Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Dar
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewazawadia wahitimu wawili bora wa Chuo cha Maji, Florence Theonist na Emmanuel Nyaki, kompyuta mpakato na fedha taslimu milioni sita.Ambapo kila mmoja milioni 3,kama sehemu ya kutambua juhudi zao katika masomo na kuwahamasisha vijana wengine kujiunga na kozi zinazohusu masuala ya maji.
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso,amewakabidhi wahitimu hao, zawadi hizo wakati wa mahafali ya 48 ya Chuo cha Maji yaliyofanyika Novemba 13, 2024, jijini Dar es Salaam.
Florence Theonest, amehitimu Stashahada ya Uhandisi wa Ugavi wa Maji na Usafi wa Mazingira, na Emmanuel Nyaki, Stashahada ya Teknolojia ya Maabara ya Ubora wa Maji katika Chuo cha Maji.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA baada ya hafla hiyo, Mhandisi Mwandamizi wa Maji na Usafi wa Mazingira,David Linda,amesema lengo la zawadi hizo ni kuhamasisha vijana wengi kujiunga na kozi za sekta ya maji,ili kuwa na wataalamu wengi watakaosaidia kutoa huduma bora na kuchangia maendeleo ya sekta hiyo.
“Moja ya malengo endelevu ya dunia (SDGs) ni kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wote.Hili halitowezekana kama hatutakuwa na wataalamu wa kutosha. Ndio maana EWURA iko mstari wa mbele kushirikiana na Chuo cha Maji ili kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kufanikisha lengo hili,”amesema Linda.
Florence Theonest, mmoja wa wahitimu waliotunukiwa, ameishukuru EWURA kwa zawadi hiyo na kueleza kuwa kompyuta aliyopokea itamsaidia katika kazi za kiufundi, hasa ikizingatiwa kuwa shughuli nyingi za uhandisi wa maji zinategemea programu mbalimbali za kiteknolojia.
Kwa upande wake, Emmanuel Nyaki alitoa mwito kwa wanafunzi wanaosoma kozi zinazohusiana na sekta ya maji kuongeza juhudi katika masomo yao, akisisitiza kuwa ujuzi wa kitaalamu ni muhimu kwa maboresho ya sekta ya maji nchini.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote