January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Fikira za Rais Samia zaanza kubadili vijana kupitia unenepeshaji mifugaji

Na Mwandishi Wetu,TimesMajiraOnline

MAONO na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, yamewezesha kuanzisha Programu ya Kielelezo “Jenga Kesho Iliyo Bora” BBT – LIFE kwa ajili ya kuwezesha vijana kupata elimu ya vitendo katika unenepeshaji wa mifugo na viumbe vya kwenye maji

Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia imefanikisha kuanzisha mafunzo ya unenepeshaji mifugo kwa vijana wanaopatiwa mafunzo kwa vitendo katika Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) wilayani Misungwi.

Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia imeamua kukuza sekta ya mifugo kupitia unenepeshaji wa mifugo ili wananchi waweze kufuga kibiashara na kwa tija zaidi.

Kupitia dira na maono ya Rais Dkt. Samia, Serikali imeonelea kuichangamsha Sekta ya Mifugo, kupitia unenepeshaji na ufugaji wenye tija, hivyo wizara kuja na programu ya Samia Ufugaji kwa Tija (SAUTI).

Dhamira ya Rais Samia ni kutaka kutengeneza matokeo chanya kwa vijana katika maendeleo yao. Hicho ni kielelezo wazi kwamba RaisSamia anataka vijana wachakarikaji, wenye kasi ya maendeleo.

Programu ya SAUTI ambayo imeanzishwa kutokana na maelekezo ya Rais Samia, aliyotoa wakati wa kuhitimisha sherehe za wakulima (Nanenane) Mwaka 2022, imelenga kuwabadilisha vijana kifikra kwa kuwapatia mbinu mbalimbali za ufugaji wa kisasa na kibiashara ikiwa ni pamoja na kuwaonesha fursa zilizo.

Kufuatia maelekezo hayo ya Rais Samia, Serikali tayari imetenga sh. Bilioni 4.4 katika programu ya vituo atamizi kwenye vituo vinane kote nchini kupitia Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifyugo Tanzania (TALIRI).

Hadi Machi mwaka huu ng’ombe 865 kati ya 900 walinunuliwa kwa ajili ya programu hiyo ambayo mpango wa mafunzo ni mwaka mmoja na kila kijana atapata fursa ya kunenepesha mifugo hususan ng’ombe katika mizunguko minne ya ng’ombe kumi 10 kwa kila mzunguko na faida itakayopatikana baada ya kuuza ng’ombe hao itatumika kama mtaji kwa ajili ya kijana mnufaika kwenda kuanzisha miradi kama hiyo.

Rais Samia Suluhu anawataka vijana wanaoshiriki programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), kuongeza kasi ya unenepeshaji wa ng’ombe kutokana na kuwepo kwa soko kubwa la nyama ndani na nje ya nchi.

Rais Samia alitoa wito machi, mwaka huu alipotembelea banda la unenepeshaji wa ng’ombe kupitia programu hiyo lililopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

“Wanangu soko la nyama ni kubwa mno hata wanyama hai kuna kipindi nchi za wenzetu huko wanataka, sasa wanyama wakuja kuwachukua ni hawa walioko kwenye mabanda yetu, lakini pia tuna soko ambalo hatuwezi kulisha mpaka nilizungumza na Waziri wa Zambia nikamwambia tuletee tuchanganye tupeleke kwa pamoja, ili Tanzania isikose hilo soko,”anasema Rais Samia.

Anasema wapo vijana wengi wakiwemo waliohitimu mafunzo ya JKT hawana kazi, hivyo programu hiyo ikihamasishwa itawezesha vijana wengi kujiajiri na kuongeza kipato chao na Taifa kwa ujumla na kuwataka vijana wanaoshiriki programu hiyo kutokata tamaa kutokana na changamoto wanazokabiliana nazo wanapotekeleza programu hiyo.

Anawapongeza wataalamu wa mifugo kwa kusimamia vizuri programu hiyo na kufanikisha maendeleo yaliyopatikana hadi sasa .

Hadi sasa vijana 240 wamepata mafunzo hayo kwa kushiriki katika hatua zote ikiwemo ya kujenga mabanda na kwenda minadani na kuchagua ng’ombe wazuri ambao wanaweza kunenepeshwa na namna hatua za unenepeshaji zinavyofuatwa.

Kupitia programu hiyo tangu siku ya kwanza kila kijana anajua idadi ya ng’ombe atakaowasimamia na kila anapowauza, ule mzunguko faida inayobaki ndiyo atakayoondoka nayo kuanzisha biashara yake.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, Programu inalenga kupanua zaidi program hiyo na kuishusha katika ngazi ya mkoa na wilaya ili ziweze kujiendesha pamoja na kuongeza kundi la vijana kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili wapate pia mafunzo hayo.

Waziri Ulenga anasema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia, imeahidi kuboresha zaidi sekta ya mifugo ili kuwawezesha wafugaji nchini kufanya ufugaji wenye tija.

Akizungumza kwenye katika Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi madume ya ng’ombe 36, aina ya boran Heifer kwa halmashauri ya Buchosa;Waziri Ulega alisema;

“Lengo la Serikali ni kuona vijana wanafanya uzalishaji wenye tija na baadaye kupata masoko mazuri.

Kupitia programu maalum ya Samia Ufugaji kwa Tija (SAUTI), serikali imefanikisha kuanzisha mafunzo ya unenepeshaji mifugo, ambapo vijana 70 walipatiwa mafunzo hayo kwa vitendo katika Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Wilayani Misungwi.”

Aliongeza kuwa kuwa Serikali imeanzisha vituo atamizi vya SAUTI ambapo mpaka sasa kuna vituo nane kwa ajili ya mafunzo ya ufugaji kwa vinana, ambapo wanafundishwa namna bora ya ufugaji wa kisasa ya kutengeneza mashamba ya malisho na upatikanaji wa mifugo bora.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega amesema programu hiyo imeleta mafanikio makubwa ambapo kampuni ya Heifer International imeunga mkono kwa kuwaunganisha na wadau wa vyombo vya habari vya mitandaoni kwa lengo la kuwawezesha vijana wanaonenepesha ng’ombe kuuza kwa njia ya mtandao.

Waziri Ulega ameongeza kuwa tayari Wizara ya Fedha imeanza mipango ya wa kuwaingiza vijana hao katika masoko ya kimtandao, badala ya kutegemea masoko ya minada ya vijijini, ili kuwasaidia kupata masoko ya kimataifa.

“Tumezungumza pia na benki yetu ya maendeleo ya kilimo TADB pamoja na benki nyingine ziamini katika ufugaji huu wa unenepeshaji mifugo,na kuanza kuwakopesha vijana wetu, Ili wapate mitaji,”amesema Waziri Ulega.

Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda anawataka Watanzania hususan vijana wanaopatiwa mafunzo ya unenepeshaji mifugo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambapo baada ya mafunzo hayo ya mwaka mmoja kila mmoja ataondoka na mtaji usiopungua sh. Milioni kumi kufanya ufugaji kibiashara.

Waziri Mkuu Mstaafu MPinda ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kumshauri Rais Kuhusu Utekelezaji wa Masuala ya Kilimo na Chakula, alitoa kauli hiyo mapema mwaka huu, wakati alipofanya ziara ya siku moja Mkoani Tanga, kutembelea vituo atamizi vya wizara hiyo vinavyotekelezwa kupitia Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa ajili ya kutoa mafunzo ya vitendo ndani ya mwaka mmoja kwa vijana juu ya unenepeshaji ng’ombe katika kipindi cha miezi mitatu.

Akiwa katika vituo hivyo kwa nyakati tofauti alisema ni vyema baada ya mafunzo vijana hao waliopo kwenye vituo atamizi vinane kwenye maeneo mbalimbali nchini kufahamika katika mikoa wanayotoka ili wakitafutwa watoe taarifa wametoa faida gani kwa wafugaji wengine, ambao watakuwa wamebadilika kibiashara.

Aliongeza kuwa ufugaji wa kibiashara ni muhimu kwa vijana hao kuzingatiwa kwa kutoa elimu waliyopata kwa wafugaji ya namna bora ya kuchagua mifugo minadani na kuipatia malisho bora vikiwemo vyakula vya ziada ili kuwanenepesha na kuuza kwa faida baada ya miezi mitatu.

“Kumbe kilimo hiki au ufugaji huu ni biashara kwa uhakika, ng’ombe uliyemnunua Laki Mbili unakuja kumnenepesha kwa miezi mitatu baadaye unakuja kumuuza Milioni Mbili kwa nini usihangaike nalo hili?, Mwaka mzima unaniachia Milioni kumi kwa nini nisifanye?” alisema Pinda

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Silinde alisema kuanzishwa kwa programu ya vituo atamizi ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan lengo likiwa ni kuboresha Sekta ya Mifugo kuwa ya kisasa na kuleta tija zaidi.

Aliongeza kuwa kijana atayakayemaliza pogramu ya unenepeshaji mifugo hususan ng’ombe itakayodumu kwa mwaka mmoja atapatiwa na serikali sh. Milioni Kumi za mtaji na kwamba fedha hizo siyo mkopo bali aende kujiendeleza katika ufugaji kibiashara.

Alitoa rai kwa Watanzania kumuunga mkono, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa anajihusisha na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja ili kuboresha maisha ya wananchi.

Naye Mwakilishi wa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Mifugo Dkt. Angello Mwilawa, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani alimwambia Pinda namna wizara ya Mifugo na Uvuvi inavyoshirikiana na taasisi nyingine za serikali ili vijana kupata mafunzo hayo kupitia mikopo pamoja na uwekaji wa miundombinu pamoja na rasilimali chakula cha mifugo kwa gharama za chini huku mmoja wa vijana wanaopatiwa mafunzo ya unenepeshaji ng’ombe, Happy Samson akisema mtaji atakaopata baada ya kumaliza mafunzo utamwezesha kuanza biashara ya mifugo kwa ufasaha kwa kufuata elimu ya vitendo aliyoipata.

Nao baadhi ya vijana wanapata mafunzo hayo wanasema wamejiwekea mikakati ya kufanya ufugaji wenye tija mara wakapomaliza mafunzo yao ambayo yanadumu kwa mwaka mmoja.

“Ni wakati wetu sasa kufikiria kujiajiri na hata kutoa mafunzo kwa wafugaji wengine wa asili ili wafuge kisasa na kuingia katika biashara ya unenepeshaji wa mifugo,” anasema kijana mmoja wapo anayenufaika na programu hiyo.

Mnufaika mwingine, ng’ombe Rest Gonja ,amasema hadi sasa programu hiyo imewaingizia faida ya zaidi ya sh. Millioni 74 kutokana na ng’ombe 6,55 waliowauza kati ya ng’ombe 2,400 waliowanenepesha.

***Kituo cha Kikulula

Aidha, vijana waliojiunga na programu ya BBT Mifugo. wanaoendelea na mafunzo ya unenepeshaji katika kituo cha Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Kikulula walianza kuonja matunda ya mafunzo hayo baada ya kuuza ng’ombe 310 waliowanenepesha kwa muda wa miezi mitatu.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ulega alipofika katika kituo hicho kilichopo Wilayani Karagwe, Mkoani Kagera.

Akiongea kwa niaba ya vijana wenzake, Salum Husidicheki alisema mpaka sasa wameshauza ng’ombe 310 ambapo awamu ya kwanza waliuza ng’ombe 150 na awamu ya pili wameuza ng’ombe 160.

“Wastani wa bei tulizofanikiwa kuuza ng’ombe wetu sio chini ya Laki sita na nusu (650,000) na katika mauzo hayo faida kwa kila ng’ombe haipungui Elfu tisini (90,000),” alisema Husidicheki.

Alitumia nafasi hiyo pia kumshukuru Rais Samia kwa kuwawezesha kupata fursa hiyo ya mafunzo wao kama vijana wa kitanzania kwani wanaamini kupitia mafunzo hayo wataweza kuwa na ujuzi wa ufugaji wa kibiashara na kukuza kipato chao.

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ulega, amewapongeza vijana hao kwa hatua hiyo ya kuanza kuuza mifugo kwani inaashiria kuwa tayari wameshaanza kupata ujuzi ambapo watakapomaliza mafunzo yao wanaweza kuendesha maisha yao kupitia biashara hiyo ya mifugo.
Alisema maono na dira ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuifanya hiyo programu ya BBT inaenea nchi nzima na vijana waingie katika uzalishaji wa mali kupitia rasilimali zilizopo hapa nchini.

“Tunataka nyie muwe mabalozi wa mabadiliko katika sekta ya mifugo kwa kwenda kutekeleza yale ambayo mmejifunza katika programu hii ili itusaidie kupata wafanyabiashara wengi wa mifugo nchini,”alisema Ulega.