September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Familia ya Nyerere, MPC, MRPC kuanzisha Fimbo Day

Judith Ferdinand na Fresha Kinasa, TimesMajira Online, Butiama

KATIKA kuendelea kumbukumbu Mwalimu Nyerere, klabu ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Mwanza(MPC) na ya Mkoa wa Mara(MRPC) pamoja na familia ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere zimeazimia kushirikiana kuaanda na kuweka katika kumbukumbu ya maandishi yale aliyosisita baba wa Taifa sanjari na kuanzisha siku ya fimbo(fimbo day).

Endapo mambo hayo yataanza kufanyiwa kazi baada ya makubaliano itasaidia vijana ambao hawakujua historia yake maana tangu afariki Baba wa Taifa ni miaka 21 hivyo itasaidia kukumbushana na kuyaenzi yale aliokuwa anayasisitiza na kujenga historia kwa vizazi vijavyo.

Maazimio hayo yamekuja jana wakati waandishi wa habari kutoka Mikoa ya Mwanza na Mara walipokwenda kuzuru kaburi la Baba wa Taifa na kushiriki misa ya kumbukizi ya kifo chake Wilayani Butiama Mkoani Mara, ambapo mtoto wa Baba wa Taifa Madaraka Nyerere aliwaomba waandishi wa Klabu hizo kuandika kumbukumbu ya Mwalimu ili iwe ni kumbukizi kwa vizazi vyao huku akiwahimiza vijana kusoma historia ya Mwalimu na ya nchi.

Madaraka amesema, ni miaka 21 tangu Baba wa Taifa afariki hivyo kuna vijana wakati huo ndio walikuwa wanazalisha na hawaufahamu vizuri historia yake,hivyo kuputia waandishi wa habari wakiandika historia yake itasaidia vijana hao kuifahamu na hivyo fikra zake na mambo ambayo alisisitiza ikiwemo amani,umoja kwa maana ya kulinda muungano yataendelea kufuatwa.

“Kwa miaka 21 ni umri wa mtu mzima inawezekana kuna watu walizaliwa wakati anafariki,kwaio kuna vijana wengi ambao hawamfahamu mwalimu Nyerere sasa nitoe wito kwa vijana kusoma historia ya Mwalimu na ya nchi hii,na wafahamu hasa alikua kiongozi wa namna gani,alisimamia nini,aliamini juu ya nini, na katika kumuenzi Baba wa Taifa kumuandalia kumbukumbu ili vijana amabo hawakumkuta wamsome na kumuelewa zaidi na kuyaenzi yale aliyokuwa anayafanya,” amesema Madaraka.

Pia Madaraka ametumia fursa hiyo, kwa sababu taifa lipo kwenye mfumo wa vyama vingi basi wajaribu kutumia mawazo ya Baba wa Taifa kuhusu namna gani tunaweza kuishi katika mfumo huo,kwani alikua anasema mfumo huo ni sehemu ya kusikiliza mawazo mbalimbali,sera na mitazamo ya masuala mbalimbali ili wapiga kura waende kusikiliza na kupiga kura ya kumchagua kiongozi ambaye atakidhi matakwa ya wananchi.

“Nyerere alisema tupingane ila tusipigane,tukubaliane tu kama kiongozi wako ajachaguliwa mwaka huu basi,tusubilie miaka mitano ijayo wakati wa uchaguzi,tukubaliane kwenye tofauti yetu lakini tuhakikishe katika kutofautiana tunalinda amani yetu na Umoja wetu,” amesema Madaraka.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara, Robinson Wangaso amesema, klabu ya Mara na ya Mkoa wa Mwanza(MPC) watashirikiana kuandaa kwa kuweka katika maandishi mambo muhimu aliyoyasisitiza Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake pamoja na kuandaa maadhimisho ya siku ya fimbo kutokana na Mwalimu kuwa anafimbo wakati wa uhai wake.

“Tutashirikiana na Edwin Soko Mwenyekiti wa Mwanza Press klub kwa kushauriana na Madaraka na familia ya Mwalimu Nyerere kuanzisha kifimbo day( siku ya kifimbo) siku hiyo ambayo wanaume wote watahimizwa kutembea na fimbo kumuenzi Mwalimu ili kuendelea kumuenzi bila ya kusubilia siku ya kumbukizi ya kifo chake” amesema Wangaso.

Mwenyekiti wa MPC Edwin Soko amesema, waandishi wa habari katika Mikoa ya Mwanza na Mara watashirikiana kutafuta fursa ili kufanikisha azma ya kuandaa documentary ya Mwalimu kwa kutumia wanafamilia na watu walioshi na Mwalimu Nyerere wakati akiwa hai.

Ofisa Tarafa ya Makongoro Wilayani Butiama, Wakili Frank Rumishankya amesema, kutembelea katika kaburi la baba wa Taifa ni bure lakini kwenye makumbusho yake utalipia kwa gharama ndogo,ambapo watanzania bado hawana muamko wa kutembelea eneo hilo na kujifunza vitu mbalimbali vinavyohusika na historia ya mwalimu Nyerere wengi wao ni wanafunzi pia wanapokea watu kutoka maeneo ya nchi za jirani ikiwemo Kenya.

Rumishankya ametoa wito kwa watanzania kumuenzi baba wa Taifa kwani alisisitiza sana amani na katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi nguzo muhimu ya kuzingatia ni amani ya nchi na wananchi watembelee maeneo hayo kwani ni sehemu ya watanzania wote na ni sehemu ya kujifunza na kujivunia.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Butiama, wamesema wanacho kitaka kwa sasa historia ya Mwalimu Nyerere ndio itungwe zaidi ya mwaka 75 na ifanye kazi katika suala la uongozi ikiwemo kusimamia haki za binadamu,kuelimisha watanzania na aliondoa ukabila,ubaguzi katika elimu na dini.