March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

FCC yafungua Kliniki ya biashara kwa faragha

Na Penina Malundo,Timesmajira

Mamlaka ya Udhibiti wa Ushindani wa Kibiashara (FCC),imezindua klinic maalumu ya biashara inayotoa ushauri wa faragha kuhusu masuala ya ushindani wa kibiashara na ulinzi wa walaji.

Akizungumza katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam,Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Hadija Ngasongwa, amesema maonesho haya ni fursa muhimu kwa mamlaka hiyo kufikia zaidi ya washiriki 3,500 wa sekta mbalimbali za biashara kwa lengo la kuhamasisha ushindani wenye tija na mazingira bora ya uwekezaji nchini.

“FCC imefungua kliniki ya biashara ili kuwawezesha wafanyabiashara hasa wale wadogo na wa kati kupata taarifa sahihi kuhusu sheria za ushindani na haki za walaji kwa faragha kabisa,” amesema Ngasongwa.

Amesema FCC imekuwa ikifanya kazi ya kuelimisha umma, kufuatilia mienendo ya soko, pamoja na kudhibiti bidhaa bandia zinazohatarisha afya za walaji na kuathiri ushindani halali wa kibiashara

” Serikali kupitia FCC imeweka mazingira rafiki ya kufanya biashara, jambo linaloendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, Tanzania bado ni mahali salama na bora pa kuwekeza kutokana na mfumo thabiti wa kisheria unaolinda haki za wafanyabiashara wote.

“Sheria zetu ni rafiki kwa wawekezaji, na tunajivunia kuona kwamba sasa Serikali imeweka mazingira mazuri zaidi kwa biashara kushamiri,” amesema

Akitaja dhamira ya FCC ni kuhakikisha siyo tu wawekezaji kutoka nje wanafaidika na mazingira ya biashara, bali pia wajasiriamali wa ndani wapate nafasi ya kukuza mitaji yao kupitia ushindani wa haki.

“Tunaamini kuwa kupitia elimu na usimamizi madhubuti wa ushindani, tunaweza kuwawezesha wafanyabiashara wa kati kukua na kuwa wawekezaji wakubwa wa baadaye,” amesema