November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Fao la upotevu wa ajira na mifuko ya hifadhi ya jamii

Na Christian Gaya

FAO la Upotevu wa Ajira limo kwenye sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ya mwaka 2018 na kwenye Mfuko wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Agosti Mosi, mwaka 2018, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ulianza rasmi ukiwa ni utekelezaji wa Sheria Namba 2 ya 2018, ambayo pamoja na mambo mengine, iliunganisha mifuko ya pensheni minne ya PSPF, LAPF, PPF na GEPF na kuunda mfuko mmoja kwa ajili ya watumishi wa umma yaani PSSSF.

Sambamba na kuanzishwa kwa PSSSF, sheria hii ilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Sura ya 50 ili kuufanya mfuko wa NSSF kuwa utakaohudumia wafanyakazi wa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi.

Ili kukabiliana na tatizo hilo la wanachama kujitoa katika mifuko hii ya hifadhi ya jamii pamoja na kukidhi mahitaji ya mfumo wa hifadhi ya jamii wa kuwa na utaratibu wa kinga ya kipato kutokana na upotevu wa ajira, Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) wakati huo kabla ya kuvunjwa rasmi, ilikuja na mapendekezo ya kuanzishwa kwa fao la upotevu wa ajira.

Fao hili la upotevu wa ajira litatolewa kwa wafanyakazi ambao ni wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii pale wanapopoteza ajira zao.

Fao hili linatokana na mchango wa pensheni wa mwanachama kumwezesha kujikimu katika kipindi anachotafuta ajira nyingine.

Ikitokea mwanachama huyo hajapata ajira nyingine miezi 18 baada ya kupokea malipo ya kutokuwa na ajira basi atatakiwa kubadili michango yake kwenda mpango wowote wa kuchangia kwa hiyari aupendao.

Kiwango kinachohamishwa kwenda mpango huo kinakuwa jumla ya michango yote kutoa pensheni aliyolipwa kipindi cha kukosa ajira. Mwanachama huyo ataendelea kuchangia mpango aliouchagua kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazousimamia.

Utaratibu wa fao la kukosa ajira linawahusu wale wanaofanya kazi za muda mfupi au za mkataba pia.

Wafanyakazi wanaopoteza ajira wameanza kunufaika na fao la upotevu wa ajira katika mifuko ya hifadhi ya jamii baada ya mifuko hiyo kutangaza kuanza kupokea maombi tangia mwaka mwanzoni 2019.

Tunafahamu kwamba fao la kukosa ajira halitolewi kama msaada, bali lipo kwenye sheria mpya ya mifuko ya hifadhi ya jamii na kuunganishwa kwa baadhi ya mifuko hiyo, hivyo wana haki kabisa ya kulipwa kama ilivyoelekezwa.

Fao la upotevu wa ajira ni jipya lililoanzishwa baada ya kuwapo kwa kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi kutaka kujitoa katika mifuko ya hifadhi ya jamii wanapoacha kazi.

Uanzishwaji wa fao hili unawezesha kutekelezwa na kuimarishwa kwa dhana ya hifadhi ya jamii kwa kuwajali wafanyakazi wanaopoteza ajira kwa kuwawekea kinga ya kipato itakayo wawezesha kupata fedha za kujikimu katika kipindi wanachotafuta kazi.

Faida nyingine kuwa ni kuondoa migogoro ya kikazi na malalamiko ya wafanyakazi yaliyopo kutokana na kuwepo utaratibu unaokubalika na hivyo kuongeza ari na tija sehemu za kazi.

Fao la upotevu wa ajira inaimarisha mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kupunguza matumizi ya fedha ya kuwalipa wanachama wanaoamua kujitoa kwenye mifuko bila sababu za msingi na kisha kuwa mzigo kwa jamii na serikali hapo baadaye.

Utaratibu huu hautakuwa na gharama kwa serikali kwa sababu fedha za malipo ya fao la upotevu wa ajira zitatokana na michango ya pensheni ya mwanachama mwenyewe.

Kabla ya fao hili jipya, kilio cha wafanyakazi wengi waliokuwa wanapoteza kazi ilikuwa ni kujitoa katika mifuko ya hifadhi ya jamii kiasi cha kuwapo kwa dhana kwamba lipo fao la kujitoa.

Hivyo, kutokuwepo kwa utaratibu mbadala wa kujipatia kipato mara baada ya kupoteza ajira kulisababisha baadhi ya wafanyakazi kudai kulipwa michango yao ya pensheni.

Kwa mujibu wa takwimu, wafanyakazi walio kwenye kundi la masharti ya ajira za kudumu ndio lina matukio mengi ya wanachama kujitoa.

Kwa mfano katika kipindi cha Julai 2016 hadi Disemba 2017, kati ya wanachama 23,000 waliojitoa kwenye Mfuko mmoja wa hifadhi ya jamii iliyokuwa sawa sawa na asilimia 78.3 sawa na wanachama 18,000, walikuwa wafanyakazi walio kwenye masharti ya kudumu.

Wafanyakazi 5,000 sawa na asilimia 21.7 walitokana na kundi la wafanyakazi walioajiriwa kwa mikataba ya muda mfupi na ambao hawana ujuzi mkubwa walioajiriwa kwenye mashamba, migodi na miradi mbalimbali ya muda mfupi.

Kanuni ya mpya mafao ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2018, imebainisha kuwa mafao ya upotevu wa ajira yatakuwa sawa na asilimia 33.3 ya mshahara wa mwezi wa mwanachama aliyepoteza ajira.

Sheria hiyo inautaka mfuko husika kushughulikia maombi ya mwanachama ndani ya wiki sita, baada ya kukamilisha atakuwa anapewa asilimia 33.3 ya mshahara wake wa mwisho kwa kipindi cha miezi sita.

Aidha, mafao haya yanatakiwa kulipwa kwa kipindi kisichozidi miezi sita kwa mwaka na mwanachama anatakiwa kulipwa kwa kipindi kisichozidi miezi 18 katika kipindi chote cha ajira.

Kama mwanachama atakuwa hajapata ajira baada ya miezi 18 anaweza kumwandikia mkurugenzi mkuu wa mfuko huo kuomba kuhamisha michango yake kwenda kwenye mfuko wa hiari wa chaguo lake na anaweza kuendelea kuchangia katika mfuko huo.

Mwanachama akiacha kazi kwa hiari yake hatapata mafao hadi atakapofikisha umri wa kustaafu kisheria. Atashauriwa kuendeleza uchangiaji wake akiwa kwenye ajira nyingine. Kama akiwa ameachishwa kwa sababu nyingine yeyote bila hiari yake, Mfuko utamlipa mafao ya kukosa ajira kwa kipindi cha miezi 6, mafao hayo yatasita endapo atapata kazi kabla ya kuisha kwa miezi hiyo sita.

lkipita miezi 18 baada ya kwisha kipindi cha kupata fao la kukosa ajira, mwanacharma anaweza kuomba michango yake kwenye mfuko kuhamishiwa kwenye Mfuko wa hiari. Michango itahamishwa baada ya kuondoa jumla ya fao la kukosa kazi. Fao la kukosa kazi litalipwa si zaidi ya mara tatu katika utumishi wote wa wanachama.