Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara Balizi Dkt. John Simbachawene ameitaka Tume ya Ushindani (FCC) kuongeza nguvu ya kuwa na maafisa wa kudhibiti bidhaa bandia nchini katika Vituo vyao rasmi vya kuingizia bidhaa ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam, Tunduma, Holili , Tarakea na Namanga.
Balozi Dkt. Simbachawene aliyasema hayo jana Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara yake katika Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) ili kujifunza, kujua shughuli za Taasisi hiyo na kuweza kufahaminiana na watendaji wa Tume hiyo.
Balozi Dkt. Simbachawene alisema wamekuwa na vikao vya kujadili kuzungumzia suala la soko huru la biashara Afrika ambalo wapo katika hatua za mwisho na watakapoanza utekelezaji wa soko huru la bidhaa inamaana watakua wamefungua bidhaa kutoka nchi yoyote ya Afrika kuweza kuingia nchini Tanzania.
Kutokana na hivyo Balozi Dkt. Simbachawene aliitaka Taasisi hiyo kuhakikisha wanaweka nguvu kubwa bidhaa zinazoingia nchini zisiwe bidhaa feki.
“FCC tumejikita zaidi Dar es Salaam kutokana na kudhibiti bidhaa ambazo wingi wa bidhaa zinazoingia nchini tulikuwa tunajua zinaingilia katika bandari ya Dar es Salaam lakini kwasasahivi kutokana na biashara tunayotaka kwenda nayo ni kuwa na biashara ya soko huria kwahiyo itatulazimu kama nchi kuweza kuongeza udhibidi wa bidhaa ambazo hazipo katika viwango”
“Mbali na Bandari ya Dar es salaam tuna entry point katika mikoa yetu takribani nane hivyo bidhaa zinazoingia nchini sasa si zitakazokuwa zinazoingia katika Bandari ya Dar es Salaam, Tunduma, Holili, Tarakea, na Namanga hivyo kama Taasisi tuna kila sababu ya kuongeza nguvu ya kuweza kuwa na maafisa kwaajili ya kutoa nguvu kubwa zaidi katika kudhibiti bidhaa bandia kuingia nchini na kuwa na maafisa katika maeneo hayo.”
Pia aliishauri FCC kuongeza nguvu katika kutekeleza majukumu yao ili kuweza kudhibiti vizuri zaidi bidhaa feki na kuwalinda walaji na kulinda uchumi kwa ujumla.
“Tunapowalinda walaji tunajilinda na sisi ambao tunatumia bidhaa na tunalinda uchumi kwa maana ya kwamba tunapofungua soko ushindani utakua mkubwa, bidhaa zitatoka Uganda, Kenya, Malawi hivyo bidhaa hizo kama tusipokuwa na tume ya FCC iliyokuwa imara tutajikuta bidhaa za Tanzania zinaweza kukosa soko”
Mbali na hayo aliitaka FCC kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo ili waweze kuelewa kwa undani kuhusu masuala ya bidhaa bandia na jinsi ya kuzidhibiti.
Aliwapongeza watumishi wote wa FCC kwa ujumla kwa kazi nzuri wanazozifanya kwaajili ya kuwalinda wananchi kupata bidhaa ambazo ni sahihi kwaajili ya matumizi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) William Erio aliishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia na baraza lake la mawaziri kuridhia kupitishwa kwa sheria ambayo wanaamini itawaletea ufanisi zaidi katika utekelezaji wa shughuli zao za kukuza na kushajiisha uchumi wa nchi kupitia biashara
“Tunaishukuru Serikali kupitia Bunge kwa kupitisha marekebisho ya sheria ya FCC ambapo sheria iliyopo sasa ilianza kutumika mwaka 2003 na kufanyiwa marekebisho madogo mwaka 2019/ 2020-2021 ”
Erio alisema wao kama Tume ya muelekeo wao ni kuwa na wafanyakazi katika vituo vyote vya mipakani ili kuhakikisha kwamba bidhaa bandia haziingii na hazipitishwi nchini lakini pia hazizalishwi ndani ya nchi kwani sheria hairuhusu hali itakayowasaidia kuhakikisha kwamba wanatumia kwa ufanisi fursa inayotokana na kuwepo kwa soko huru la Biashara Afrika.
Taasisi ya FCC imeanzishwa kwa mujibu wa sheria na ni Taasisi ya Serikali ambapo wanaongozwa na sheria ya Ushindani na Alama za bidhaa.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua