kuwasahau wananchi.

Haijalishi mafanikio ya R4 yamefikia kiasi gani lakini furaha iliyopo sasa katika mikutano ya hadhara na maandamano yanayofanyika sehemu mbalimbali nchini ni matokeo ya maono ya Rais Samia kuwaachia watu uhuru wa kujieleza pasipo kutweza haki za wengine.

Samia kama kiongozi mkuu wa nchi alijaribu kulinda taswira ya serikali ya Tanzania, kisha akajenga taswira ya hali ya demokrasia. Kwa kipindi cha miaka mitatu, serikali ya awamu ya sita imefanikiwa kuwaachia uhuru wa kujieleza hali ambayo inawapa furaha wanasiasa na manazi wao. Kuanzia Chadema,ACT Wazalendo na wengineo wamekuwa kwenye mchakamchaka wa kisiasa na kuitengeneza taswira ya kidemokrasia kuwa yenye kulinda haki na kuheshimu uhuru wa watu wengine.

Samia wakati akifanya hivi, yeye ameruhusu wasaidizi wake ndani ya chama kuhakikisha wanafanya siasa za kistaarabu.

Mathalani, katika siasa kumeshuhudiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Paul Makonda akizunguka sehemu mbalimbali kuwahutubia wananchi na kusikiliza kero zao na kukiuza vizuri chama cha CCM.

Hali kadhalika Chadema nao wapo kwenye mikutano na maandamano ya Amani kwa kila mkoa, ambako walianzia mkoa wa Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na kisha wakaelekea Arusha.

Hii ni taswira ambayo inamfanya Rais Samia kuwa mjenzi wa nuru ya kisiasa inayoendelea hapa nchini.

Anaweza kuzungumziwa kwa namna yoyote ile lakini haiwezekani kunyimwa maua yake kuhusu hali ya kisiasa nchini. Amedhihirisha kudhibiti mihemko ya kisiasa pamoja na kuweka dira muhimu ya nini kinachopaswa kufanyika katika mikutano hiyo.

Kimsingi ameelekeza, amesimamia,ameonesha dira,amewapa uhuru wasaidizi wake ndani ya chama chake kuwapa uhuru wa kupambana kisiasa na wanasiasa wa vyama vya upinzani.

Kwamba amejaribu kutenganisha shughuli za chama na serikali. Kwamba CCM wanaweza kuendesha hekaheka za siasa kwa kunyukana na wapinzani wao bila serikali kutia mkono wake.

Hayo ni machache kati ya mengi ambayo Rais Samia ameyafanya kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake.
Baruapepe: mawazoni15@gmail.com