Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Fainali ya msimu wa 13 wa Shindano la Startimes Bongo Star Search (BSS) zinatarajiwa kufanyika Februari 4, 2023 huku mshindi akitarajiwa kuondoka na kiasi cha fedha Tsh. Milioni 20/-.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Startimes, David Malisa amesema kuwa wanaunga mkono vijana na kuhakikisha kuwa pamoja na Serikali chini ya Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) za kukuza Sanaa ya Muziki kwa vijana nchini.
Malisa amesema Startimes imekua ikishirikiana na Benchmark Production kwa kipindi kirefu kuvumbua vipaji vya muziki vilivyojificha na kuhakikisha vinatambulika kwa umma.
“Kampuni ya Startimes kupitia Chaneli ya ST Swahili imekua ikionyesha mashindano haya kwa uzuri na weledi mkubwa sana, safari hii ni kali sana na balaa zaidi ni fainali ya Februari 04, 2023 katika ukumbi wa Superdome Masaki jijini Dar es salaam,” amesema Malisa.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Benchmark 360 ambae pia ndio Jaji Mkuu wa Shindano hilo, Rita Paulsen amesema wamekuwa na msimu 12 lakini msimu huu wa 13 umekuwa na tofauti zaidi na misimu yote kwani washiriki wamepata nafasi ya kazi zao kuwepo kwenye Mtandao wa Kimataifa wa kupakua nyimbo wa Boomplay.
“Msimu huu ni wa tofauti haijawahi kutokea kwani kulikuwa na Majaji ambao ni mastaa wakubwa akiwemo Rayvan,Nandy, Jux na wengine wakali ambapo walifanya mchujo wa hali juu bila upendeleo wowote,” amesema Ritha.
Aidha, amesema malengo ya msimu huu ni kuwajenga na kuwawezesha vijana kuwa mastaa wakubwa, kuwapa fursa ya kurekodi nyimbo zao wenyewe huku wakinufaika binafsi kupitia kazi hizo walizoandaa.
Kwa mujibu wa Paulsen Mshindi wa kwanza atapata kiasi cha fedha Tsh. Milioni 20, Mshindi wa pili atapata Tsh. Milioni tatu na Mshindi wa tatu atapokea Tsh. Milioni moja, hata hivyo zawadi hizo tayari washiriki 8 wamepata nafasi ya kurekodi nyimbo zao pamoja na kufanya video kwa watayarishaji nguli na wabobezi wa Muziki.
More Stories
Startimes yazindua makala ya China, Africa
Mwanasheria wa Katavi aliyetimkia kwenye muziki achaguliwa tuzo za MIEMMA
Coca-cola ‘Kitaa Food Fest’ yahitimishwa kwa mafanikio