Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline,Dar
WAKATI akikabidhiwa kijiti Machi, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alisitiza dhamira yake ya kuijenga Tanzania moja yenye ustawi kwa wananchi wote.
Na mara zote wito wake umekuwa kutaka kujenga jamii yenye maelewano, umoja na mshikamano, uzalendo, maridhiano, ustahamilivu na yenye uchumi unaokua kwa wote.
Falsafa yake ya 4R yaani maridhiano, ustahamilivu, mageuzi na kujenga upya sasa imeanza kueleweka kwa wadau wa demokrasia nchini.
“Tutajitahidi kuijenga Tanzania yenye haki, demokrasia na usawa na mafanikio na ndiyo maana katika kipindi hiki tulikuja na ‘idea’ nne (akimaanisha maridhiano, ustahamilivu, mabadiliko na kujenga upya)…vyama vya siasa tunazungumza, tunaelewana,” alisema Rais Samia katika moja ya mikutano yake.
Kueleweka kwa falsafa hizo kulidhihirika hivi karibuni wakati wa mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa uliofanyika Dar es Salaam, ambapo 4R ilikuwa moja moja ya mada iliyojadiliwa.
Katika mkutano huo uliokuwa ukijadili miswada ya sheria za uchaguzi na muswada wa sheria ya vyama vya siasa, wadau wa demokrasia wanakiri 4R za Rais Samia zimeleta mabadiliko.
Makala haya yanaangazia mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia katika uwanja wa kisiasa na namna wadau walivyoelewa falsafa yake ya 4R.
Itakumbukwa miaka sita iliyopita kulikuwa na tofauti za kisiasa zilizosababisha kutokuwa na majadiliano baina ya chama tawala na vya upinzani lakini tangu Rais Samia aingie madarakani mazungumzo yanafanyika.
Rais Samia amefungua ukurasa mpya wa siasa na demokrasia lakini kubwa ni fursa ya maridhiano ambayo yanaendelea mpaka sasa.
Dhamira yake ya kukutana na vyama vya siasa, mtu mmoja mmoja inatafsiriwa na wadau mbalimbali wa demokrasia kuwa inaleta faraja kwa wengi.
Rais Samia pia alitangaza kuruhusu kufanyika kwa mikutano ya kisiasa ya hadhara ambayo ilipigwa marufuku tangu mwaka 2016.
Aidha katika kuendelea kushughulikia masuala yanayohusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa, Rais Samia alielekeza kuundwa kwa kikosi kazi ambacho kilipokea maoni na mapendekezo kisha kupendekeza mabadiliko yanayoweza kufanywa kuelekea mwaka 2025.
Kikosi kazi hicho kilichokuwa kikiongozwa na Profesa Rwekaza Mukandala, kilijumuisha viongozi wa serikali, asasi za kiraia, wasomi na viongozi wa vyama vya kisiasa.
Kilifanyia kazi maeneo tisa, mikutano ya hadhara na mikutano ya ndani ya vyama vya siasa, masuala yanayohusu uchaguzi, mfumo wa maridhiano ili kudumisha haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa.
Maeneo mengine ni ushiriki wa wanawake na makundi maalumu katika siasa na demokrasia ya vyama vingi vya siasa, elimu ya uraia, rushwa na maadili katika siasa na uchaguzi, ruzuku ya Serikali kwa vyama vya siasa, uhusiano wa siasa na mawasiliano kwa umma na suala la katiba mpya.
Mpendekezo kadhaa ya kikosi kazi hicho yanaendelea kufanyiwa kazi.
Pia chini ya utawala wake Rais Samia alielekeza kupitiwa mienendo ya baadhi ya kesi nchini pamoja sheria zilizoonekana kuwa na ukakasi na kuzifanyia marekebisho.
Kutokana na hatua hiyo watu zaidi ya 400 waliokuwa mahabusu kwa kesi zisizo na ushahidi waliachiwa huru, wakiwamo viongozi wa Uamsho waliokaa mahabusu kwa miaka minane wakituhumiwa kwa ugaidi.
Rais Samia alitangaza nia yake ya kuhakikisha Tanzania inachangamana na jumuiya ya kimataifa na kuihakikishia dunia kuwa Tanzania haitajifungia, itayapa kipaumbele mashirikiano ya kiuchumi na kimaendeleo.
Ameendelea kutembelea nchi mbalimbali na kuhudhuria vikao vya wakuu wa nchi mbalimbali ukiwamo mkutano wa 76 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa.
Hatua ya kurejesha uhusiano wa kimataifa baina ya Tanzania na mataifa mengine duniani imewezesha kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo mkopo wa Sh trilioni 1.3 wa masharti nafuu uliotolewa na IMF kwa ajili ya mapambano dhidi ya Uviko-19.
Fedha hizo zimetumika katika miradi mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa madarasa ya shule za msingi na sekondari, ununuzi wa vifaa tiba na miradi ya ujenzi wa miundombinu ya maji safi na salama.
***WADAU WA DEMOKRASIA WANAVYOMZUNGUMZIA
Wadau mbalimbali wa demokrasia wameonesha namna 4R zilivyoleta mabadiliko nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Zanzibar, Salum Mwalimu, anasema 4R zinajenga misingi ya kuvumiliana kwa hoja ili kufika kwenye ujenzi wa Tanzania mpya.
“Rais alichukua nchi katikati ya mawimbi makubwa, tulitoka katika uchaguzi uliozaa taharuki kubwa ndani na nje. Rais aliona tunahitaji kurejea kwenye mstari, aliona haja ya kuzungumza kama taifa na kutuunganisha Watanzania,” anasema Mwalimu.
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT – Wazalendo, Ado Shaibu, anasema 4R zitazamwe kwa muktadha zaidi kwani zikitekelezwa kwa ukamilifu taifa litakwenda sambamba na malengo ya dunia.
“Rais hakuwa na presha yoyote ya kisiasa lakini alitukuta tuko hoi, lakini kwa uungwana na hekima zake aliona bado taifa linahitaji 4R, kwa hilo tunampongeza sana…4R itapimwa kwa vitendo hivyo wadau wote tunayo kazi kubwa ya kufanya,” anasema Ado.
Mwanasiasa Mkongwe, Dkt. Getrude Mongela, anasema Rais Samia ameleta misingi ambayo itasaidia hasa wakati huu wa kutengeneza dira ya taifa na kushauri elimu iendelee kutolewa ili umma uzielewe 4R.
“4R zisiwe za mama Samia peke yake, ziwe za Watanzania wote, elimu itolewe huku tukizingatia pia matumizi ya lugha kwa sababu kuna watu wasomi na wasiosoma bado hawajajua 4R,” anasema Dk. Mongela.
Mwanasiasa Stephen Wassira, anasema; “Nimemuelewa zaidi Rais Samia na falsafa yake ya 4R, tunaendelea kuwa na mfumo wa vyama vingi, tofauti zetu hazivunji umoja wa kitaifa hivyo, kuaminiana kunahitajika zaidi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Doyo Hassan, anasema watendaji wa Serikali wanapaswa kuzielewa 4R za Rais Samia na kushauri yatengenezwe mazingira ya kuhakikisha falsafa hizo zinatekelezwa kwa vitendo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenister Mhagama, anasema Rais Samia ameanzisha utaratibu shirikishi wa watu kusikilizana ambao umeleta mabadiliko makubwa.
“Vyama viendelee kuzingatia falsafa ya 4R ili kuleta mageuzi ya mfumo wa demokrasia nchini,” anasema Waziri Mhagama.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia