January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

FCC yaagizwa kuboresha huduma udhibiti na usimamiaji mikataba

Judith Ferdinand na Daud Magesa, TimesMajira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa bado yapo malalamiko kutoka kwa watumiaji wa huduma za fedha kutokana na vipengele kandamizi kwenye mikataba wanayoingia na watoa huduma za kifedha nchini.

Kutokana na changamoto hiyo, Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji,ameielekeza Tume ya Ushindani(FCC)ijipange zaidi katika kuboresha utoaji huduma za udhibiti na usimamiaji wa mikataba ya mtumiaji.

Dkt.Kijaji ametoa maelekezo hayo wakati akifungua kongamano la wadau katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Haki ya Mtumiaji Duniani,yenye kauli mbiu “Kumlinda Mtumiaji Katika Huduma za Fedha Kidijitali”,lililofanyika mkoani hapa kitaifa.

Amesema,kwa mantiki hiyo,tume ina kazi kubwa ya kufanya kuwaelekeza wajipange zaidi katika kuboresha utoaji huduma za udhibiti na usimamiaji wa mikataba ya watumiaji.

Pia wahakikishe wanarahisisha utaratibu wa uwasilishaji na usajili wa mikataba hiyo kwa kutumia mifumo ili waweze kuwahudumia watoa na wapokea huduma wengi zaidi nchini na kwa urahisi.

“Maboresho hayo yahusishe kuboresha kanuni za udhibiti wa mikataba ili kuhusisha huduma za fedha mtandaoni na biashara mtandao, kama inavyoelekezwa katika kanuni za Umoja wa Mataifa za kumlinda mtumiaji (UNGCP), toleo la Mwaka 2015,”amesema Dkt.Kijaji.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) Godfrey Machimu, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa FCC William Erio, amesema siku ya Haki za Mtumiaji Duniani huadhimishwa kote ulimwenguni na Mamlaka ya Ulinzi wa Watumiaji ili kuhamasisha wadau wote wa soko juu ya umuhimu wa kuzingatia haki za watumiaji kama juhudi za kuimarisha ulinzi wa watumiaji.

“Siku ya Haki za Mtumiaji Duniani (WCRD) ni siku maalum iliyotokana na harakati za taasisi huru ya utetezi wa haki za mtumiaji ijulikanayo kama Consumers International (CI) ili kuadhimisha uanzishwaji wa Haki za Mtumiaji duniani zinazokubalika kote mnamo Machi 15, 1962,ni fursa ya ukuzaji haki za msingi za watumiaji Tanzania Bara,” amesema Machimu.

Pia amesema, kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu imelenga kuendesha kampeni ya ulimwengu ya kusimamia huduma za kifedha kidijitali zilizobuniwa mahususi kukidhi mahitaji ya mteja,zilizo salama na zinazozingatia uboreshwaji wa data na faragha,jumuishi na endelevu.

“Kauli mbiu hiyo inawaongezea watu maarifa mapya ya kuwa teknolojia za kidijitali zinaboresha ufanyaji malipo,ukopeshaji,bima na usimamizi wa mali kila mahali, zinaendelea kuwa kichocheo kikuu cha watumiaji wa huduma za kifedha,”amesema.

Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji,akizungumza wakati akifungua kongamano la wadau katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Haki ya Mtumiaji Duniani,yenye kauli mbiu “Kumlinda Mtumiaji Katika Huduma za Fedha Kidijitali”,lililofanyika mkoani hapa kitaifa.picha na Judith Ferdinand
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) Godfrey Machimu, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa FCC William Erio, katika kongamano la wadau katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Haki ya Mtumiaji Duniani,yenye kauli mbiu “Kumlinda Mtumiaji Katika Huduma za Fedha Kidijitali”,lililofanyika mkoani hapa kitaifa.picha na Judith Ferdinand
Baadhi ya washiriki wa kongamano la wadau katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Haki ya Mtumiaji Duniani,yenye kauli mbiu “Kumlinda Mtumiaji Katika Huduma za Fedha Kidijitali”,lililofanyika mkoani hapa kitaifa.picha na Judith Ferdinand
Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji( wa tatu kutoka kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa kongamano la wadau katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Haki ya Mtumiaji Duniani,yenye kauli mbiu “Kumlinda Mtumiaji Katika Huduma za Fedha Kidijitali”,lililofanyika mkoani hapa kitaifa.picha na Judith Ferdinand