Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma
NYOTA wa kimataifa wa Tanzania katika mchezo wa riadha, Failuna Matanga na Gabriel Geay wameapa kuadhika rekodi mpya dhidi ya wanariadha wa Kenya, Uganda na Malawi katika mbio za mbio za Kimataifa za NBC Marathon zinazotarajiwa kufanyika Novemba 22.
Failuna na Geay watakimbia mbio hizo baada ya kufanya maandalizi ya muda mrefu wakijiandaa na mashindano ya kimataifa ya riadha ambapo Failuna alikuwa anatarajiwa kwenda India katika mbio za New Dehil wakati Geay anatarajia kushiriki mbio za Valencia zitakazofanyika Desemba 6 baada ya kukwama kwenda nchini Poland kwa ajili ya kuiwakisha nchi katika mashindano ya Dunia ya riadha ya ‘World Half Marathon’ yaliyofanyika Oktoba 17.
Katika mbio hizo zinazotambuliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa ‘World Athletics’ zamani IAAF na Chama cha Kimataifa cha Marathon (AIMS), inaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) zinatarajiwa kushirikisha washiriki 3,000.
Tayari wanariadha mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wameshaanza kuwasili jijini Dodoma tayari kwa mashindano hayo huku wakitamba kufanya vizuri na kuwagaragaza washindani wao.
Hadi sasa wanariadha kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini wakiongozwa na Sara Ramadhani kutoka Arusha ambaye amekuwa akifanya vizuri katika mbio za Kilomita 42 ‘Full Marathon’ wameshawasili huku akijinasibu kuhakikisha bendera ya Tanzania inang’ara na kukata ngebe wapinzani wao kutoka Kenya.
Wanariadha wengine wa Tanzania walioahidi kufanya vema ni pamoja na Hamis Misai, Jafar Rajab kutoka Singida ambao wote wamejitosa kuwania mbio za Kilomita 42.
Lakini shughuli pevu katika mbio hizo inatarajiwa kuwa kwenye Kilomita 21 ‘Half Marathon’ ambako wakali wengi wamejitosa akiwemo Failuna ambaye tayari amefuzu kwa Olimpiki ya Tokyo, Geay, Angelina Tsere na Ezekiel Ngimba huku Grace Jackson kutoka JKT Arusha akiahidi kuendeleza makali yake kwenye Kilomit 10.
Pia mmoja wa wanariadha kutoka Kenya Joan Jerop Massah ametamba kufanya vema katika mbio za Kilomita 21 ‘Half Marathon’ na kuondoka na zawadi nono zilizoandaliwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).
Wanariadha wengine kutoka Kenya ni Judith Cherono na Esther Chesang Kakuri (Km 21),
Euliter Jepchirchir Tanui (Km 24), Isgah Cheruto, Rubein Kipkemboi, Abraham Kipkosgei Too na Wilson Kiprop Tuitoek (Km 42) wakati Edward Kibet Kiprop na Elijah Kibiwot Cheruiyot wakikimb ia kilometa 21.
Kutoka Uganda wapo Philip Kiplimo na Vincent Chelimo watakaokimbia kilometa 42 huku
Doreen Chemutai, Julius Ochieng na Melly Chelimo wakikimbia kilometa 21 wakati wanariadha kutoka Malawi wakitarajia kuwasili leo.
Katika mbio hizo mshindi wa kwanza kwa Mbio za Kilomita 42 kwa upande wa wanaume na wanawake ataondoka na kitita cha Sh. 3,500,000, mshindi wa pili atajinyakulia kitita cha Sh. 2,500,000 wa tatu atapata Sh. 1,500,000, wa nne Sh. 1,000,000 huku wa tano akijitwalia Sh. 750,000 wakati watakaoshika nafasi ya sita hadi kumi kila mmoja ataondoka na Sh. 500,000.
Kwa upande wa Kilomita 21 mshindi atajipatia Sh. 2,500,000, wa pili 1,500,000 wa tatu 1,000,000, Sh. 750,000 kwa msindi wa nne na Sh. 500,000 kwa mshindi wa tano huku wale watakaoshika nafasi ya sita hadi kumi wakiondoka na Sh. 300,000 kila mmoja.
Mbio za Kilomita 10 mshindi atajitwalia kitita cha Sh. 1,000,000 wa pili Sh. 750,000 wa tatu Sh. 500.000 wa nne Sh. 250,000 wakati wa tano atajishindia Sh. 200,000 wakati wa sita hadi kumi wakijipoza na Sh. 100,000.
Kwa upande wa mbio za kujifurahisha za Kilomita 5, washiriki wote watakaofanikiwa kumaliza watajipatia medali.
Ada kujisajili ni Sh. 25,000 ambapo usajili unaendelea katika matawi ya NBC, Shoppers Plaza jijini Dodoma na Mlimani City Dar es Salaam na kila atakayejisajili atapata fulana maalumu ya kukimbilia.
Mbali na kujenga afya na kuutangaza zaidi mchezo wa Riadha, NBC Marathon pia inalenga kusaidia jamii yenye uhitaji, ambapo kwa mwaka huu mapato yote yatakayopatikana kupitia usajili yatapelekwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kusaidia akina mama wanaosumbuliwa na kansa ya shingo ya kizazi.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025