Judith Ferdinand,Mwanza
Tukiwa katika maadhimisho ya siku 16,za kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto, wanawake wametakiwa kutokubali vikwazo vilivyopo kuwakwamisha katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika nyanja mbalimbali.
Tukiangazia uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa Mkoa wa Mwanza uliofanyika Novemba mwaka huu,je ni wanawake wangapi wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali ndani ya chama na namna walivyoweza kukabiliana na vikwazo ikiwemo mfumo dume ambao umezoeleka.
Florah Magabe,Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mwanza,ambaye amefanikiwa kutetea kiti hicho kwa mara pili anaeleza namna alivyoweza kuvuka vikwazo na kufanikiwa kutetea nafasi hiyo akitokea Wilaya ya Nyamagana.
Akizungumza na TimesMajira Online ameeleza kuwa mchakato wa uchaguzi ndani ya chama kwa mwaka huu umekuwa na changamoto sana.
“Kwa sababu ni mchakato ambao umekuwa mgumu kwa sababu umehusisha nguvu ya fedha,ukiwa na fedha unakuwa na urahisi wa kupenyeza na kushinda katika nafasi ambayo unaiwania,”ameeleza Flora.
Sababu za wanawake kutojitokeza kuwania nafasi mbalimbali
Flora ameeleza kuwa,katika mchakato wa uchaguzi wa CCM kwa Mkoa wa Mwanza wanawake wengi hawakujitokeza kuwania nafasi mbalimbali ukilinganisha na wanaume ambao idadi ya wanawake ili kuwa ndogo huku wanaume ikiwa kubwa.
Hii imetokana kwanza na mfumo dume uliopo ambao umewafanya wanawake wengi kutojiamini kwamba wanaweza kugombea na wakachaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama na sehemu nyingine.
Anaeleza kuwa kutokana na kutojiamini imesababisha kushindwa kujitokeza kuwania nafasi ya juu kabisa ndani ya chama ambayo ni ya Mwenyekiti CCM Mkoa ambapo wagombea wake walikuwa wanaume.
“Katika jamii yetu hii ya kusukuma,ukienda vijijini asilimia kubwa hawaamini sana kama mwanamke anaweza akaongoza hii imekuwa ikisababisha wanawake kutojitokeza sana kuwania nafasi mbalimbali ukilinganisha na wanaume,”anaeleza Flora.
Pia anaeleza,kuwa sababu nyingine ni kuwa uchaguzi ni mchakato ambao una uhusiano wa karibu na matumizi ya fedha.
“Tumeona kwa uchaguzi huu wa mwaka 2022 ukilinganisha na chaguzi zingine zilizo pita na mimi nimeisha pita katika chaguzi hizo, zimekuwa zikihusisha fedha kwa karibu,”anaeleza Flora.
Kwaio katika mchakato wa uchaguzi wanawake wengi hawana fedha,hivyo mtu mwingine anajikatia tamaa,kwamba naenda kushiriki uchaguzi lakini je fedha nitatoa wapi ya mchakato mzima pamoja na kumuwezesha kuwashawishi watu waweze kumchagua.
Pia anaeleza kuwa wanawake wengi wana nyongonyea kujitokeza kwa wingi kushiriki mchakato wa kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi kutokana na mfume dume,fedha,mila na desturi.
“Kitu kimoja tunapoadhimisha siku 16 za kupinga ukatili,ni pamoja na suala la rushwa katika chaguzi ikiwemo ya ngono na maneno mengine yote ambayo yanadhalirisha utu wa mwanamke,yamekuwa ni visababishi vikubwa vinavyochangia wanawake wengi wasijitokeze kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya vyama na mahali pengine,”.
Hamasa kwa wanawake kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Licha ya changamoto zote lakini jamii kwa uzuri ikiisha ona mwanamke ana uwezo ni rahisi kumuamini na kumpa nafasi ya kuongoza.
Anaeleza kuwa watu wengine wanaangalia uwezo ulionao,kama umeshiriki shughuli nyingi za kijamii na wameona uwezo wako ni rahisi kukuamini na kukupa nafasi ili uweze kuchaguliwa katika nafasi nyingine.
“Tunapo adhimisha siku hizi 16 za kupinga ukatili, zitukumbushe sisi wanawake kuwa ili tushinde ni lazima tusimame kwenye nafasi zetu ili tushindane na vyote vinavyochangia sisi kurudi nyuma ikiwemo kushindana na suala la rushwa,yani siyo kuwa una shinda kwa sababu umetoa rushwa ya ngono au fedha bali ni Kwa uwezo ulio nao,”anaeleza Flora.
Aidha amewatia shime wanawake wenzake kuwa badala ya kukaa na kusema kuwa huu ni mfumo dume, wanawake hawawezi kushindana nao au hawana fedha bali wasimame imara na kufanya kile wanacho kiamini.
“Lazima tusimame kwenye nafasi zetu,tusilaani giza tu kwa kuliacha giza liwepo,lazima tuwashe mshumaa ili giza liondoke,tuna washaje mshumaa kwa kushiriki mchakato katika kuingia kwenye nafasi za maamuzi haijalishi tuna fedha au hatuna fedha,”
Namna alivyoweza kupata ushindi katika kinyanganyiro cha nafasi ya Ujumbe Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mwanza katika uchaguzi wa Chama mwaka huu
Anaeleza kuwa kwa nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu CCM Mkoa,jumla walikuwa wagombea 13 kati yao wanawake 3 na wanaume 10 kwa Wilaya ya Nyamagana ambapo kwa bahati nzuri kwa Wilaya hiyo walishinda wanawake.
Changamoto ilikuwepo kwa sababu walikuwa wanashinda nao ni watu wazito wenye ujuzi wa kutosha lakini kwa sasa jamii imeanza kuona imani na uwezo walio nao wanawake wanapo wapa nafasi.
“Hatuja shinda kwa sababu ya kuonewa huruma,ila tumeshinda kwa sababu ya uwezo wetu wa uongozi,na wametupima katika hayo nimekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Mkoa hii ni mara yangu ya pili,”.
“Maana yake wapiga kura walio nichagua kipindi kile wameona kazi zangu nilizokuwa nafanya mfano mwaka 2020 niliwezesha vifaa vya kujikinga na uviko-19 ikiwemo vitakasa mikono Kata zote 119, katika Wilaya zetu zote 7 za Mkoa wa Mwanza,”.
Pia anaeleza kuwa sababu nyingine ya kuaminiwa ni kutokana na uwezo wake pamoja ushirikiano aliouonesha awali pamoja na kuwa na jamii katika shida na raha ikiwemo shughuli za kampeni na kuhakikisha chama chao kina shika dola.
“Mchakato wa uchaguzi Mkuu na serikali za mitaa,ushiriki wangu katika kujenga na kuimarisha chama,ndicho kilicho nipima na kuona kwamba ninatosha na ninaweza kuongoza,niwatie moyo wanawake wenzangu fedha tu siyo suluhu ya kila kitu tunapo shindana katika ulimwengu huu ambao unaangalia vitu kuliko uwezo ni muhimu tuoneshe uwezo wetu zaidi ili waendelee kutuamini na kutupa nafasi za kuongoza,”
Nini msimamo wake katika safari ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Flora anaeleza kuwa uwezi kuna mstari mwembamba unaotenganisha fedha na uchaguzi, ukiwa na fedha unapata urahisi katika mchakato wa uchaguzi je ni wanawake wangapi wana fedha,wengi unakuta hawana hizi fedha pia katika fedha kuna mstari mwembamba kati ya rushwa na uchaguzi.
Ambapo wao wanawake wanakutana na rushwa za ngono,rushwa za fedha lakini ukisimama imara ukaamini unacho kiamini na kuendelea kuwatumikia wananchi na kuonesha uwezo wako ni rahisi kukuamini na jamii inaona Florah au fulani ni tofauti na watu wengine ana uwezo wa kutuongoza na kutuwakilisha.
“Mimi naitwa Flora Magabe a.k.a wanapenda kuniita Iron Lady,ni askari ambaye nimekuwa mstari wa mbele nisiye kimbia uwanja wa mapambano,ninasema haya kwa maana kwamba ni mtu yule ambaye ninasimamia kile ninachokiamini haijalishi napitia changamoto ipi,”anaeleza na kuongeza kuwa
“Nimewania nafasi nyingi nimeisha gombea nafasi ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)Mkoa wa Mwanza kura hazikutosha,nimegombea tena kiti hiki kura hazikutosha,nimetetea nafasi yangu ya Ujumbe Halmashauri CCM Mkoa,nimepata kwaio mimi ni mwanamke ambaye ninajiamini na ni askari,”.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza azungumzia nafasi ya mwanamke katika uongozi ndani ya chama kwa Mkoa wa Mwanza
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Omar Mtuwa, anaeleza kuwa chama hicho kina tambua na kuthamini wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi.
“Katika Ilani yetu ya uchaguzi ya 2020-2025,ina mtaja mwanamke na Chama chetu cha CCM kimefika mbali kwa sababu ya mwanamke,tangu enzi na enzi imeanzisha Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), ambapo wanao shiriki katika nyadhifa za uongozi ni wanawake tu na ndio,hao hao wanaruhusiwa kugombea nafasi nyingine za uongozi ndani ya chama”anaeleza Mtuwa.
Wanawake wakiwa na umri unaruhusu watagombea nafasi katika Umoja wa vijana wa CCM,nafasi ya wazazi nafasi za chama,kwaio unajikuta chama hicho wanawake ni wengi kutokana na kuwa wamechanganyika kupitia jumuiya na chama,
Hivyo chama kinamtambua mwanamke,nguvu yake na uzoefu wake katika taifa na ndio sababu nchi hiyo kwa sasa inaongozwa na wakina mama na kazi zinaonekana na wananchi wanaishi kwa amani.
Akizungumzia uchaguzi wa CCM Mkoa wa Mwanza,Mtuwa anaeleza kuwa licha ya chama hicho kumtambua mwanamke katika nafasi ya uongozi bado hawajitokezi kuwania nafasi za juu za uongo ndani ya chama mfano ya Mwenyekiti CCM Mkoa katika uchaguzi wa chama mwaka huu waliojitokeza wanaume tupu.
Hivyo anaeleza kuwa sababu ya wanawake kutojitokeza kuwania nafasi hizo ni kutokana na heshima pamoja na woga walionao.
“Waligombea katika nafasi za ujumbe wa NEC Mkoa, Mjumbe Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa lakini nafasi ya Mwenyekiti wanaona ni nafasi ya mwanaume na si yao,nitajitahidi katika chaguzi zijazo kuwaelimisha ili nao waone kuwa wana haki ya kugombea nafasi kubwa ya uenyekiti ndani ya chama,”anaeleza.
Pia anaeleza kuwa wanawake waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho kwa Mkoa wa Mwanza ni wengi lakini upande wa Ujumbe wa NEC Mkoa mwanamke alikuwa mmoja na wanaume wawili ingawa aliyeshinda ni mwanaume.
Lakini nafasi ya Mjumbe Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa,kila Wilaya walikuwa hawakosi wagombea wanawake.
“Tumepata mwanamke mmoja kutoka Wilaya ya Ukerewe, Ilemela,tuna wanawake wawili kutoka Nyamagana kwaio kati ya watu 14 ambao ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa nusu yake ni wanawake walioshinda katika uchaguzi wa mwaka huu ngazi ya Mkoa,”anaeleza Mtuwa.
Anaeleza kuwa hakuna chama cha siasa nchini kinachotekeleza usawa wa kijinsia kwa kila hali na Makundi kama CCM ikiwemo nafasi ya uongozi.
“Ukienda kwenye ulemavu CCM tunatekeleza,vijana CCM tunatekeleza,wazee CCM tunatekeleza lakini pia ukija kwenye suala la kinamama CCM tunatekeleza ndio maana unaona tuna usawa wa wanawake tunao nusu kwa nusu kwenye uongozi,”.
Pia anaeleza kuwa katika vikao vyao vya maamuzi Katiba ya chama inawataka kuangalia suala la jinsia na izingatiwe ambapo Kamati ya siasa uwezi kutwa bila kuzingatia usawa wa kijinsia kadhalika kamati ya maadili na kamati ya udhibiti na nidhamu.
Mdau wa kutetea haki za wanawake na watoto, anena
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea wanawake na watoto la Hakizetu Gervas Evodius, anaeleza kuwa uongozi ni una nafasi kubwa ya kubadilisha vitu ambavyo vinaonekana kwenye jamii aidha vinavyoenda sawa au haviendi sawa.
“Mara nyingi tumekuwa tukusema wanawake wapo wengi ata Tukiangazia kwenye matokea ya sensa ya mwaka huu idadi ya wanawake ni wengi kuliko wanaume lakini kwenye ngazi za uongozi wanawake ni wachache,”.
Anaeleza kuwa uongozi unaangalia kuanzia chini shuleni je?, wasichana wangapi ni viranja na kwenye elimu ya juu wasichana wangapi ni Marais wa vyuo na kwenye vyama vya siasa je?,wanawake wangapi ni Wenyeviti wa vyama vya siasa na ni makatibu wakuu wa vyama vya siasa.
Je,ni wanawake wa ngapi wapo kwenye nafasi za juu za vyama vya siasa ambavyo vinakwenda kutoa mustakabali wa uongozi wa taifa.
“Bado tuna safari ndefu ya kufikia asilimia 50/50 kwa sababu katika vyama vingi vya siasa nafasi kubwa za juu asilimia kubwa wanakuwa wanaume mengi na wanawake ni wachache au wasiwepo kabisa,”.
Pia anaeleza kuwa sababu ya wanawake wengi kutojitokeza kuwania kwenye nafasi za uongozi,baadhi waliojitokeza lakini hawakuwa na nguvu ya kutosha aidha ya ushawishi au ya kifadha.
“Tunafahamu kwamba uchaguzi unahitaji fedha mfano kwenye chaguzi za serikali inahitajika unigharamie kampeni,uchukue fomu kwa fedha zako,hivyo vyote vinahitaji fedha na wanawake wengi hawana uwezo kiuchumi ili kuweza kumudu vyote,”.
Sababu nyingine ni kuwa jamii bado haija waruhusu wanawake kuwa viongozi na ukikuta mwanamke ni kiongozi jua amekwepa mishale mingi sana.
“Mwanamke kufikia kuwa kiongozi kuna vitu vingi sana kuna rushwa za ngono wakati mwingine,kudharauliwa na kukatisha tamaa kutoka kwa wanaume na wakati mwingine kwa wanawake wenyewe,kwanini inapotokea mgombea urais ni mwanamke wanawake wenzake hawamuungi mkono kwa kumpigia kura na tunajua wanawake wana nguvu kubwa,”.
Mfano chama A labda kimemsimamisha mwanamke katika nafasi ya urais lakini matokea yakitoka anakuwa kashika nafasi ya tano au sita akitanguliwa na wanaume wakati waliopiga kura kwa wingi ni wanawake lakini hawajamchagua mwenzao.
Hivyo bado wanawake hawajaamua kuingia kwenye madaraka hasa yale makubwa lakini waliamua tu hata leo watakuw na mara nyingi wamekuwa wakishiriki kama wapiga kura na siyo wagombea na wanatumia haki ya kuchagua na siyo kuchaguliwa.
Hata hivyo anaeleza kuwa ili wanawake waweze kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi lazima waweze kulelewa kwenye misingi ambayo itakuwa inawaanda wenyewe kuchukua uongozi.
Kwani hauwi kiongozi bora kwa sababu wewe ni mwanaume au mwanamke bali ni Kwa sababu ya ujuzi na uwezo ulio nao.
Kama shirika wana mpango kazi wao wa 2023/25 wameangalia kwa upana zaidi suala la wanawake katika uongozi kwani wameona kuna haja ya kuwafunza na kuwaelea watoto wadogo wakiwa bado ili kuwa viongozi.
Wasichana wakiandaliwa bado wadogo na kuanza kuwania nafasi mbalimbali wakiwa bado chini mfano yupo shule ya msingi akawania nafasi ya uongozi ya kuwa kiranja,akifika chuo akawania nafasi ya urais wa chuo au nafasi nyingine unakuwa umeanza kumlea katika mfumo wa uongozi.
“Viongozi wanaandaliwa,kwani uwezi kuwa kiongozi ghafla utakwama sehemu,na Ili uwe na viongozi bora lazima uandaliwe changamoto ya kuwa na kiongozi ambaye hajaandaliwa ni kuwa hatoweza kumudu presha,”.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika