January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Fahamu umuhimu wa ziara ya Rais Dkt. Samia nchini Uturuki

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

KWA kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, Rais Samia Suluhu Hassan, amedhihirisha kwamba anaaamini katika kujenga na kudumisha mahusiano ya kidiplomasia na mataifa na jumuia zingine, ambapo mahusiano hayo yamekuwa na fursa na faida nyingi.

Hilo lilionekana dhahiri kwani tangu ameingia madarakani uhusiano wa Tanzania na mataifa mengine umeimarika, ambapo umesaidia kufungua fursa mbalimbali katika nyanja za kiuchumi, huku idadi ya wawekezaji ikiongezeka kwa kasi.

Kwa jinsi wawekezaji wanavyozidi kumiminika nchini sasa, Watanzania wengi wanaanza kutafakari kauli yake aliyoitoa kwamba Tanzania itakuwa sawa na Ulaya ndani ya miaka sita.

Rais Samia alitoa kauli hiyo baada ya kurejea nchini akitokea barani Ulaya alikokuwa na ziara ya kikazi katika nchi za Ufaransa na Ubelgiji.

Kauli iliyoibua mjadala mkubwa, ambapo wapo waliojiuliza itawezekanaje? Na wapo walioona inawezekana. Lakini hilo halizuii mtazamo wa namna ziara za Rais Samia zinavyoleta sura tofauti kwenye nyanja ya kidiplomasia na fedha za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Ziara za Rais Samia zimefungua milango ya mahusiano ya kidiplomasia, kiuchumi na kijami, milango ambayo ilifungwa kabla ya kuingia madarakani Machi, 2021.

Chini ya uongozi wa Rais Samia hakuna taasisi, taifa au mtu yeyote ambaye anaweza kuinyoshea kidole Tanzania kwa kutokuwa na mahusiano mazuri kidiplomasia na Jumuiya au nchi zingine.

Tangu aingie madarakani, Rais Samia amekuwa akifanya ziara mara kadhaa na kuhudhuria mikutano ya kimataifa ambayo huko nyuma, walitumwa wasaidizi au mabalozi.

Tumeshuhudia, faida kubwa ya Rais kufanya hivyo katika kipindi cha miaka mitatu.

Rais Samia anaaamini katika kujenga na kudumisha mahusiano ya kidiplomasia na mataifa na jumuia zingine. Hilo lilionekana dhahiri na matokeo ya kazi nzuri yanapimwa kwa idadi ya ziara zake nje ama amekutana na watu wangapi na zimeleta matokeo gani.

Kutokana na mazingira mazuri ya kisiasa imekuwa ni moja ya sababu ya nyingi kupenda kuleta mitaji yao kuwekeza nchi. Lakini pia Rais Samia, ameendelea kupata mialiko maalum kutoka kwa marais mbalimbali, ambapo ziara zake anazofanya zimekuwa na tija kubwa kwa taifa letu.

Mfano, kuanzia jana Rais Samia ameanza ziara nchini Uturuki kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdoğan.

Samia anakwenda ziara hiyo ikiwa ni miaka 14 imepita tangu Rais wa Tanzania alipotembelea nchi hiyo ikiwa ni miaka saba tangu Rais wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdogan alipotembelea Tanzania, Januari 2017.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, January Makamba, anasema Uturuki ni kati ya nchi zilizoweka msisitizo katika mahusiano yake na nchi za Afrika, jambo lililojenga muingiliano wa watu kati ya nchi hizi mbili.

“Wafanyabiashara wengi wa Tanzania wamekuwa wakienda kukununua bidhaa Uturuki na sisi tumekuwa tukiuza bidhaa nyingi huko, hivyo lengo la kwanza ni kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia, kibiashara na kisiasa kati ya nchi hizi mbili,” anasema Makamba.

Makamba anasema lengo la ziara hiyo pia ni kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kiuchumi kwani Tanzania inahitaji mitaji, teknolojia na wawekezaji.

“Tumeona kampuni nyingi kutoka Uturuki zinafanya kazi hapa nchini, Uturuki ni miongoni mwa nchi 20 zilizo na uchumi mkubwa duniani, hivyo kuwa nayo karibu tutanufaika kibishara na kiuwekezaji,” amesema Makamba.

Rais Suluhu Hassan (kulia)akizungumza na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinumwi Adesina pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) Ngozi Okonjo katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika (EU-AU)

Ushirikiano katika maendeleo pia ni moja ya jambo ambalo linaangaziwa, kwani nchi hiyo imekuwa ikiisaidia Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo maji, afya na elimu.

Makamba anasema mbali na Rais kufanya mazungumzo ya kiserikali na mwenyeji wake kupitia maeneo ya ushirikiano yaliyopo, pia yataangazia maeneo mapya ambayo yanaweza kutumiwa kati ya nchi hizo mbili.

“Baada ya kumaliza mazungumzo hayo, Rais Samia atakwenda mjini Instanbul ambao ndiyo mji wa kibiashara na huko limeandaliwa kongamano kubwa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki, ambalo litakutanisha wafanyabiashara wa pande zote,” anasema Makamba.

Baada ya kongamano hilo, Rais atakutana na kampuni kubwa 15 nchini humo kwa ajili ya kuzishawishi kuja kuchangamkia fursa zilizopo Tanzania.

“Kuna maeneo ambayo tunashirikiana nao yalitarajiwa kuwa maeneo zaidi ya 10, lakini hadi sasa tuna maeneo kama sita, ambayo yamethibitishwa kuwa tutasainiana mikataba na hati za makubaliano,” anasema Makamba.

Kati ya maeneo ambayo wanatarajia kuingia makubaliano Tanzania na Uturuki ni ufadhili wa masomo ya elimu ya juu.

Rais Samia akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya maandalizi ya mkutano wake na Diaspora nchini Norway

***Hali ya sasa

Uwekezaji wa kampuni za Uturuki Tanzania bara una thamani ya takribani dola milioni 414,23 za Kimarekani kwenye sekta za usafirishaji, uzalishaji na utalii ambao umetoa ajira 6,062.

Kwa Upande wa Zanzibar ,Uturuki imefanya uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 96.4 kwenye sekta ya utalii na kutoa fursa za ajira 719.

Katika upande wa Biashara na Utalii, Biashara kubwa Tanzania inayouza Uturuki ni kahawa, nazi, tumbaku ghafi, minogu ya samaki ,dhahabu,mchele na maharage ya soya ambapo huuza bidhaa zenye thamani ya wastani wa Dla za Marekani milioni 15.99 kwa mwaka.

Kila mwaka Serikali ya Uturuki hutoa udhamini kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Tanzania kusoma Uturuki kuanzisha shahada ya kwanza hadi shahada ya uzamivu,Udhamini wa vyuo vikuu vya Uturuki ni katika masomo ya Afya,Uhandisi ,Uchumi ,Biokemia,Famasia ,Kilimo na Sayansi ya Jamii.

Tanzania na Uturuki zina ushirikiano mkubwa kwenye sekta ya afya, ambapo Uturuki imekuwa ikitoa misaada ya vifaa vya kitabibu na idadi kubwa ya Watanzania hupata matibabu katika hospitali za Uturuki.